Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati)
akizungumza na Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
wakati alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Buruhani Nyenzi na kulia ni
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Dkt. Hamza Kabelwa
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiy (hayupo pichani)
akiangalia picha za usafiri wa anga na majini ambazo usafiri wake
unategemea utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza
kushoto) akipatiwa taarifa ya hali ya hewa kwa usafiri wa anga na
Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa Bwana Samwel Mbuya wa Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania wakati alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini
Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani)
akiangalia picha ya ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendokasi ambapo
ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli unategemea utabiri wa hali ya
hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani)
akiangalia picha ya rada ya hali ya hewa iliyopo kwenye vituo vya
utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani)
akipatiwa maelezo na msomaji wa taarifa ya hali ya hewa kwenye vituo
mbalimbali vya televisheni Bi. Hellen Msemo kuhusu namna wanavyotoa
taarifa za utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
……………………
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameilekeza Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) kujitangaza umuhimu wake katika nyanja ya kiuchumi
na kijamii kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Mhandisi Nditiye ameyasema
hayo alipotembelea makao makuu ya TMA na kuzungumza na bodi ya Mamlaka
hiyo, menejimenti na wafanyakazi kwa lengo la kutambua majukumu yao na
kufuatilia utekelezaji wake ili kufikia malengo ya Serikali ya
kuwatumikia wananchi.
Akizungumza
na Bodi, menejimenti na wafanyakazi, Mhandisi Nditiye amewaeleza kuwa
TMA ni chombo muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa
letu na wananchi kwa ujumla kwa kuwa sekta ya usafiri wa anga, majini,
ujenzi wa majengo mbalimbali, miundombinu ya barabara na reli, afya,
kilimo na mazingira vyote vinategemea taarifa za hali ya hewa kutoka
kwenye Mamlaka hii. “Mtambue kuwa hakuna ndege inayoweza kutua wala
kuruka bila kupata taarifa kutoka kwenu, vile vile mkandarasi anayejenga
reli ya kisasa ya SGR nae anategemea taarifa zenu kwa kiasi kikubwa,
hivyo mtambue ninyi ni muhimu na mjitangaze,” amesema Mhandisi Nditiye.
Amesisitiza
kuwa ni vema mjitangaze ili wananchi na wadau mbalimbali wafahamu
majukumu na umuhimu wa taasisi yenu kwa kuwa uchumi wa taifa hili
unategemea taarifa zenu ambapo wananchi wengi wamezoea kusikia na
kuwaona mkitoa taarifa za tahadhari za hali ya hewa zinazohusiana na
majanga na matukio mengine yanayohusiana na utabiri wenu angali ninyi
mna taarifa muhimu zaidi na tofauti na mtazamo wa wananchi walio wengi.
Amefafanua
kuwa wananchi wanaziamini taarifa zenu za hali ya hewa kwa kuwa kwa
kiasi kikubwa yale mnayotabiri na kuwaeleza ndiyo yanayotokea iwe ni
mvua kubwa, upepo mkali au joto kali kama ilivyo sasa. “Nimetembea na
kukagua mitambo, vifaa vya kisasa na namna wanavyofanya kazi na
nimebaini kuwa taarifa zinazotolewa hapa zimekusanywa kutoka vituo mbali
mbali vya hali ya hewa nchini ambapo hapa makao makuu wataalamu
wanazichakata, kusambaza kwa wahusika na kuhifadhiwa, na zinaonesha kuwa
ni taarifa za uhakika kwa kiwango cha asilimia 87.5 ambapo imeongezeka
kutoka asilimia 82.1 kwa miaka mitatu iliyopita,” amesema Mhandisi
Nditiye.
Mwenyekiti
wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akiwasilisha taarifa yake
kwa Mhandisi Nditiye amesema kuwa Mamlaka hii ni muhimu kwa ustawi na
maendeleo ya taifa letu na wananchi kwa ujumla kwa kuwa utoaji wa
taarifa na huduma za hali ya hewa nchini zimewezesha uokoaji wa maisha
ya watu na mali zao; kuepuka au kupunguza athari na hasara
zinazosababishwa na matukio ya hali ya hewa; kuongeza tija na mafanikio
katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi; kuwa na
miundombinu imara kama vile barabara, madaraja; kuongeza ufanisi katika
sekta za usafiri na mawasiliano; kuchangia katika sekta za ujenzi na
uendeshaji wa viwanda nchini na kukuza pato la taifa.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Hamza Kabelwa amemueleza Mhandisi
Nditiye kuwa wahitaji wa taarifa za hali ya hewa kutoka kwa taasisi na
wadau mbalimbali ambao wanahitaji kwa ajili ya kutekeleza shughuli za
kiuchumi na kijamii wamekuwa wengi na teknolojia ya utabiri wa hali ya
hewa na utoaji wa taarifa zake umebadilika ambapo inatulazimu kuhuisha
Sheria Na. 6 ya Hali ya Hewa ya Mwaka 1978 na kukamilisha Sera ya Taifa
ya Hali ya Hewa ili ziweze kwenda na wakati pamoja na kuboresha chuo cha
Hali ya Hewa Kigoma kwa kuwa ndio chuo pekee nchini kinachotoa elimu ya
awali na ya kati ya hali ya hewa.
Ameongeza
kuwa TMA imepatiwa cheti cha ubora wa utoaji huduma na Shirika la
Viwango la Kimataifa (ISO) kwa kutoa huduma kwa sekta ya anga nchini.
Pia, inashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo ya nchi za Kusini mwa jangwa la Afrika (SADC), Shirika la
Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
kwa kubadilishana taarifa za hali ya hewa, mabadiliko ya hali ya hewa
yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa, na kuendeleza na kutunza mtandao
wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa ili kukidhi makubaliano ya
kimataifa ya kubadilishana taarifa hizo.
Dkt.
Nyenzi amemshukuru Mhandisi Nditiye na kumueleza kuwa TMA inafarijika
kusikia kuwa anafahamu kwa undani umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa
nchini, hivyo ni imani yake kuwa ataisamimia vema ili ifikie malengo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
SHARE
No comments:
Post a Comment