Na Hamza Temba-Dodoma
Serikali
imeanza utekelezaji wa mkakati wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii
nchini unaohusisha upanuzi wa maeneo ya kijeografia yenye vivutio pamoja
na mazao ya utalii ili sekta hiyo ichangie zaidi kwenye pato la taifa
na kuondoa umaskini katika jamii.
Hayo
yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao cha Bunge
kinachoendelea mjini Dodoma.
Mnyama aina ya twiga
Alisema
kwa upande wa mkakati wa kupanua jeografia ya vivutio vya utalii nchini
Serikali itafungua utalii wa ukanda wa kusini kwa kuboresha vivutio na
miundombinu ambapo tayari imesaini mkataba wa mkopo nafuu kutoka benki
ya dunia wa milioni 150 za kimarekani sawa na zaidi ya Shilingi bilioni
340 za kitanzania kwa ajili ya mradi wa REGROW ambao utasimamia
maliasili na kuendeleza utalii wa ukanda wa kusini.
Alisema
kupitia mradi huo jumla ya viwanja vya ndege 15 vitaboreshwa ndani ya
Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na uwanja wa
ndege wa Nduli uliopo mjini Iringa. Maeneo mengine yatakayoboreshwa
katika hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni Hifadhi ya Taifa
ya Udzungwa na Mikumi.
"Mradi
huo utaboresha pia usafiri wa reli kwa kuimarisha kituo cha Matambwe
ambacho ni kitovu cha utalii katika Pori la Akiba la Selous",. Alisema
Dk. Kigwangalla.
Akizungumzia
upanuzi wa mazao ya utalii, alisema sekta hiyo kwa muda mrefu imekuwa
ikitegemea zaidi utalii wa wanyamapori huku ukiegemea zaidi katika
ukanda wa kaskazini kwa zaidi ya asilimia 90.
Alisema
kwa sasa Serikali itapanua wigo wa mazao hayo ya utalii ambapo mwezi
Septemba kila mwaka utakuwa mwezi maalum wa maadhimisho ya urithi wa
Tanzania (Urithi Festival) kwa ajili kuimarisha utalii wa kiutamaduni na
kuhamasisha utalii wa ndani.
Alisema Serikali kupitia Wizara yake itaimarisha pia utalii wa fukwe na utalii wa mikutano.
Awali
Dk. Kigwangalla alisema sekta ya Utalii ina mchango mkubwa katika
uchumi wa taifa ambapo huchangia asilimia 17.6 ya pato la taifa,
asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni na asilimia 12 ya ajira
zote nchini.
Alisema
pamoja na mafanikio hayo sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi
ikiwemo uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi na kuegemea zaidi kwenye
vivutio vya ukanda wa kaskazini huku vivutio vya kanda nyingine vikiwa
havichangii ipasavyo kwenye pato la taifa.
SHARE
No comments:
Post a Comment