Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha bunge mjini Dodoma Februari 9, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imefanikiwa kurejesha mali tisa kati ya 10 za Chama
Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambazo zilichukuliwa kinyume cha
taratibu na kuagiza watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.
Amesema mali moja iliyobakia bado
inafanyiwa uchunguzi na mali mbili za Chama Kikuu cha Ushirika cha
Shinyanga (SHIRECU) nazo pia zimepatikana lakini bado ziko kwenye hatua
ya makabidhiano.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya
kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili
3, mwaka huu.
Waziri Mkuu amezitaja mali za
Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) zilizorejeshwa kuwa jengo la
Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd. maarufu kwa jina la “Transport
House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa
wa Stesheni; kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil Mill,
kilichopo katika eneo la Igogo; na jengo na viwanja vya Ashock
Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.
Nyingine ni majengo ya
kilichokuwa kiwanda cha mkonge na dengu kilichopo eneo la Igogo kwenye
kiwanja namba 41 na 79; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo
namba 80, kitalu “D”; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo
namba 110, kitalu “D” na ghala moja katika kiwanja namba 104, kitalu “A”
kilichopo eneo la Igogo.
“Mali nyingine zilizorejeshwa ni
jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja namba 8 Kitalu “K”; jengo
moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja namba 24, Kitalu “K” na jengo
lililopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”,” amesema Waziri
Mkuu.
Kwa upande wa mali za SHIRECU,
Waziri Mkuu amezitaja mali zilizopo kwenye hatua ya makabidhiano kuwa ni
ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya ghorofa tatu
iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, jijini Dar es Salaam.
“Katika kusimamia misingi ya
utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa vyama vya ushirika, Serikali
inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu mikataba mibovu ya Chama
Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha
Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na Chama
Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU). Vilevile, tunachunguza
kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea
kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vilivyosinzia
katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara na kwamba juhudi na hatua
hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza imani, hamasa na
uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua kipato
cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri wenyewe katika
sekta ya kilimo.
SHARE
No comments:
Post a Comment