Na Lorietha Laurence-Dodoma
Serikali imeeleza kuwa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kama zilivyo taasisi nyingine kimefuata taratibu za
ujenzi na umiliki wa viwanja vya michezo kwa mujibu wa sheria, taratibu
na kanuni zilizopo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe .Juliana Shonza leo Mkoani
Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupa Victor Mwambalaswa,
lililohoji kuhusu viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na Chama hicho.
“Ni vizuri ikafahamika kwamba
mpaka sasa viwanja hivyo vinaendelea kutumika na umma wa watanzania kwa
shughuli mbalimbali za kimichezo, kijamii na kiserikali sawa kabisa na
Mipango ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995, Sura ya 4
(i)-(ii)”
“kwa hiyo kuhusu suala la uporaji
wa viwanja hivyo, CCM hakijafanya uporaji wowote kwa kuwa kinamiliki
viwanja hivyo kihalali kwa mujibu wa sheria zilizopo hivyo ushiriki wa
wananchi wenye mapenzi mema katika ujenzi wa viwanja hivyo hauondoi
uhalali wa Chama cha Mapinduzi kumiliki viwanja hivyo”amefafanua Shonza.
Aidha Naibu Waziri Shonza amesema
kuwa, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1955, sura ya 7(vi)
inaeleza wajibu wa Mamlaka ya Serikali za mitaa kushirikiana na wadau
kujenga, kulinda na kutunza miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja.
Akizungumzia kuhusu mpango wa
serikali katika kusaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja wa chunya Shonza
amesema kuwa, ujenzi wa viwanja vya michezo ni jukumu jumuishi ambalo
linawapa fursa wadau na wananchi kujenga na kuendeleza miundombinu ya
michezo katika maeneo yao kwa manufaa ya jamii.
Hata hivyo, Mhe. Shonza
amepongeza juhudi za wananchi wa Chunya kwa jitihada za kuanza ujenzi wa
uwanja wa kisasa wenye thamani ya bilioni 8 huku Halmashauri ya Chunya
ikiwa imetenga kiasi cha shilling Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo.
Mhe. Shonza amezidi kufafanua
kuwa Serikali katika awamu zote tokea kupatikana kwa uhuru imekuwa
mstari wa mbele katika kuhimiza watu binafsi, mashirika na Taasisi
kuchangia katika kujenga na kuendeleza viwanja vya michezo nchini.
SHARE
No comments:
Post a Comment