Mwandishi WEtu, TJNCDF
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2007 duniani kote kulikuwa na wagonjwa
milioni 246, mwaka 2012 wagonjwa milioni 371, mwaka 2013 wagonjwa milioni 382
na takwimu za shirika la Afya Duniani(WHO) za hivi karibuni, zinaonyesha kuwa watu
milioni 422 wanaugua ugonjwa huu.
Wataalamu wanakadiria kuwa ifikapo mwaka 2035, idadi ya watu wanaougua
kisukari itafikia milioni 592.
Udhibiti wa ugonjwa huo kwa kawaida hutegemea matumizi ya dawa sanjari
na mfumo mzuri wa ulaji wa vyakula na mazoezi.
Mpangilio mzuri unaosaidia katika udhibiti wa tatizo la kisukari
unaweza kukumbukwa haraka kwa kutumia mfano wa rangi za taa za barabarani
zinazotumika kuongozea watumiaji wa barabara. Taa hizi zina rangi tatu;
nyekundu, njano na kijani.
Katika lishe kwa ajili ya udhibiti wa kisukari, rangi nyekundu
inawakilisha vyakula ambavyo unatakiwa usile kabisa.
Rangi ya njano inawakilisha vyakula ambavyo mtu anaweza kula kwa
uangalifu au kwa wastani na rangi ya kijani inaonyesha kuwa unaweza kula
vyakula hivi kwa wingi bila madhara.
Vyakula
ambavyo vinawakilishwa na rangi nyekundu
Vyakula ambavyo vinawakilishwa na taa nyekundu na unatakiwa kuviepuka
kabisa kama unakisukari ni vifuatavyo:
•
Sukari, soda tamu, juisi za viwandani, pipi,
chocolate, biskuti, miwa na asali.
•
Nyama nyekundu ambayo ina mafuta mengi hasa nyama
ya nguruwe, sausage, na maziwa ambayo hayajaondolewa mafuta.
Vyakula hivi vinaongeza lehemu
(cholesterol) mbaya na mafuta mwilini. Lakini pia vyakula hivi havina
nyuzinyuzi za lishe zinazosaidia tumbo kusaga chakula taratibu na kupunguza
mahitaji ya insulini.
•
Vyakula vilivyokobolewa kwani vinapungukiwa
nyuzinyuzi za lishe na ambazo husaidia chakula kumengenywa taratibu na hivyo
kuifanya sukari isiongezeke mwilini kwa haraka. Pia vinapunguliwa na vitamini.
Tumbaku na bidhaa zake zote sio salama kwa binadamu ye yote na
zitajadiliwa kwenye makala ya pekee.
Vyakula
ambavyo vinawakilishwa na rangi ya njano
Katika kundi la vyakula vinavyowakilishwa na taa ya njano tunapata
vyakula kama vile samaki na mafuta yanayotokana na mbegu au matunda ya mimea.
Mafuta ya samaki yanaleta afya bora ya mishipa ya fahamu na ubongo.
Katika utumiaji wa mafuta, inashauriwa usikaange vyakula.
Katika kundi hili pia kuna vyakula kama mikate na ugali wa unga
usiokobolewa, ndizi za kupika, wali na viazi mviringo vya kuchemsha.
Vyakula hivi vina wanga ambao hugeuzwa taratibu sana kuwa sukari katika
kipindi cha saa tatu hadi nne za uyeyushaji wa chakula tumboni. Vyakula hivi
pia vina nyuzilishe nyingi, vitamini B1 na E na vinaondosha tindikali katika
damu, hali inayoimarisha afya ya figo.
Katika kundi hili la vyakula pia kuna karanga, njugu, njegere, korosho
na maharage. Vyakula hivi huleta nguvu na hupunguza kiwango cha sukari mwilini
kwa vile vimesheheni vitamini na madini ya aina mbalimbali.
Ulaji wa kiasi wa matunda kama vile maembe, mapapai, matufaa,
parachichi, tikitimaji, n.k. ni mzuri kwa sababu sukari inayotokana na matunda
haihitaji insulini nyingi, hupunguza lehemu mbaya na huimarisha afya ya mishipa
ya damu.
Tufaa lina aina ya nyuzinyuzi ambazo husaidia kurekebisha taratibu
kiasi cha sukari katika damu. Parachichi pia ni zuri kwa vile hurekebisha
kiwango cha sukari na husawazisha kiwango cha mafuta ndani ya damu.
Tikitimaji na matango yana wanga kidogo na huleta hali ya kushiba
haraka na kupunguza unene.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliochapishwa mwaka1991 katika jarida
la ‘Diabetes Research and Clinical Practice’ toleo namba 14, sukari katika
ugonjwa wa kisukari wa aina ya pili hushuka kuliko inavyotazamiwa pale mgonjwa
anapokula embe. Tunda hili pia huimarisha afya ya mishipa na kudhibiti athari
za kisukari kwenye mishipa ya damu.
Ndizi pia sukari yake inaingia ndani ya damu taratibu sana na zina
madini ya potasiumu kwa wingi hivyo hudhibiti shinikizo la damu na kuboresha
maisha pale zinapoliwa kwa uangalifu.
Yote yaliyo juu kuhusu matunda ni kuhusu matunda yenyewe na sio juisi.
Kwa sababu juisi haikai tumboni, sukari yake huingia mwilini haraka na
kusababisha sukari kwenye damu kupanda haraka. Hivyo inashauriwa kula matunda
bila kuyakamua.
Chumvi inapaswa kupunguzwa sana katika chakula ili kudhibiti shinikizo
la damu.
Ni heri kutotumia pombe lakini kama unatumia, usizidishe glasi moja ya
mvinyo, au kipimo kimoja cha pombe kali, au chupa moja ya bia ya Tanzania kwa
siku. Pombe huchangia ongezeko la uzito na kwa wale wanaotumia dawa za
kusukari, pombe huifanya vigumu kurekebisha sukari ikiwa imeshuka Zaidi ya
kawaida.
Vyakula
ambavyo vinawakilishwa na rangi ya kijani
Vyakula ambavyo ni vizuri kula kwa wingi ambavyo vinawakilishwa na
rangi ya kijani katika taa za barabarani ni pamoja na mboga mboga kama vile
majani ya maharagwe, bamia, spinachi, kabeji, karoti na uyoga. Mbogamboga zina
wanga kidogo, huzuia na kupunguza unene.
Dk Ernst Schneider katika kitabu chake cha ‘Health through Nutrition’ toleo
la mwaka 1986, anasema kabeji ina viinilishe vinayofanya kazi kama insulini.
Kabeji pia ina wanga kidogo, inaleta hali ya kushiba haraka na inaimarisha afya
ya mishipa ya damu na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na shinikizo
la damu.
Mambo ya kukumbuka wakati unapangilia mlo wako kwa ajili ya kudhibiti
kisukari na kupata afya maridhawa ni kwamba mboga zinazoandaliwa bila
kuchemshwa sana, saladi na matunda vina faida zaidi.
Usile chakula kilichokufa kwa kuoza na kuungua au mboga zilizochemshwa
kupita kiasi na kupoteza rangi yake ya kijani. Kwa ajili ya siha njema
unapokuwa na kisukari, kula milo midogo midogo mara 5 au 6 kwa siku badala ya
milo mitatu mikubwa.
Mtu mwenye ugonjwa wa kisukari anaweza kutumia kahawa au chai mradi
asiwe sukari au asali.
Makala haya
yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
(TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA).
Maoni, maswali na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam au kwa simu
0713247889 .
SHARE
No comments:
Post a Comment