TRA

TRA

Sunday, February 11, 2018

Saratani ya shingo ya kizazi tishio zaidi kwa wanawake

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



Mwandishi Wetu
SARATANI ya Shingo ya kizazi imekuwa tishio kwa wanawake wengi hapa nchini.

Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa asilimia 33 ya wanawake wenye saratani, wanaugua ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga ya Saratani katika hospitali ya Saratani Ocean Road, Dkt. Crispin Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi ni kati ya magonjwa yanayosababisha wanawake wengi kupoteza maisha kwa kutofahamu uwepo wa tatizo hilo.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi imeshika nafasi ya pili kwa magonjwa ya saratani kwa wanawake na ni sababu kubwa ya vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea.



Saratani hii husababishwa na virusi viitwavyo 'Human papilloma Virus (HPV)’ iwapo kinga ya mwili itashindwa kuondoa maambukizi ya hivi virusi.

Dkt. Kahesa anasema iwapo maambukizo hayo yataendelea kwa muda mrefu chembe hai za kawaida huanza kukua bila mpangilio na kuwa saratani, jambo ambalo linaweza kuchukua miaka miwili hadi ishirini tangu kuambukizwa.



Kirusi cha HPV huenea kwa njia ya kugusana sehemu za siri, hivyo maambukizo yanaweza kutokea hata kama tendo la kujamiina halijahusisha muingiliano wa sehemu za siri. Hivyo mpira wa kiume unaweza kupunguza maambukizi lakini si kwa asilimia 100.

Maambukizi ni makubwa hasa kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 25 ambao miili yao haijapambana na kupata kinga ya mwili ya kuondoa hivyo virusi.

Baadhi ya vitu vinavyochangia maambukizi ya HPV ni kuanza kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo, upungufu wa kinga mwilini, kurithishana kati ya vizazi, na ukali wa virusi.

Dkt. Kahesa anasema hakuna dalili zinazojitokeza katika hatua za mwanzo za maambukizi lakini katika hatua za mbele za ugonjwa dalili zinajitokeza kama kutokwa na damu au ute ukeni kusiko kwa kawaida, maumivu wakati wa tendo la kujamiiana, uvimbe ukeni, na kutokwa haja ndogo na kubwa kusikojulikana.

Anasema upimaji wa ufasaha unawezasha ugunduzi mapema na huweza kuzuia kuendelea kwa ugonjwa na hatimaye kupunguza hatari ya vifo vitokanavyo na saratani.

Dkt. Kahesa anasema kuwa njia mbili za kupambana na tatizo hili ni kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV na uchunguzi wa mara kwa mara kugundua ugojwa mapema. Tiba ya mapema ni gharama ndogo kuliko ile ya ugonjwa ulioenea na pia huweza kuondoa kabisa saratani.
Pia anasema saratani inatibika mtu akiwahi hospitali mapema na huduma kwa sasa zimesambaa hospitali zote za rufaa.

Hata hivyo  anasema jamii inatakiwa kubadilisha mfumo wa maisha, kufanya mazoezi na kula vyakula bora ambavyo havina kemikali.

Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maoni, maswali na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam au kwa simu 0713247889 .


Mwisho

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger