TRA

TRA

Thursday, June 9, 2016

BAJETI KUU YA TANZANIA KWA MWAKA 2016/2017

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango
HOTUBA   YA   WAZIRI   WA   FEDHA NA MIPANGO,  MHESHIMIWA  DKT.  PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSUMAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2016/2017
TANGULIZI
1.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17. Pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha matumizi ya Serikali wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.  
2.      Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama hapa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya nchi yetu. Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa kuwa Mbunge wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu Tukufu. Kadhalika, natumia fursa hii kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kuongoza mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.

3.      Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu wa kitaifa: Mama Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu wa Rais), Mama Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani Mganga (mke wa Mhe. Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na Mama Saada El-Maamry Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza viongozi wetu vizuri.  Asante kwenu wote na Mungu awabariki.

4.      Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968 Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata” mwisho wa kunukuu. Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na kuwa sehemu ya Bunge hili.  Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa na Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania. Nampongeza pia Dkt. Thomas Kashililah, Katibu wa Bunge na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuratibu vyema shughuli za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia kumpongeza Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma kwa wakati.

5.      Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara vijijini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa mapendekezo na ushauri. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

6.      Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kumshukuru Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti hii.

7.      Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri wao. Kipekee niwashukuru wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa masuala ya kodi (Task Force) na kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think Tank) kwa ushauri wao mzuri walionipa.

8.      Mheshimiwa Spika,kwa kukamilisha shukrani hizi, napenda kutoa shukrani maalum kwanza kwa Prof. Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, mwalimu wangu na mfano bora wa maisha yangu kikazi.  Amenilea kitaaluma na kikazi tangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Benki ya Dunia, na ameendelea kunishauri katika utumishi wangu Serikalini. Ninamshukuru sana kwa uzalendo na unyenyekevu wake na ninamtakia kheri na afya njema yeye na familia yake. Pia ninapenda kutoa shukrani maalum kwa rafiki yangu mpenzi, mke wangu Mbonimpaye kwa kunitunza vizuri, lakini hasa kwa kuniombea msaada wa Mungu siku zote akishirikiana na watoto wetu, wanafamilia wengine na marafiki zetu. Asanteni na Amani iwe kwenu! Aidha nawashukuru viongozi wa dini mbalimbali na watanzania wote ambao waliitikia rai ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kumuombea na wanatuombea sana na sisi wasaidizi wake ili tujitoe na kuwatumikia watanzania, na hasa maskini, kwa bidii na unyenyekevu. Mungu awabariki! Kadhalika, nawashukuru sana wananchi wa kijiji cha Kasumo, wilaya ya Buhigwe nilikozaliwa, pamoja na wananchi wa Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Asanteni kwa kunilea na kwa mapenzi yenu mema.

9.   Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kweli ya kutekeleza ahadi zake zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kukidhi kiu na matarajio ya Watanzania. Malengo makuu ya kiuchumi ya Bajeti hii ni mawili. Kwanza ni kutatua matatizo yanayowakabili wananchi ili kuleta matumaini mapya ya maisha mazuri zaidi kwa wananchi wetu, hasa wa kipato cha chini. Lengo hili litahusisha kufanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa Serikali, hususan kurejesha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, na kuondokana na ufanyaji kazi kwa mazoea, pia kuimarisha uadilifu na usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za Taifa. Pili ni kujenga uchumi wa kipato cha kati kiuhalisia kwa kusimamia kwa umakini utulivu wa uchumi na uendelezaji wa viwanda vitakavyoongeza ajira hasa kwa vijana wetu nchini na kuongeza tija kwenye kilimo ili kuongeza kipato katika sekta hii inayotegemewa na wananchi wengi.

10.     Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa Rais akifungua Bunge hili tarehe 20 Novemba 2015, alibainisha maeneo yanayolalamikiwa sana na wananchi, na kuelekeza Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua malalamiko hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Naomba niyarejee kwa kifupi. Kwanza ni rushwa katika maeneo yote ya utoaji huduma kwa wananchi; Pili, ni upotevu wa mapato, ujangili, wizi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha, uzembe na urasimu katika maeneo mbalimbali; eneo la tatu ni huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu bora na afya; eneo la nne ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, vijiji na hifadhi, wananchi na wawekezaji, wananchi na wamiliki wa mashamba pori na uvunjaji wa sheria za ardhi.

11.     Mheshimiwa Spika, eneo la tano ni huduma zisizoridhisha za usafiri na usafirishaji kutokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa majini; na udhaifu mkubwa wa shirika la ndege. Eneo la sita ni upungufu katika utoaji haki ikiwa ni pamoja na mlundikano wa kesi mahakamani, wananchi kubambikiwa kesi na polisi, makazi duni na ukosefu wa vitendea kazi kwa askari; eneo la saba ni kodi na tozo za kero kwenye mazao, uhaba wa zana na pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi, uhaba wa masoko ya uhakika, maghala, maafisa ugani na huduma za ugani, na uvuvi haramu; na eneo la nane ni uwezeshaji mdogo kwa makundi maalum hususan wazee, walemavu, wanawake, watoto, vijana, wafanyakazi, wasanii, wanamichezo, wachimbaji wadogo na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

12.     Mheshimiwa Spika, baada ya rejea hiyo, naomba niseme tena kwamba mkazo mkuu wa Bajeti hii ni kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kutatua kero za wananchi. Aidha, Serikali itatekeleza azma ya kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha Taifa letu kufikia hadhi ya kipato cha kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi ifikapo mwaka 2025.

13.       Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha miundombinu ya msingi kama vile ya maji, umeme na usafirishaji kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi viwandani. Ili kufanikisha hilo, mkazo mkubwa utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa rasilimali hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuibua vyanzo vipya vya mapato, na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki - EFDs ili kuongeza makusanyo na vile vile kudhibiti matumizi yasiyokuwa na tija. Hivyo, kauli mbiu ya Bajeti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira” (Industrial growth for job creation). Kwa msingi huo, Bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 imeongezwa kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 40 ya bajeti yote tofauti na miaka yote ya nyuma ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 25. Bajeti hii pia inalenga kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza ili kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje katika kuendeleza viwanda na kilimo.

 I.      MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2015/16

14.       Mheshimiwa Spika, mpango na bajeti ya Serikali mwaka 2015/16 ililenga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 22.49 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 13.99 zilikuwa ni makadirio ya mapato ya ndani zikijumuisha mapato ya Halmashauri; shilingi trilioni 2.32 ni mikopo nafuu na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo; shilingi trilioni 4.03 ni mikopo ya kibiashara ya ndani; na shilingi trilioni 2.14 ni mikopo ya kibiashara ya nje. Aidha, kiasi cha shilingi trilioni 16.57 kilipangwa kutumika kwenye matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 5.92 kwenye matumizi ya maendeleo.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger