
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt Philip Mpango (kushoto) akiongea na waandishi wa habari (hawamo
pichani)jijini Dar es Salaam, kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali
dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na ushiriki wake katika
kuwezesha mkopo wa Serikali wa Dola za Kimarekani Milioni 600 na Kulia
kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Bw. Lila Mkila.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt Philip Mpango (katikati) akitoa tamko kwa waandishi wa habari
(hawamo pichani) jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kusudio la kuitoza
Benki ya Stanbic faini ya shilingi bilioni 3. Kulia kwake ni Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Servicius Likwelile na Kushoto kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) Bw. Lila Mkila.
………………………………………………………………………………………
Utangulizi
Mwezi Julai 2013, Benki Kuu ya
Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za mabenki iligundua
matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia kuacha na
kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania
Limited (Stanbic) katika muda mfupi. Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua
kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo.
Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya
Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha
Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika ukaguzi huo, wakaguzi wa
Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini miamala ya kutia shaka
iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth Market
Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa
upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc
(ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank
Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger).
Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu
za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic. Jumla ya malipo
yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na zililipwa katika
akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu
(cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
Taarifa ya ukaguzi huo
iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu, na Benki Kuu
iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kuchukua hatua stahiki za
kurekebisha kasoro zilizoonekana. Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa
kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU)
kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye
mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa
Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money Laundering Act, 2006)
inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU
kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
Mnamo 29 Septemba 2015, Benki Kuu
ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya Uingereza inayohusika na
Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa (Serious Fraud Office – SFO)
ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama
ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni
mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika kuwezesha mkopo wa dola
za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba ripoti hiyo ingekuwa
wazi kwa umma. Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti
za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika,
hata hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za
ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye, Standard Bank Plc
ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za kimarekani
milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni 7 zinalipwa
kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6 zilikuwa ni fidia
na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
Kwa kuzingatia mapungufu ya
kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia kutokuweka taratibu madhubuti
za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki
na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeiandikia benki ya
Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3. Sheria
inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku ishirini
(20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari 2016. Endapo Benki Kuu
haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
Hitimisho
Benki Kuu imechukua hatua hizo
kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze kuwa makini katika
kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za
kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha, hatua hii ni onyo kwa
mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hii ambayo
ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni uvunjaji wa Sheria za nchi.
Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote
itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na Sheria ya
Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
SHARE









No comments:
Post a Comment