Mkuu
wa Wilaya mpya ya Buhigwe, Mary Tesha akiwasilisha taarifa kuhusu kero
na changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya nishati, zinazowakabili
wananchi wake mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard
Kalemani (wa pili kutoka kulia), alipofanya ziara wilayani humo hivi
karibuni.
Na Veronica Simba - Buhigwe
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amekataa kupokea Taarifa
ya utendaji kazi kwa Wilaya mpya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kutoka kwa
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa Wilaya hiyo, Ntungwa
Njegelo.
Dk Kalemani alikataa kupokea taarifa hiyo juzi Februari 19, alipokutana
na Uongozi wa Wilaya hiyo mpya, kwenye Ofisi ya muda iliyopo wilayani
humo, akiwa pamoja na watendaji mbalimbali kutoka wizarani, Tanesco na
Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
Akizungumzia
sababu za kukataa kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri alisema
haijitoshelezi kwani haijaeleza kwa kina masuala mbalimbali muhimu ya
kiutendaji katika wilaya hiyo.
“Kwa
mfano, taarifa hii inaeleza vijiji 12 vimepata umeme lakini haielezi
idadi hiyo ni kati ya vijiji vingapi. Pia, haielezi ni asilimia ngapi ya
umeme imepatikana. Taarifa hii haiwezi kunisaidia maana nataka kutatua
kero hivyo ni lazima nijue ukubwa wa tatizo.”
Kufuatia
hatua hiyo, Naibu Waziri Kalemani alimwagiza Meneja huyo aandae taarifa
mpya, yenye maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
umeme hususani mradi wa REA (Umeme Vijijini) Awamu ya pili na
kuiwasilisha kwake Jumatatu, Februari 22 mwaka huu.
Aidha,
Dk Kalemani alimwagiza Meneja huyo kufuatilia na kufanyia kazi
malalamiko ya wananchi katika eneo lake, kuhusu kuwepo na mashimo
yaliyochimbwa kwa ajili ya kusimika nguzo za umeme katika mashamba yao
lakini yameachwa wazi kwa muda mrefu pasipo zoezi hilo kufanyika hivyo
kuwazuia kuendelea na shughuli zao za kilimo.
Awali,
akiwasilisha taarifa kwa niaba ya wananchi wake kuhusu kero na
changamoto mbalimbali zinazowakabili kuhusiana na sekta ya nishati, Mkuu
wa Wilaya ya Buhigwe, Mary Tesha alimwomba Naibu Waziri kusaidia ili
mashimo yaliyochimbwa katika baadhi ya vijiji kwa ahadi ya kusimika
nguzo za umeme, yafanyiwe kazi mapema ili wananchi waendelee na shughuli
za kilimo katika mashamba yao.
Vilevile,
Dk Kalemani alisema pamoja na mapungufu kadhaa, Tanesco wamejitahidi
kufanya kazi nzuri ya kuwaunganishia wananchi wa vijijini umeme kwa
kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alimpongeza
Mkandarasi mzalendo anayeunganisha umeme wa REA Awamu ya pili mkoani
Kigoma, Wilbroad Mutabuzi kupitia kampuni yake ya JV State Grid
Electrical and Trchnical Works Ltd kwa kazi nzuri anayoifanya.
“Kuna
baadhi ya maeneo tumekutana na matatizo ya wakandarasi kufanya kazi
chini ya kiwango hivyo kuturudisha nyuma. Huyu Mkandarazi mzawa
anayefanya kazi hiyo hapa Kigoma anajitahidi sana na namtaka aendelee
hivyo.”
Alisema
ameagiza zoezi la kuunganisha umeme wa REA Awamu ya pili likamilike
ifikapo Mwezi Aprili mwishoni, hivyo wale wote waliopangwa kuunganishiwa
umeme katika awamu hiyo, wanapaswa kuwa wamepatiwa huduma hiyo ndani wa
kipindi hicho.
Naibu
Waziri Kalemani yupo katika ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa chini ya wizara yake. Alianza ziara hiyo mkoani Tabora,
sasa yupo Kigoma na anatarajia kumalizia ziara hiyo ya siku 10 mkoani
Geita.
SHARE
No comments:
Post a Comment