Mkuu
wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samuel Nzoka (kulia) akipokea moja kati ya
mashuka 170 yaliyotolewa juzi na Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya
afya (NHIF) wa mkoa wa Manyara, Isaya Shekifu (kushoto) kwenye uzinduzi
wa uhamasishaji wa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF.
Na Woinde Shizza,Manyara
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Manyara, umekabidhi mashuka 170
kwenye zahanati ya Kijiji cha Engusero na hospitali ya wilaya ya Kiteto
kwa ajili ya kutumiwa kujifunika na wagonjwa wanaofika kulazwa.
Mashuka
hayo yalikabidhiwa kwa mkuu wa wilaya hiyo Kanali Samuel Nzoka na
meneja wa NHIF wa mkoa huo Isaya Shekifu, kwenye uzinduzi wa
uhamasishaji wa kujiunga mfuko wa afya ya jamii (CHF) uliofanyika juzi
kijiji cha Engusero.
Akizungumza
wakati akipokea mashuka hayo Kanali Nzoka aliushukuru mfuko huo na
kuzitaka kaya za eneo hilo kujiunga na CHF ili wajipatie matibabu kwa
mwaka mzima kwani kaya moja yenye watu sita italipia sh10,000.
Alisema
tatizo la ukosefu wa dawa kwenye zahanati, vituo vya afya na
hospitalini litamalizika, endapo kaya nyingi zikijiunga na CHF kwani
serikali nayo itaweka mkono wake ili kuhakikisha huduma za afya
zinaboreshwa.
Wakati
wa uzinduzi wa zoezi hilo Kanali Nzoka alijitolea sh20,000 kwa ajili ya
kuzilipia kaya mbili za watu 12 wa kijiji cha Engusero na Dosidosi na
kuungwa mkono na viongozi wanne wa wilaya hiyo waliojitolea sh10,000 kwa
kila mmoja.
Kwa
upande wake, Shekifu alisema mwanachama wa CHF atanufaika na huduma zote
za afya za msingi za kinga na tiba zitolewazo katika zahanati, kituo
cha afya na hospitali ikiwemo huduma za wagonjwa wa kutwa na kulazwa.
Alitaja
huduma nyingine ambazo zitatolewa kwa mwaka mmoja kwa kuchangia
sh10,000 ni vipimo vya maabara, upasuaji kulingana na utaratibu
uliowekwa na halmashauri husika na wanachama kupata huduma bora ya
afya.
“Pia
watapata huduma ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na
Halmashauri zinazoendesha mifuko hii zinapata mapato ya tele kwa tele
kutoka serikalini ambayo yatatumika kuboresha huduma za afya,” alisema.
Ofisa
uratibu na matokeo wa CHF, Nicholaus Mwangomo alisema mpango huo
ulianzishwa kwa sheria namba moja ya mwaka 2001 sura ya 409 ya sheria ya
Tanzania toleo la 2002 wa kaya au familia kuchangia gharama za matibabu
kabla ya kuugua.
Mwangomo
alisema sababu za kuanzishwa CHF ni kuiwezesha jamii kumiliki huduma za
afya zinazowahusu katika maeneo wanayoishi, kuchangia huduma za afya
kwa wananchi na kuboresha huduma za matibabu kwa utaratibu rahisi.
SHARE
No comments:
Post a Comment