Naibu
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Watoto na Wazee Mhe.Hamis
Adrea Kigwangalla akijibu maswali kutoka kwa wabunge mbalimbali katika
kipindi cha maswali na majibu katika kikao cha Tano cha Bunge la 11
linaloendelea Mjini Dodoma. Picha na Raymond Mushumbusi MAELEZO
…………………………………………………………………………………………….
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Serikali
imejipanga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kuwawezesha kila
mwananchi kupata Bima ya Afya itakayosaidia kupata huduma bora za afya
katika zahanati na hospitali mbalimbali.
Akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Faida Mohammed Bakar(CCM)
lililouliza kuwa bado kuna ukiukwaji wa huduma za afya, haki za afya na
haki za uzazi katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya wakati
wa maswali na majibu,Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,
Jinsia,Watoto na Wazee Mhe.Hamis Adrea Kigwangalla amesema katika
kuhakikisha kuwa haki hizi zinapatikana,Serikali kwa kupitia mifumo
yake, ikiwa ni pamoja na mabaraza ya weledi, kurugenzi ya uhakiki na
ubora wa huduma za afya na idara mbalimbali zilizo chini ya Waziri
zinatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusiana na haki za wateja.
Mhe.
Hamis Adrea Kigwangalla amesema katika kutekeleza hili vituo vyote vya
kutolea huduma za afya vina masanduku ya maoni na ofisi za malalamiko
ambazo ni sehemu muhimu ambapo wateja wanaweza kupeleka malalamiko yao
ili hatua zaidi zichukuliwe kukomesha na kutokomeza ukiukwaji wowote wa
haki za wateja.
“
Tutawachukulia hatua wale wote watakaobainika kukiuka haki za wateja kwa
kupitia baraza la wauguzi na wakunga ili kuhakikisha wananchi wanapata
huduma bora zinazostahili ili kuokoa maisha ya wananchi hasa maisha ya
mama na mtoto” Alisema Mhe.Kigwangalla.
Aidha
Mhe. Hamis Adrea Kigwangalla amesema Wizara yake imeandaa rasimu ya
Sheria ya Bima ya Afya ambayo itamuwezesha kila mwananchi kupata bima ya
afya itakayomsaidia kupata huduma bora za afya katika maeneo yao.
Serikali
kupitia Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Watoto na Wazee
inatoa mafunzo kwa Wakunga wa Jadi ambao wamekuwa wakitumika sana sehemu
ambazo huduma za afya zipo mbali ili kuwezesha wananchi hao kupata
huduma bora za afya kutoka kwa wakunga hao hasa katika afya ya mama na
mtoto.
SHARE
No comments:
Post a Comment