Meneja wa
Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshach Bandawe, akifungua semina ya
waajiri wa taasisi za umma na sekta binafsi jijini Mwanza jana. (PICHA NA
BALTAZAR MASHAKA)
Mfuko wa
Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa umewashukuru waajiri kutokana na mafanikio
uliyoyapata wa kuandikisha wanachama wapya na uwasilishaji wa michango yao
kwenye mfuko kwa wakati katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015 /2016 .
Shukurani hizo zilitolewa jana na Meneja wa
PPF Kanda ya Ziwa, Meshach Bandawe wakati akifungua semina ya elimu kwa waajiri
wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mandela
Gold Crest jijini Mwanza.
Alisema
ushirikiano uliotolewa na waajiri uliwezesha mfuko huo kufanya vizuri kwa
kuandikisha wanachama wapya na kuwasilisha michango yao kazi ambayo wao pekee
wasingeweza kuifanya na kufikia kwenye mafanikio waliyoyapata.
“Katika mwaka wa fedha kipindi cha Julai 2015
hadi Februari 2016 tumeandikisha wanachama 8,124 sawa na asilimia 98.5 ya lengo
la wanachama 8,240.
“Lakini pia
tumekusanya michango ya sh. bilioni 9.6 sawa na asilimia 83.5 kati sh. bilioni
11.5 ya malengo. Pia tumelipa sh. bilioni 1.5 kwa mafao 1,149, kuanzia Julai
hadi Desemba 2015,” alisema Bandawe.
Alieleza
kuwa mafanikio ya PPF Kanda ya Ziwa hayawezi kuwaacha wadau (waajiri) hao
ingawa jukumu la kuandikisha wanachama na kuwasilisha michango yao kwenye mfuko
ni kutimiza wajibu wao wa kisheria, lakini pia kutowasilisha michango kwenye
mfuko kunaufanya ushindwe kuwalipa wanachama mafao yao.
Alisema
semina hiyo imelenga kuwaongezea waajiri uwajibikaji katika shughuli zao na
kuwawekea akiba waajiriwa licha ya kuwalipa mishahara ili siku wakiondoka
kwenye ajira waendelee kupata mishahara hiyo wakiwa nje ya ajira.
“Kama
waajiri wapeni waajiriwa elimu ya mfuko wa PPF ili wafahamu vizuri mafao na
huduma zinazotolewa na mfuko huo, pale mnapokaa nao mna wajibu wa kuwaelimisha
waelewe kile wanachochangia. Pia kutofutiana kwa mafao baina ya mfuko na mfuko
hilo limeshapatiwa ufumbuzi kupitia SSRA,” alifafanua.
Meneja huyo wa PPF aliongeza kuwa mfuko huo
kwa miaka 25 umekuwa wa kwanza kuelimisha wanachama na wadau wake kuhusu mafao
na huduma mbalimbali wanazozitoa kwa misingi ya kuboresha huduma zao.
Bandawe pia
alisema mfuko huo uko mbioni kujenga nyumba 500 za gharama nafuu katika eneo la
Kiseke Manispaa ya Ilemela zitakazouzwa kwa wanachama wake ambapo alitoa rai
kwa waajiri kuendelea kuwasajili wafanyakazi wao kwenye mfuko wa PPF wakiwemo
walimu ili wafaidike na huduma zake bila kujali wana ajira ya muda au ya
kudumu.
SHARE
No comments:
Post a Comment