
Meneja wa
mradi wa Ujenzi wa Flow Meter ya Kigamboni Eng. Mary Mhayaya akifafanua
jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi huo.

Muonekano wa Flow Meter mpya ya Kigamboni katika hatua za mwisho za ujenzi wake.

Muonekano wa Daraja la Kigamboni mara baada ya ujenzi wake kukamilika.

Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati)
akijadiliana jambo na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni (kushoto) na Nahodha
wa kivuko hicho (kulia) wakati alipokikagua.

Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipata
maelekezo kwa Mkurugenzi Msaidizi Barabara za Mijini Eng. Hussein
Mativila (kushoto) alipokagua Daraja la Kigamboni.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mtambo
mpya wa kisasa wa kupima mafuta yanayoingia nchini flow meter unaojengwa
Kigamboni jijini Dar es salaam uko katika hatua za mwisho za kukamilika
kwake na utaanza kazi rasmi mapema mwezi ujao.
Prof.
Mbarawa amesema hayo wakati alipokagua mtambo huo unaosimamiwa na
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na kuhimiza waendeshaji wa mtambo huo
wawe watu wenye uadilifu wa hali ya juu na elimu ya kutosha ili kuulinda
na kuwezesha kufanyakazi inavyostahili.
“Hakikisheni
mnawasiliana na Wakala wa Vipimo nchini (WMA), ili wahakikishe mtambo
huu unaviwango vinavyotakiwa vitakavyowawezesha wafanyabiashara wa
mafuta kuridhika na ufanyakazi wa mtambo huu ili kuondoa malalamiko”,
amesema Prof. Mbarawa.
Zaidi ya
shilingi bilioni 12 zimetumika katika ujenzi wa mtambo huo ambao
utawezesha Serikali kupata mapato stahiki na wafanyabishara kupata
mafuta sahihi kwa mujibu wa mahitaji yao.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa Daraja la Kigamboni na
kuwataka wananchi kuhakikisha wanalitumia daraja hilo kwa usahihi na
kuepuka vitendo vyote vya hujuma.
Amesema
daraja hilo lililojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 214 linatarajiwa
kufunguliwa rasmi Aprili 16 na litakuwa na njia sita za magari na mbili
za watembea kwa miguu.
“Nawataka
wananchi na watumiaji wote wa daraja hili kuhakikisha kuwa miundombinu
ya daraja haihujumiwi na watu wenye nia mbaya kwani vitendo vya aina
hiyo licha ya kuharibu daraja vitahatarisha usalama wa watumiaji”,
amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye
Msimamizi wa Daraja hilo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng.
Karim Mataka amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa Daraja la
Kigamboni umekamilika katika hatua zote na kinachosubitriwa na ufunguzi
na kuanza kutumika.
Amesema
wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu matumizi
ya daraja hilo kwa madereva na watembea kwa miguu ili kuepuka usumbufu
siku za mwanzoni.
Daraja
hilo litakalofunguliwa rasmi Aprili 16 litapunguza msongamano wa usafiri
kwa wakazi wa kigamboni na maeneo ya katikati ya jiji la Dar es salaam.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment