Na Lydia Churi- Musoma
Mahakama
ya Tanzania inakusudia kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wa Mara ambapo
ujenzi wa jengo la mahakama hiyo unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka
huu.
Akizungumza
leo mjini Musoma katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama
katika kanda ya Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande
Othman alisema mkoa wa Mara unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu kwa kuwa
nia ya Mahakama ni kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Alisema
mahakama hiyo itajengwa kwa haraka na itamalizika katika kipindi cha
mwaka moja kwa kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi huo tayari imeshatengwa
ambapo nyingine imetokana na msaada waliopewa kutoka Benki ya Dunia.
Alisema
kuanzishwa kwa mahakama hiyo katika Mkoa wa Mara kutawapa fursa wananchi
wa Mara ya kupata huduma kwa karibu zaidi na pia itasaidia kupunguza
kesi zilizoko mahakamani kwa haraka.
Awali
akimkaribisha Jaji Mkuu ofisini kwake alipomtembelea, Mkuu wa Mkoa wa
Mara, Magesa Mulongo alimwomba Jaji Mkuu kuanzisha Mahakama Kuu katika
mkoa wake kwa kuwa asilimia 55 ya kesi zote za mauaji katika Mahakama
kuu kanda ya Mwanza zinatoka katika mkoa wa Mara hivyo mkoa huo unayo
haki ya kuwa na Mahakama Kuu.
Pamoja na
mkoa huo kuwa na kesi nyingi za mauaji, Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa
wa Mara pia unakabiliwa na kesi nyingi zinazohusu masuala ya ardhi kwa
kuwa ni asilimia 38.3 tu ya eneo zima la mkoa huo ndiyo eneo linalotuwa
kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli za maendeleo
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Mara una wakazi zaidi ya milioni 1.3.
Alisema
Mkoa wa Mara una eneo lenye kilometa za mraba 30,150 ambapo asilimia 36
ya eneo hilo ni maji wakati asilimia 25.7 ni eneo lenye mapori na
hifadhi za Taifa ikiwemo mbugaya wanyama ya Serengeti.
Aidha,
Mkuu huyo wa mkoa aliisifu Mahakama ya Tanzania kwa kufanya kazi yake
kwa weledi ya kuzimaliza kesi zilizohusu mapigano ya koo zilizokuwepo
katika siku za nyuma mkoani humo kwa kuwa zimesaidia maeneo ya mkoa huo
kuwa salama hivi sasa na hayaonyeshi dalili za kujirudia. Aliongeza kuwa
eneo la haki likitulia hata masuala ya utawala yakuwa rahisi.
Jaji mkuu
Leo amehitimisaha ziara yake katika kanda ya Mwanza yenye mikoa ya
Mara, Geita na Mwanza ambapo alikuwa akikagua shughuli mbalimbali za
kimahakama katika kanda hiyo.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment