Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Enterberth Nyoni akitoa ufafanuzi
kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuhusu uboreshaji wa vyuo kwa
kujitegemea wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya
Jamii mjini Dodoma.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Bw.Dickson Rusage akitoa ufafanuzi kwa Wakuu wa Vyuo
vya Maendeleo ya Jamii kuhusu matumizi mazuri ya rasilimali fedha, watu,
utunzaji wa mali za Serikali na Utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora
katika Taasisi za Maendeleo ya Jamii leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi
wa Utawala na Uendeshaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Bi. Eliasifu Mlay akitoa ufafanuzi kuhusu uzingatiaji
wa Maadili katika Utumishi wa Umma wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii leo mjini Dodoma.
Na.Aron Msigwa - Dodoma.
Maafisa
Maendeleo ya Jamii wanaohitimu mafunzo katika vyuo mbalimbali nchini
na wale waliko kazini wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi vijijini ili
kuwawezesha wananchi kuzitumia fursa za maendeleo zilizoko katika maeneo
wanayoishi kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Bw. Enterberth Nyoni wakati akitoa ufafanuzi kuhusu Utendaji
Kazi wa Maafisa hao wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya
Maendeleo ya Jamii mjini Dodoma.
Amesema
Maafisa Maendeleo popote walipo lazima watambue kuwa wao ni dira na
chachu ya mabadiliko ya kuwafanya wananchi kubadilika kwa kufanya kazi
kulingana na mabadiliko na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Amesema
kuwa dhana ya Maendeleo ya Jamii ni pana na ikilenga kuwafanya wananchi
kutumia rasimali zinazopatikana katika mazingira yao kujiletea
maendeleo akibainisha kuwa maafisa Maendeleo wanaozalishwa katika vyuo
mbalimbali lazima washiriki kikamilifu katika katika kuwaletea wananchi
maendeleo endelevu kwa kuwapatia elimu, ushauri na mbinu mbalimbali za
kuondoa umaskini.
Kuhusu
ubora wa kiwango cha taaluma ya maendeleo ya Jamii inayotolewa katika
vyuo mbalimbali amesema kuwa ipo haja ya kuendelea kujenga msingi imara
vyuoni na kuandaa vigezo vya kuwapima maafisa maendeleo ya Jamii kwa
kuangalia ufanisi wa utendaji kazi wao wa kila siku.
Amefafanua
kuwa jukumu kubwa la vyuo hivyo pamoja na mambo mengine ni kubadilisha
mitazamo ya wanafunzi walioko vyuoni kwa lengo la kuwafanya kuwa chachu
ya mabadiliko na kuwa msaada kwa wananchi wanaowatumikia.
Kuhusu
mafunzo kwa vitendo Bw.Enterberth amesema kuwa ipo haja kwa wanafunzi
walio katika mafunzo kupangiwa mazoezi kwa vitendo katika maeneo ya
vijijini kwa kuwa ndiko liliko chimbuko la shughuli Maendeleo ya jamii
na kutoa wito kwa wahitimu hao kuwa tayari kufanya kazi katika mazingira
ya vijijini.
Aidha,amesema
kuwa katika kufanya mabadiliko katika taaluma ya maendeleo ya jamii
kitaanzishwa Chama au Bodi ya kitaaluma kusimamia wahitimu wanaomaliza
katika vyuo mbalimbali kwa lengo la kupima uelewa, ubora na viwango
kabla ya kuruhusiwa kuitumikia jamii.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu mafunzo kwa maafisa maendeleo ya Jamii walioko kazini
amesema kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo kwa
kuhakikisha kuwa mafunzo rejea kwa maafisa maendeleo ya jamii
walioajiliwa yanatolewa ili maafisa hao waweze kwenda na kasi ya
maendeleo na mabadiliko yanayotokea katika jamii.
Kwa
upande wao baadhi ya Wakuu wa vyuo hivyo wakizungumza kwa nyakati
tofauti kuhusu namna bora ya kuboresha maslahi ya vyuo hivyo hususan
kiwango cha taaluma inayotolewa wameiomba Serikali kwa kushirikiana na
wanataaluma husika kuanzisha Bodi itakayosimamia suala la viwango na
uhakiki wa wataalam wanaohitimu.
Aidha,
wamebainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wahitimu wa
fani ya Maendeleo ya Jamii imeongezeka jambo linalotoa matumaini ya
kukua kwa taaluma hiyo na kuiomba Serikali kuendelea kuweka vigezo vya
udhibiti ili kulinda viwango vya huduma zinazotolewa.
SHARE
No comments:
Post a Comment