Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali
ya Tanzania imepewa tuzo 2 za masuala ya Ustawi wa Jamii pamoja na
ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi ya maamuzi ya Serikali na
Taasisi mbalimbali katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU)
uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi, Augustine Mahiga, wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo yaliyojadiliwa
katika mkutano wa 27 wa Umoja wa nchi za Afrika uliofanyika hivi
karibuni Kigali nchini Rwanda.
“Tanzania
imetambuliwa na AU kama nchi ambayo kwa miaka 15 sasa imekua na
mikakati mbalimbali ya kitaifa ya kuzingatia haki za wanawake na
kutimiza malengo ya Milenia,” alisema Balozi Mahiga
Aliongeza kuwa Tanzania ni kati ya nchi tano bora katika bara la Afrika ambazo zimepewa tuzo hizo.
Katika
hatua nyingine, Balozi Mahiga amasema kuwa katika mkutano huo wa 27
viongozi wa Afrika walizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo hati ya
kusafiria Afrika (passport), ambayo itawezesha watu wa bara hilo
kusafiri katika nchi zote za Afrika.
Balozi
Mahiga aliongeza kuwa, lengo la kuanza kutumia hati hiyo ya kusafiria
kwa nchi za Afrika ni kutoa vikwazo vilivyokuwepo wakati wa kutembelea
na kusafiri ndani ya nchi hizo.
Aidha,
Balozi Maiga amesema kwamba, kutolewa kwa hati ya kusafiria ya Afrika ni
ishara ya Umoja na mshikamano, hati hizo zimeanza kutolewa kwa marais
na viongozi wa Serikali wa nchi ambazo zilihudhuria mkutano huo. Hati
hizo zitatumika kwa kuzingatia sheria za kila nchi.
Hali
kadhalika, mkutano huo ulijadili migogoro ya nchi za Burundi na Sudani
Kusini ambapo viongozi hao walikubaliana kupeleka Jeshi la Umoja wa
Afrika nchini Sudani Kusini ili kutenganisha majeshi ya pande mbili
zinazoendelea kupigana nchini humo.
Aidha,
mgogoro wa Burundi bado unaendelea kupatiwa ufumbuzi kutokana na
jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Rais Mstaafu Benjamin
Mkapa, ambaye aliteuliwa na mapema mwaka huu na viongozi wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Mkutano
wa 27 wa Umoja wa nchi za Afrika wenye wanachama 54 ulifanyika Kigali
nchini Rwanda tarehe 18 mwezi huu, ukiwa ni mkutano wa pili kwa mwaka
huu ulikua na kauli mbiu inayosema mwaka wa haki za binadamu.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment