Mkuu wa Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma Bw. Peter Buluku akizungumza na wanahabari kwenye Ofisi ndogo ya Wizara ya Mambo ya ndani kuhusu kutenga eneo kwa ajili ya wakimbizi wenye ualbino. (Picha na Jacquiline Mrisho –MAELEZO)
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO Kigoma
Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma imewatengea eneo maalumu la kuishi watu wenye ulemavu wa ngozi ili kulinda usalama wa maisha yao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kambi hiyo, Peter Buluku alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya maisha halisi ya wakimbizi hao wanaoishi katika kambi hiyo wakitokea nchini Burundi.
Buluku amesema kuwa katika kambi hiyo kuna baadhi ya wakimbizi wanaojihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa wakimbizi wenzao vikiwemo vya ubakaji, wizi na kujaribu kuteka watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mkuu huyo wa kambi amefafanua kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu, familia moja yenye mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ilivamiwa na watu wasiojulikana na kumchukua mtoto huyo lakini kwa bahati nzuri majirani walijitahidi kupiga kelele hivyo, watuhumiwa waliamua kumtelekeza mtoto huyo na kukimbilia kusikojulikana.
"Kutokana na kujitokeza kwa hali hiyo, Sisi pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayotoa huduma kambini hapa tuliamua kuwatengea eneo maalumu lililo karibu na kituo cha polisi watu hawa wenye ulemavu wa ngozi ili wawe na ulinzi wa kutosha hivyo kuishi kwa amani kama binadamu wengine", alisema Buluku.
Hadi sasa kambi hiyo ina jumla ya watu watano wenye ulemavu wa ngozi kutoka kwenye familia mbili tofauti, Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) limehaidi kujenga jengo la kudumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu huo.
Kambi ya Nduta ilianzishwa rasmi mwaka 1998 na kufungwa mwaka 2009. Ilifunguliwa kwa mara ya pili mwaka 2015 baada ya kutokea kwa vurugu nchini Burundi na kusababisha baadhi ya raia wa nchi hiyo kukimbilia nchini Tanzania, hadi sasa kambi hiyo ina jumla ya wakimbizi 55,320 ambao ni raia wa Burundi.
SHARE
No comments:
Post a Comment