
Wahamiaji
6,500 wameokolewa nje ya pwani ya Libya hapo jana kupitia operesheni 40
tofauti za uokozi. Ni idadi kubwa ya wahamiaji walionusurika, katika
safari za hatari za kuingia Ulaya katika siku za hivi karibuni.
Kikosi
cha ulinzi wa pwani kimeandika katika ukurasa wao wa Twitter, kwamba
uokoaji huo wa wahamiaji 6,500 uliwezekana kupitia operesheni 40
tofauti, zilizojumuisha meli za Kitaliana, mashirika ya kibinaadamu
pamoja na Shirika la Kulinda Mipaka ya Umoja wa Ulaya Frontex.
Picha za
kushtusha za moja ya operesheni hizo za uokoaji, zinawaonyesha wahamiaji
wapatao 700 wamekusanyika katika boti ya kuvulia, huku wengine
wakioneka wanajitosa kutoka katika boti hiyo wakiwa wamevalia makoti ya
kuokoa maisha, wakijaribu kuogelea ili wawafikie waokoaji.
Mtoto
mwenye umri wa siku tano alikuwani miongoni mwa wahamiaji waliokolewa
pamoja na watoto wachanga wengine, ambao walibebwa juu kwa juu kwa
kutumia helikota ya uokozi na haraka kufikishwa hospitali moja nchini
Italia, hayo ni kwa mujibu wa Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), ambao
walishiriki katika operesheni hizo za uokozi.
Siku ya Jumapili pekee, zaidi ya wahamiaji 1,100 waliokolewa wote katika eneo moja.
Kwa
mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pamoja na
wanajeshi wa majini, idadi jumla ya wahamiaji waliowasili nchini Italia
hadi sasa imeshatimia 112,500, ikiwa imepungua kidogo ikilinganishwa na
ya mwaka uliopita ambayo ilifika wahamiaji 116,000 katika wakati kama
huu.
Wengi wa wahamiaji wanatokea Afrika
Karibu wahamiaji wote miongoni mwa hao, wametokea nchi za Afrika Magharibi pamoja na za Pembe ya Afrika.
Kawaida
wahamiaji hao huondokea nchini Libya, wakati bahari ikiwa shwari huku
boti zikitegemea upepo wa kusini kuzisukuma katika bahari ya kimataifa.
Waokoaji
wa kikosi cha Italia wametabiri kwamba kuboreka kwa hali ya hewa,
kutawahamasisha zaidi wahamiaji kufunga safari za hatari za kuvuka
bahari ya Mediterania.
Boti
zinazotumika kwa safari hizo mara nyingi zinakuwa dhaifu, haziwezi
kubeba idadi kubwa ya watu wanaojazwa ndani yake. Pamoja na hayo, baadhi
ya wahamiaji huanza safari hiyo wakiwa hawana afya nzuri na hivyo
hushindwa kuhimili safari za aina hiyo hata pale bahari inapokuwa
imetulia.
Tokea
mwaka huu ulipoanza zaidi ya wahamiaji 3,000 wamepoteza maisha wakiwa
majini wakijaribu kuelekea nchini Ugiriki au Italia. Hilo ni ongezeko la
asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka jana katika wakati kama wa sasa.
Wahamiaji wengine 204,000 wamevuka bahari ya Mediterania na kuingia barani Ulaya katika miezi ya sita ya kwanza ya mwaka huu.
Shirika
la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema bara la Ulaya
linakabiliana na mgogoro mkubwa wa wahamiaji kuwahi kutokea tangu vita
vikuu vya pili vya dunia. DW
SHARE








No comments:
Post a Comment