Mkutano
wa kilele wa siku mbili wa kundi la G20 umefunguliwa nchini China
Jumapiliv (04.09.2016) kwa wito kwa chombo hicho kuwa timu ya vitendo
badala ya kuwa mahala pa kupiga porojo.
Akifunguwa
mkutano huo katika mji wa Hangzhou Rais Xi Jinping wa China amesema
anataraji huko Hangzhou wanaweza kushughulikia dalili za matatizo
halikadhalika sababu kuu za matatizo ya uchumi wa dunia ....."G20
inapaswa ibadili mtizamo wake na kuweka umuhimu sawa kwa sera za muda
mfupi na sera za muda mrefu."
China ni
mwenyeji wa viongozi 20 wa kundi hilo la nchi zenye maendeleo makubwa ya
kiuchumi duniani na zile zenye kuinukia kiuchumi katika mji mashuhuri
wa kihistoria wa Hangzhou ulioko mashariki mwa China kuanzia Jumapili
(04.09.2016) hadi Jumatatu ambapo usalama umeimarishwa kwa kuwekwa kwa
vikwazo barabarani.
Rasi Xi
alisalimiana kwa kupeana mikono na wageni waliokuwa wakiingia mmoja
baada ya mwengine katika kituo cha Maonyesho ya Kibiashara cha Kimataifa
cha Hangzhou kunakofanyika mkutano huo miongoni mwao Rais Barack Obama
wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Vladimir Putin wa
Urusi, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Waziri Mkuu wa Uingereza
Theresa May na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Dhima ya China
Tukio
hilo linaonyesha dhima ya China katika jukwaa la dunia wakati baadhi ya
viongozi wakitarajiwa kuishinikiza China kutii kanuni za kimataifa za
biashara na uzaslihaji wake wa kupindukia wa chuma.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi Rais Xi amesema kundi hilo la G20 halipaswi
kuchukuwa hatua mpya za kuhami masoko na badala yake ichukuwe hatua
madhubuti za kuchochea ukuaji wa uchumi duniani.
Obama na
XI walikutana Jumamosi jioni ambapo nchi zote mbili zilitangaza kujiunga
rasmi na makubaliano ya Paris ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia
nchi.
Wakati wa
mazungumzo yao yaliochukuwa muda mrefu Xi aliihimiza Marekani kutimiza
dhima yenye tija katika kudumisha amani na utulivu katika eneo la Bahari
ya China Kusini.China inadai kumiliki takriban eneo lote hilo ambalo
pia linagombaniwa na Vietnam, Taiwan,Ufilipino,Malaysia na Brunei.
Nafasi ya vyombo vya habari yaleta tafrani
Mkutano
wa Xi na Obama ulitiwa kiwingu na mzozo kuhusu suala la vyombo vya
habari kuuangazia mkutano huo ambapo hapo Jumapili Rais Obama alikiri
kwamba kulikuwepo na mvutano kuhusiana na sisitizo la Marekani la
kujumuishwa kwa vyombo vya habari wakati wa Mkutano huo wa kilele wa
kundi la mataifa 20 ambapo amesema hatoomba radhi kwa kuvitetea vyombo
vya habari.
Akizungumza
katika mkutano huo Obama amesema "tunafikiri ni muhimu kwamba vyombo
vya habari vinapatiwa nafasi ya kuelewa kazi tunayoifanya ili wawe na
uwezo wa kujibu maswali. Hatuyaachi nyuma maadili yetu wakati
tunapofanya safari hizi."
Mzozo huo
ulianza mara baada ya kutuwa kwa ndege ya Air Force One katika mji wa
Hangzhou hapo Jumamosi ambapo kundi la waandishi wa Kimarekani
lililokuwa likiandamana na Rais Obama lilipozuiliwa wakati rais
alipokuwa akiteremka kwenye ndege ambapo afisa wa China aliwapigia
makelele wafanyakazi wa Ikulu ya Marekani kuwaondowa kabisa waandishi wa
habari katika eneo hilo.
Wakati
afisa wa Ikulu aliposema hilo lilikuwa ni suala linamhusu rais wa
Marekani na kwamba hiyo ilikuwa ni ndege ya Marekani kwa hiyo waandishi
hao wataendelea kubakia katika eneo hilo afisa huyo wa China alijibu kwa
ukali kwamba "Hii ni nchi yetu".
Afisa
huyo pia alipapurana na Mshauri wa Usalama wa Taifa Susan Rice na Naibu
Mshauri wa Usalama wa Taifa Ben Rhodes wakati walipokuwa wakijaribu
kutembea karibu na Rais Obama.Kuhusiana na kisa hicho Rice alisema
baadae "Wamefanya mambo ambayo hawakuyategemea."
Mvutano
huo uliendelea tena hapo Jumapili wakati sehemu ya mkururo wa vyombo vya
habari uliokuwa ukimsindikiza Obama ulipozuiliwa kukaribia eneo la
mapokezi la mkutano huo wa kilele wa G20.
Mbali na suala la ukuaji wa uchumi mkutano huo unatowa fursa kwa viongozi kujadili masuala mbali mbali muhimu duniani.DW
SHARE








No comments:
Post a Comment