
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Mamalaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma
Oktoba 6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya
Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa
Hazina mjini Dodoma Oktoba 6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya
Watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu CDA wakimsikilizwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa
Hazina mjini Dodoma Oktoba 6, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Kiwanja chauzwa kwa sh. milioni 240 lakini zilizoingia CDA ni milioni 6 tu
*Ahimiza kasi ya upimaji viwanja, asema waliolipa nusu wasinyang’anywe
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Bunge), Bw. Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa
na CDA kwa sh. milioni 240 lakini fedha iliyoingia ofisini ni sh.
milioni 6 tu.
“Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba
26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa sh. milioni 240
lakini fedha iliyoingia CDA ni sh. milioni 6 tu. Nataka kujua nani
ameingiza milioni 6 na nani kachukua hizo sh. milioni 234,” amesema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 6, 2016) wakati
akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Bila
kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu amesema eneo hilo lilipaswa kuwa na
kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia
amemwagiza Katibu Mkuu huyo afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la
CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa
mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha
juu.
Waziri
Mkuu amewaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao waache tabia ya
kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi
wakijielekeza na kasi ya Serikali ya kuhamia Dodoma.
“Tabia ya
watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata hivyo,
nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi
ya huduma. Ni lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya
kieletroniki, madalali hawana nafasi,” amesisitiza.
Ameutaka
uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni
makubwa lakini akaonya kuwa wakati zoezi hilo likifanyika, wananchi
walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa
kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.
“Mimi
nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie
fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu
Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” amesema.
“Kama mtu
amepewa offer au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu
asinyang’anywe. Ahimizwe kumalizia hilo deni na ninyi kazi yenu ni
kupima viwanja vingine,” amesisitiza.
“Natambua
mnayo benki ya viwanja, lakini inabidi muongeze idadi ya viwanja vingi
zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi,
mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,”
amesema.
Amesema
jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973.
Amesema kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka,
itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000
ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni.
Mapema,
akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Eng.
Paskasi Muragili amesema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika
na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni
2017.
Waziri
Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa
zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa
kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao
ambayo hata hivyo bado haijakamilika.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amepokea mchango wa zaidi ya sh. milioni moja
kutoka kwa Mkuu wa Wilaya wa Kongwa, Bw. Deogratius Ndejembi zikiwa ni
kwa ajili ya wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika kwa tetemeko la
ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.
Pia
Waziri Mkuu amepokea mchango mwingine wa zaidi ya sh. milioni tano
kutoka kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiasha wa Manispaa ya Dodoma
wakiwemo wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, waendesha bodaboda
na madereva wa daladala.
Akipokea
msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wafanyabiashara hao na
kuwahakikishia kwamba fedha hizo zitapelekwa mkoani Kagera na kuwafikia
walengwa kama ilivyokusudiwa. (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment