Mkuu wa
mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, kushoto akizungumza jambo na Mkuu
wa Wilaya ya Temeke, Felix Jackson Lyanivana pamoja na Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa na
Ofisa Habari, Jaffary Idd wakati alipofanya ziara katika klabu hiyo
Chamazi jijini Dar es salaam)
MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, leo mchana amefanya
ziara kwenye Makao Makuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati,
Azam FC akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa
wanazofanya za kuwekeza katika soka la Tanzania.
Mbali na
kuipongeza Azam FC inayomilikiwa na familia ya mmoja ya wafanyabiashara
maarufu Afrika, Alhaji Said Salim Bakhresa, pia ametoa shukrani zake
kutokana na jitihada zinazoonyeshwa na mfanyabiashara huyo mzawa katika
maeneo mengine aliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye tasnia ya habari (Azam
Media) na viwanda.
Kwenye
msafara huo, Makonda aliambatana baadhi ya viongozi wengine wa
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, alikofanya ziara tofauti kusikiliza
kero za wananchi wa wilaya hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya hiyo,
Felix Jackson Lyanivana.
Ugeni huo
ulipokelewa na viongozi wa juu wa Azam FC, wakiongozwa na Ofisa
Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa, Meneja
wa timu, Phillip Alando, ambao katika kumalizia ziara hiyo waliweza
kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa uwekezaji ndani ya
Azam Complex.
Akitoa
neno lake kwenye ziara hiyo, Makonda alisema haina ubishi kuwa Azam FC
ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwekeza ipasavyo kwenye soka huku akidai
kuwa timu hiyo imeshaanza kwa vitendo kutekeleza suala la kupunguza
idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini.
“Leo hii
mnatuunga mkono zaidi kwa sababu ni kiwanja kimoja na ni timu moja
ambayo kila mtu aliyeko Dar es Salaam anaizungumzia, katika suala zima
la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala
matumaini nyinyi Azam mmeshaanza kutekeleza kwa vitendo na watu wote
hatuwezi kuajiriwa serikalini, haiwezekani leo serikali ikaajiri watu
wote.
“Inawezekana
kabisa kila mtu na kipaji chake anaweza akafanya vizuri na mwisho wa
siku akaendesha maisha yake, kwa hiyo tunawashukuru sana sana sana Azam
FC,” alisema.
Makonda
alichukua fursa hiyo pia kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo
kujitokeza, na kuiga mfano wa watu wa Azam FC ili kuwa na timu nyingi
zenye ushindani na kuondoa migogoro kwenye soka la Tanzania.
“Waige
mfano wa Azam, watengeneze timu zao, watengeneze viwanja ili tuwe na
watu wengi, tuwe na timu nyingi zenye ushindani na hata hii migogoro
migogoro inayotokea Yanga na Simba, wenye hela zao wasihangaike, kama
wamegoma kukodishwa waje tu watengeneze timu zao ili na wenyewe
waendelee kunufaika kwa sababu mwisho wa siku tunajua tukiwa na timu
nyingi kama ilivyo Azam FC, ikapatikana timu nyingine ya watu wenye
uwezo kama nyie mnavyowajali vijana wenu ushindani utakuwa mkubwa sana.
“Na hivyo
ndivyo tunaweza kuweka vijana wengi wakawa kwenye vipaji vyao tukajenga
uchumi wetu kupitia ajira inayotokana na michezo na mwisho wa siku
tukapeperusha vema bendera ya Taifa letu katika mataifa mbalimbali
katika sekta nzima ya michezo, mimi naamini kwa kazi na mfano
mnaoonyesha niwaombe watu wengine waendelee kuiga,” alisema.
Katika
ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Makonda amewaomba Watanzania
waendelee kununua bidhaa zinazotengenezwa na wazawa akitolea mfano
baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na makampuni ya Bakhresa.
“Mfano
kama hivi viwanda vyenu vinatengeneza juisi, mnatengeneza maji,
mnatengeneza ngano, walioajiriwa ni Watanzania wenzetu kwa hiyo kadiri
mnavyouza bidhaa zenu manake kuna uhakika wa kupanua biashara, mkipanua
biashara wadogo zetu, kaka zetu wanapata ajira lakini la pili mkiendelea
kuuza mnalipa kodi, ile kodi tunapata barabara, madawa, tunapata shule,
tunapata kila kitu tunachokitafuta,” alisema.
Naye
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akizungumza kwa niaba ya
uongozi wa Azam FC, alimshukuru Makonda kwa ugeni wake huo ndani ya
klabu hiyo, huku akichukua fursa hiyo pia kumwelezea historia fupi ya
Azam tokea ianzishwe mwaka 2004 hadi ilipo mpaka sasa.
Mbali na
historia, alimweleza timu mbalimbali zilizoko ndani ya Azam Complex,
timu ya vijana (U-20) na ile ya wakubwa pamoja na mipango kabambe
inayoendelea ya kuunda timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15 na
17, mchakato unaoelekea ukingoni ukihusisha mikoa mbalimbali.
“Baada ya
michuano ya Copa Coca Cola kutokuwa na mwelekeo, kama klabu tumeamua
kuwafuata vijana kule walipo tumefanya majaribio katika mkoa wa Dar es
Salaam, tumekwenda Zanzibar, Tanga, Morogoro na wiki iliyopita tulikuwa
mkoani Mbeya tulikopata vijana saba, bado tutaendelea kufanya uwekezaji
tutaenda mkoani Tabora, Mwanza, Kigoma na Mtwara,” alisema.
Aliongeza
kuwa: “Kwa hiyo sisi tunaamini ya kuwa hata Mheshimiwa hapa Mkuu wa
Mkoa utakuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa wa kutusapoti na karibu
sana Azam FC usichoke kuja wakati wowote…Yote tunayoyafanya ni kutokana
na kampuni mama ya Azam na wadhamini wetu ambao ni Benki ya NMB lakini
haitoshi kwa hiyo tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni mengine ambayo
yanaweza kuona nafasi ya wao kuwekeza waje, tuna timu za vijana, njooni
mfanye kazi na sisi tuweze kusomba mbele.”(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment