Rais
mteule wa Marekani Donald Trump amesema ataiondoa nchi yake katika
Mkataba wa Biashara Huria Ukanda wa Pasifiki-TPP, siku yake ya kwanza
kazini; mojawapo ya ahadi kuu za kampeni yake kuelekea uchaguzi wa
Novemba 8.
Hayo
yameelezwa katika mkanda wa vidio ambamo ameyataja mambo yenye
kipaumbele atakayoanza kuyafanya katika kipindi cha siku 100 za mwanzo
baada ya kuingia Ikulu, tarehe 20 Januari mwakani.
Wakati wa
kampeni yake Donald Trump aliahidi kuiondoa Marekani katika mikataba 12
ya kibiashara, ambayo aliilaumu kwa ukosefu wa nafasi za ajira kwa
Wamarekani.
''Nimeitaka
timu yangu ya mpito kuandaa orodha ya hatua tutakazozichukua siku ya
kwanza baada ya kuchukua hatamu za uongozi, katika kurejesha utawala wa
sheria na kurudisha fursa zetu za kazi'', amesema Trump katika ujumbe
wake huo na kuongeza kuwa ''kuhusu biashara, nitatoa ilani ya kujiondoa
katika mkataba wa TPP, ambao ni janga linasubiri kutokea kwa nchi
yetu.''
Kiama kwa mipango ya Obama
Trump
amesema badala ya mkataba huo, atajadili mikataba bora ambayo itarudisha
viwanda katika ardhi ya Marekani, vikiambatana na fursa za kazi.
Mkataba
wa TPP ulikuwa suala muhimu katika utawala wa Rais Barack Obama,
ukidhamiria kuimarisha biashara kati ya Marekani na nchi za bara Asia,
na ulionekana kama mfano utakaofuatwa na mikataba mingine ya aina hiyo,
ukiwemo ule kati ya Marekani na nchi za Ulaya, maarufu kama TTIP.
Maoni ya
wengi ni kwamba mikataba ya aina hiyo ni sababu kuu ya kuzihamishia
katika mataifa ya nje, kazi ambazo zingeweza kufanywa na Wamarekani.
Japan yatoa kauli yake
Kufuatia
tangazo la Donald Trump, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, amesema
mkataba wa TPP bila Marekani hautakuwa na maana tena. Abe ambaye
alihudhuria mkutano wa kilele wa nchi wanachama wa mkataba huo mjini
Lima, Peru mwishoni mwa juma lililopita, amesema viongozi katika mkutano
huo hawakujadili hatua za kuiendeleza TPP baada ya Marekani kujiondoa.
Kiongozi
huyo wa Japan amesema pia kuwa hakutakuwa na haja ya kuujadili upya
mkataba huo, kwa sababa hatua hiyo inaweza kuuharibu msingi wa urari wa
faida.
Japan
vile vile ina wasiwasi kwamba Trump anaweza kutekeleza ahadi yake
nyingine ya wakati wa kampeni, ya kuiitaka Japan ilipie zaidi gharama ya
wanajeshi 50,000 wa Marekani walioko nchini humo, kulingana na
makubaliano ya kiusalama. Kwa wakati huu Japan hulipa nusu ya gharama ya
kuwepo kwa wanajeshi hao.
Mwanzo wa ''nadharia za Trump''
Tangazo
la Trump limeyagusia maeneo mengine muhimu ya sera zake, likiwemo lile
la uhamiaji. ''Nitatoa amri kwa maafisa wa wizara ya kazi, kufanya
uchunguzi kuhusu ukiukaji wa sheria za visa, ambao unawaathiri
wafanyakazi wa kimarekani'', amesema.
Aidha,
amesema bayana kwamba mojawapo ya masuala ya kiusalama atakayoyawekea
mkazo, ni ''kuunda mpango mahsusi wa kuilinda miundombinu ya marekani
dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, na aina nyingine zote za
mashambulizi'', kwa ushirikiano na wizara ya ulinzi, na makamanda wakuu
wa kijeshi.
Ama
kuhusu ahadi yake ya mageuzi ya kimaadili, Trump amesema ataanzisha
marufuku inayowazuia waliowahi kuwa viongozi wakuu wa nchi, kuwakilisha
maslahi ya nchi za kigeni katika kipindi chote cha uhai wao.
Kitu
kingine alichokitupilia mbali Trump katika ujumbe wake, ni wasiwasi juu
yake kuhusu sekta ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. ''Nitavipiga
mkasi vizuizi vyovyote vinavyoua nafasi zetu za ajira'', ametishia. DW
SHARE
No comments:
Post a Comment