Vyama
vya Ushirika vimetakiwa kushiriki katika kuanzisha viwanda vidogovidogo
ambavyo vitawezesha uchakataji wa mazao ya wakulima, wavuvi na
wafugaji, kuweka kwenye madaraja na kufungasha tayari kwa ajili ya
mauzo.
Wito
huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume
ya Maendeleo ya Ushirika nchini Bw. Tito Haule katika Ufunguzi wa Kikao
Kazi cha Warajis Wasaidizi Wa Vyama Vya Ushirika Wa Mikoa kilichofanyika
leo mjini Dodoma Novemba 15, 2016.
“Sekta
ya Ushirika ina mchango mkubwa katika kuwezesha kutimia kwa azma ya
Serikali ya kukuza uchumi, hivyo kila mmoja wetu katika eneo lake tuweke
msukumo katika vyama vya ushirika ili viweze kuwa sehemu ya utekelezaji
wa azma hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuipeleka nchi yetu katika
uchumi wa viwanda ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza kasi ya
kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025,” alisema
Mrajis.
Viwanda
vinavyomaanishwa siyo lazima viwe viwanda vyenye kuhitaji mitambo
mikubwa bali vinaweza kuanzishwa viwanda vidogovidogo ambavyo
vitawezesha uchakataji wa mazao.
Bw.
Haule akizungumzia kuhusu majukumu yatakayopewa kipaumbele na Tume ya
Maendeleo ya Ushirika alisema ni kusimamia na kudhibiti badala ya kuwa
wasuluhishi wa migogoro katika Vyama vya Ushirika.
“Sote
tunafahamu kwamba kuna udhaifu mkubwa katika eneo la usimamizi na
udhibiti wa vyama vya ushirika na hivyo kusababisha utii wa sheria
kutozingatiwa katika uendeshaji wa shughuli za vyama vya ushirika.
Hivyo, kipaumbele changu cha kwanza ni Usimamizi, cha pili ni Usimamizi
na cha tatu ni Usimamizi”, alisema Bw. Haule.
SHARE
No comments:
Post a Comment