Makamu wa
Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko
Suzuki (kulia), akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo
Pichani), alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye Ofisini kwake Jijini
Dar es salaam. Katikati ni Mwakilishi Mkuu Mkazi wa JICA nchini
Tanzania, Bw. Toshio Nagase na kulia ni Afisa wa Shirika hilo
anayeshughulikia masuala ya usafiri na usafirishaji Bi. Lilian Masalu.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kulia),
akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumzia umuhimu wa Nishati ya
umeme katika kuchochea maendeleo ya viwanda nchini, wakati alipokutana
na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA)
Bi. Noriko Suzuki, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini dar
es salaam.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia), akizungumzia
namna Serikali ya Tanzania ilivyojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya
kipaumbele ikiwemo ujenzi wa viwanda mbele ya Makamu wa Rais wa Shirika
la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki (hayupo
pichani), alipomtembelea na kufanya naye mazungumzo ofisini kwake Jijini
Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria Bw.
Elias Kalist, na kulia kwake ni Mchumi Mkuu, Yosephe Tamamu, wote kutoka
Wizara ya Fedha na Mipango.
Mchumi
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Yosephe Tamamu (kushoto),
akifafanua jambo katika kikao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki. Aliyekaa kulia ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria wa Wizara hiyo Bw. Elias Kalist.
Makamu wa
Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko
Suzuki, akizungumza katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo pichani), kuhusu ushirikiano wa
kimaendeleo kati ya Tanzania na Japan, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na
Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimsindikiza mgeni
wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan
(JICA) Bi. Noriko Suzuki, baada ya kufanya mazungumzo namna pande hizo
mbili zitakavyoimarisha ushirikiano uliodumu muda mrefu katika Nyanja
mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), (kulia) akifurahia
jambo na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa
la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, kabla ya kuondoka baada ya kufanya
mazungumzo namna pande hizo mbili zitakavyoimarisha ushirikiano uliodumu
muda mrefu katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kulia ni
Mwakilishi Mkuu mkazi wa JICA hapa nchini, Toshio Nagase. (Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano-WFM)
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Makamu wa
Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko
Suzuki, amesema kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika
Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili iweze kufikia malengo yake
ya kuondokana na umasikini.
Suzuki
ametoa ahadi hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ofisini Kwake Jijini Dar salaam.
Makamu
huyo wa Rais wa JICA, amesema kuwa nchi yake inatumia zaidi ya dola za
Marekani Milioni mia moja kila mwaka kusaidia shughuli mbalimbali za
maendeleo hapa nchini katika sekta za miundombinu ya barabara, maji,
nishati, afya na kilimo.
Miongoni
mwa miradi mikubwa inayofadhiliwa na serikali hiyo ya Japan ni barabara
ya juu ya mzunguko inayojengwa katika makutano ya barabara katika eneo
la Tazara, Jijini Dar es salaam.
“Tuko
tayari kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza Mpango wake wa Pili wa
Taifa wa Maendeleo kwa kuwekeza fedha katika miradi mbalimbali ya
maendeleo mliyoipa kipaumbele kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya
kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025” alisisitiza Makamu huyo wa Rais
wa JICA.
Ameahidi
kuwa Shirika lake pia linaagalia uwezekano wa kuishirikisha sekta
binafsi nchini Japan kujenga barabara katika eneo la Gerezani ili
kupunguza msongamano mkubwa wa magari hasa yanayotoka Bandari ya Dar es
salaam na Katikati ya Jiji la Dar es salaam.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa
uhusiano kati ya Japan na Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba nchi hiyo
imekuwa mdau wake mkubwa wa maendeleo.
Amesema
katika mazungumzo kati yake na Makamu huyo wa Rais wa JICA,
wamekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara eneo la Bendera tatu na Gerezani
ili kupunguza msongamano wa magari kutoka katikati ya Jiji la Dar es
salaam
“Mradi
Mwingine ni ujenzi wa barabara kutoka eneo la Moroco hadi Mwenge, Jijini
Dar es salaam, ambayo Japan waliahidi kuijenga muda mrefu uliopita”
Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema
kuwa wamekubaliana pia kwamba Shirika hilo lisaidie kufungua ukanda wa
Kati kwa kujenga barabara ya Kigoma-Nyakanazi na Kigoma-Mto Malagarasi,
ambazo hazijapata mfadhili mpaka sasa.
“Halikadhalika
nimemwomba atusaidie kuhamasisha sekta binafsi nchini Japan kuja
Tanzania kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa
tiba ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho serikali inatumia
kuagiza dawa nje ya nchi na pia itakuwa chanzo cha ajira kwa vijana”
alisisitiza Dkt. Mpango
Waziri
huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametaja eneo lingine kuwa
ni kuiomba Japan iongeze fursa ya mafunzo kwa vijana wa kitanzania
katika nyanja za tiba na ujuzi maalumu ambao haufundishwi hapa nchini.
Amesema
kuwa ameiomba pia nchi hiyo ya Japan iendelee kusaidia sekta ya kilimo
inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania kwa kusaidia kuongeza
uzalishaji na kusindika mazao ya wakulima ili kuyaongezea thamani.
Katika
majadiliano hayo, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la
Japan Noriko Suzuki, aliiomba Serikali ya Tanzania itoe msamaha wa kodi
kwa miradi miwili mikubwa inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali
kupitia shirika hilo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo na mradi wa
maji mkoani Tabora, maombi ambayo amesema Serikali itayafanyiakazi.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment