Kaimu
Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri anayeongoza timu
ya ukaguzi wa miradi kutoka Tume ya Mipango akielekea kukagua mradi wa
ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa katika
eneo la Narunyu wilayani Lindi. Kulia ni Bi, Yasinta Mrose (Mtawa)
ambaye anasimamia upande wa mifugo.
Kaimu
Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akitoa ushauri kwa
uongozi wa mradi ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa (ambao ni
watawa) katika moja ya mabanda ya ng’ombe wa maziwa. Wengine ni maofisa
wa Serikali walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji huyo.
Baadhi ya
ng’ombe wa maziwa wa mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa
unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wakiwa katika banda.
Bi
Yasinta Mrose (Mtawa) akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango, Florence Mwanri hatua za awali za kutengeneza gesi kwa kutumia
kinyesi cha ng’ombe.
Kaimu
Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Florence Mwanri akiwa ndani ya chumba
ambapo gesi inazalishwa (gesi ipo ndani ya turubai lililojaa ndani ya
chumba hicho linaloonekana chini).
Mwonekano wa Kiwanda cha kuzalisha nishati inayotokana na kinyesi cha ng’ombe.
Ndama
wanaofugwa katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa
unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wakiwa katika banda. PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO
Na Adili Mhina, Lindi
Tume ya
Mipango imefanya ziara katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa
maziwa unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wilayani Lindi na
kushauri uongozi wa mradi huo kutumia fursa za mikopo ya kilimo ili
kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya mifugo pamoja na kuongeza
uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia kinyesi cha wanyama.
Mradi huo
umekuwa ukizalisha maziwa na nyama kwa ajili ya biashara huku nishati
ya umeme kwa ajili kuendesha shughuli za kiwanda hicho ikiwa inazalishwa
kutokana na kinyesi cha wanayama hao.
Kwa sasa
uzalishaji umepungua baada ya kiwanda kushindwa kuzalisha nishati ya
umeme ya kutosha na kuanza kutegemea umeme wa tanesco ambao kwa mujibu
wa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, Bi Yasinta Mrose umesababisha
gharama za uzalishaji kuongezeka.
Changamoto
nyingine ni kuharibika kwa baadhi mashine zinazotumika kuandaa malisho
ya ngo’ombe, ukosefu wa soko la karibu kwa mazao ya nyama na maziwa,
pamoja na uhaba wa maeneo kwa ajili ya malisho ambapo kwa sasa mradi una
zaidi ya ng’ombe 400.
Kutokana
na changamoto hizo, Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence
Mwanri aliueleza uongozi huo kuwa ni vyema wafanye taratibu za kuomba
mkopo hususani katika benki ya kilimo ili waweze kuongeza mtaji,
uzalishaji na kupanua soko.
“Huu ni
mradi mzuri na msirudi nyuma katika uzalishaji wenu, nawashauri mkae
mjadiliane muone namna ya kupata mkopo ili muweze kununua mashine za
kisasa na muongeze uzalishaji. Bila kuchukua hatua hizo mnaweza
mkashangaa mradi unakufa wakati unafaida kwenu na hata kwa wananchi
wanaowazunguka,” alieleza.
Kuhusu
changamoto ya soko la karibu, Mwanri alieleza kuwa uongozi unapaswa
kufikiria kuzalisha maziwa na kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa
na kusafirisha nje ya wilaya ya Lindi kwani soko bado ni kubwa.
Aliongeza
kuwa hatua iliyofikiwa ya kuzalisha umeme wa kutosha kuhudumia shughuli
zote za uzalishaji kiwandani hapo ni nzuri na Serikali inaiunga mkono
jitihada za sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya uchumi ikiwa ni
njia ya kutekeleza malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2016/17-2020/21).
“Nimefarijika
sana kusikia mlikuwa mnazalisha umeme wa kuwatosheleza, mmejitahidi
kutekeleza mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa vitendo. Tume ya Mipango
inatambua na kuunga mkono jitihada zenu hivyo nawasihi shirikianeni na
Halmashauri kufanya kila linalowezekana ili shughuli zenu ziendelee
zaidi ya mlivyokuwa mnazalisha huko nyuma,” aliongeza.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment