Tuna safari ndefu kukabili adui Ukimwi
Julian Msacky
SIKU hizi watu wanasema ugonjwa wa
Ukimwi si tishio kubwa nchini kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Ugonjwa huo ulipogundulika kwa mara ya kwanza
mwaka 1983 eneo lililoathirika ni Mkoa wa Kagera.
Wakati huo ulikuwa haujafahamika kwa
watu wengi hivyo hata namna ya kujikinga ilikuwa ni tatizo kubwa.
Ilifikia hatua waliogundulika kuwa nao
walitengwa na kunyanyapaliwa kuanzia ngazi ya familia. Hali ilikuwa mbaya.
Tunashukuru teknolojia ya kisasa na
elimu vimesaidia kwa kiwango kikubwa kufahamu ugonjwa huo na dalili zake.
Elimu inatolewa namna ya kuuepuka,
kujikinga, kutumia dawa na mambo mengine mengi ya kuzingatia.
Pamoja na hayo hatutakiwi kukaa na
kufurahi kwamba tatizo limepungua. Bado tuna safari ndefu kukabili adui.
Ripoti mbalimbali zinaonesha vijana
wenye umri wa kuanzia miaka 19 hadi 24 maambukizi yapo juu. Hii ni hatari.
Kundi hili linaweza kusababisha
maambukizi yakasambaa kila kona na kuwa hatari kwa nchi na watu wake.
Ni kwa namna gani tunalinda kundi hili
ili tubaki salama? Haitoshi kusema maambukizi kitaifa yamepungua.
Tunaambiwa kiwango cha maambukizi mapya
ya virusi kimeshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 5.3.
Yapo maswali mengi yanaendelea kuulizwa
kama kweli takwimu hizo zinatoa picha halisi ya ugonjwa au la.
Wapo wanaojenga hoja kuwa kiwango cha
ufanyaji ngono ni kikubwa mno na wakati mwingine kinga hazitumiki.
Kama hiyo haitoshi yapo makundi maalumu
(key population) ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa umakini.
Je, tunayafahamu? Kama tunayafahamu
tunawakubali namna walivyo? Kama tunawakubali tunawasaidiaje?
Tunaposema makundi maalumu ni
walioathirika na Virusi Vya Ukimwi (VVU) kuliko mengine ndani ya jamii.
Kuna wanaofanya biashara ya ngono (sex
workers). Hawa tunakimbizana nao kila mara mitaani. Je, inatosha?
Wakifukuzwa leo Kigamboni watakimbilia
Bunju. Wakifukuzwa Bunju watakwenda Temeke.
Huo ni mzunguko hatari na tusipotafuta
tiba ya kudumu mapambano dhidi ya Ukimwi bado yatatusumbua.
Haitoshi kuhamisha tatizo sehemu moja na
kulipeleka kwingine. Ni lazima tutafute ufumbuzi wa kudumu.
Wanaojiuza wanagusa maisha ya kila mmoja
wetu. Kusema hawatuhusu au kukimbizana nao mtaani haisaidii.
Huu ni upande mmoja hivyo badala ya
kukimbizana nao tuwatafute, tukae nao na kuwasiliza ili kupata ufumbuzi.
Tukumbuke pia wapo wanaume wanaofanya
michezo hiyo na wanaume wenzao na wanawake vivyo hivyo.
Ni tatizo pana. Wapo wanaojidunga
sindano na kujikuta wakijiambukiza virusi. Huu ni mzunguko wa hatari.
Kwa msingi huo sisi kama nchi ni lazima
tujipange kama kweli tunataka kukomesha maambukizi mapya.
Sisi kama nchi tutambue makundi hayo na
kuhakikisha tunayasaidia ili kudhibiti maambukizi yasiendelee.
Hivi sasa tunazungumzia habari ya Tanzania
bila maambukizi mapya ya VVU, vitokanavyo na Ukimwi na ubaguzi, unyanyapaa inawezekana.
Ni jambo jema hasa wakati huu ambao
tumejiwekea Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Milenia (MSDG) ifikapo mwaka
2030.
Ifikapo mwaka huo maambukizi ya virusi
vya Ukimwi kitaifa na kimataifa yanatakiwa yawe sifuri.
Hii ikiwa na maana kuwa maambukizi mapya
sifuri, vifo vya Ukimwi sifuri na unyanyapaa sifuri. Je, tutaweza?
Hii ina maana gani? Tuna jukumu kama
nchi kuhakikisha maambuzi hayaongezeki zaidi ya hali iliyopo sasa.
Ili kufikia hapo ni lazima kazi kubwa
ifanyike. Hili ni jukumu la kila mtu, taasisi, serikali na wadau wengine.
Kwa maana nyingi kuna umuhimu wa
kuhakikisha vichecheo vya ugonjwa huo vinadhibitiwa kwa ustawi wa nchi.
Ni vizuri kuangalia hali ya umaskini
nchini kwetu kuanzia ngazi ya familia hadi taifa unavyochangia maambukizi.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa umaskini
umesukuma watu wengi kujikuta kwenye maambukizi ya VVU.
Swali ni je, sisi kama nchi tumejipanga
vipi kuhakikisha adui huyo anatokomezwa ili kulinda uhai wetu.
Jambo jingine la kuangalia ni tiba na
vidhibiti virusi. Je, tuna dawa za kutosha kwa ajili ya waathirika?
Vifaa vya kujikinga vipo vya kutosha
nchini au ni mchezo wa kutumia mpira huu na kumuazima mwingine?
Mambo ni mengi, lakini itoshe kusema
kuwa hapa tulipofikia si mahali pabaya muhimu tusibweteke.
SHARE
No comments:
Post a Comment