TRA

TRA

Friday, March 31, 2017

Mgororo wa Palestina na Israel, Trump ana ubavu?

No comments:


Julian Msacky

KAMA kuna mgororo unaisumbua dunia kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi ni wa Israel na Palestina.

Umoja wa Mataifa (UN) umesalimu amri. Mataifa ya Magharibi yanaugusagusa na kuacha ulivyo. 

Ni sawa na mfupa uliomshinda fisi. Swali sasa ni je, nani atamaliza mzozo huo? Ni viongozi wa kiserikali au dini?  

       RAIS DONALD TRUMP

Je, UN na mataifa mengine yataendelea kuangalia namna Wapalestina na Waisrael wanavyonyukana kila mara?

Historia inaonesha kuwa mgogoro huo umejikita katika masuala ya kidini hivyo ufumbuzi wake ni utata mtupu.

Tunaambiwa kuwa wakati Waisrael wakiwa utumwani Misri kuna nchi ilikuwa na asali na maziwa.

Nchi hiyo (Palestina?) ilikuwa na kila kitu, inapendeza, yenye rutuba na hakika ilikuwa ni kama paradiso.

Walipokuwa nchini Misri wana wa Israel walilalamika kuteswa hivyo wakamlilia Mungu ili awaokoe.

Mwenyezi Mungu akafanya hivyo kwa kumtumia Nabii Musa na kwa mkono wa Mungu aliwaondoa Misri.

Baada ya kufanya hivyo aliwaongoza Waisrael kwenda nchi ya ahadi.

Wakiwa tena njiani walipata mateso makali jangwani na shida zilipozidi walitamani Musa awarudishe Misri.

Mateso yalipokolea Waisrael waliamua kujitengenezea miungu ya shaba na kumweka pembeni Mungu wao.

Mwenyezi Mungu alichukizwa na tabia hiyo na kuvunja agano na wana wa Israel licha ya kuwa ni taifa teule.

Kadri siku zilivyosogea umri wa Musa nao ulisogea na alipofikisha miaka 120 alifariki dunia. Hakuona nchi ya ahadi.

Kwa sababu hiyo Waisrael walibaki wakirandaranda jangwani hadi nabii Joshua alipochukua nafasi ya Musa. 

Hii ilikuwa ni safari ndefu yenye majaribu mengi ili kupima imani ya Waisrael kwa Mwenyezi Mungu.


Kutokana na hali hiyo mgogoro wa Israel na Palestina unahitaji mkono wa Mungu kutuliza mzimu wa mababu. 
 
Hakuna mwenye jibu la moja kwa moja kama yupo kiongozi wa kisiasa au dini anayeweza kuleta amani maeneo hayo.

Amani ya kweli itapatikana endapo haki isipotamalaki na mkubwa kumheshimu mdogo ili kuondokana na mapambano ya Goliathi na Daudi

Bila kufanya hivyo Wapalestina wataendelea kujihami kwa kila mbinu ili kuzuia uvamizi katika ardhi yao. 

Kama zilivyo nchi nyingine Palestina inahitaji kutambuliwa na kupewa hadhi badala ya kunyanyapaliwa.

Kauli ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba:  

“Katika makubaliano yoyote ya amani, Israel lazima iwe na uwezo wa kudhibiti usalama katika eneo lote la Magharibi mwa mto Jordan”.

Eneo hilo linahusisha ukingo wa Magharibi na ni kitovu cha taifa la Palestina linalotarajiwa kuundwa kulingana na makubaliano ya kimataifa.

Ikumbukwe kwamba kilio kikubwa cha Palestina ni kuonewa pamoja na kuporwa haki zao asilia (ardhi) hivyo kubaki kama watoto yatima.

Pengine ni kwa kutambua ugumu wa mgogoro huo ndiyo maana Rais wa Marekani, Donald Trump alisema:

“Uongozi wangu unaunga mkono uundwaji wa taifa moja ili kumaliza mzozo wa Israel na Palestina,”.

Anachosema Trump nacho ni tatizo kwa sababu ni nani kati ya Palestina na Israel atakubaliana na hilo?

Ukimsikiliza Netanyahu ni kana kwamba anataka Israel imiliki eneo lote linalokaliwa na Palestina.

Tusisahau kuwa hivi sasa Israel inafikiria kuanzisha makazi mapya 6000 ingawa haifamiki yatatoka eneo la Palestina au la. 

Huu ni mgogoro mwingine kama nilivyogusia katika mada iliyopita. Hii inaonesha hali bado si shwari. 

Kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu wa Israel alimwambia Trump lazima Wapalestina waitambue Israel kama taifa la Kiyahudi na kutambua haki ya Israel kusimamia usalama katika eneo zima.

Hata hivyo, Trump alionekana kutomuunga mkono Netanyahu kuhusu suala hilo hususan eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa lugha nyingine Trump amevunja utamaduni wa viongozi wa Marekani kuikumbatia Israel. Hii inaashiria nini? 

Tuseme kwamba ile dhana kuwa ukimuona Mwisrael umemuona Mmarekani na ukimuona Mmarekani umemuona Mwisrael inafutika?

Pengine tukubaliane tu na ushauri wa Rais Trump kuwa pande zote mbili zinahitaji kuwa na maridhiano. 

Ni kwa njia hiyo pekee amani ya kweli itapatikana kati ya Wapalestina na Waisrael na si vinginevyo.

Lakini viongozi wakitanguliza jazba na ubabe kama anavyotaka Netanyahu badala ya amani ni vita.

TANZIA: Dr. Elly Macha mbunge wa viti maalum kupitia CHADEMA afariki dunia

No comments:


Taarifa zilizotufikia hivi punde nikwamba Dkt. Macha, Mbunge wa CHADEMA Viti Maalum akiwakilisha watu wenye ulemavu amefariki dunia leo. R.I.P Dokta Elly Macha.

DKT. KALEMANI ATAJA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA 2016/17

No comments:




Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, Dkt. Medard Kalemani akiongea jambo wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2016/17.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dotto Biteko, akichangia Hoja baada ya Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2016/17 kuwasilishwa kwa Kamati.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Susan Kiwango akichangia Hoja baada ya kuwasilishwa Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2016/17.
Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Mhe. Oscar Mkasa akichangia jambo wakati wakati wa kikao baina ya Kamati na Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake, ambapo Wizara na Taasisi ziliwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2016/17.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gisima Nyamo- Hanga, akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya REA kwa mwaka 2016/17 kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2016/17 ya shirika hilo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Haji Janabi, akiwasilisha Taarifa ya Utekelzaji wa Wizara kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baadhi ya Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakifuatilia kikao baina ya Wizara ya Nishati na Madini na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

…………………………………………………………………..

Wizara ya Nishati na Madini imekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuanzia tarehe 27 Machi, 2017, ambapo Wizara na Taasisi zilizo chini yake zimewasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2016/17.

Akielezea baadhi ya mafanikio ya Wizara kwa Kamati ya Bunge, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na;
 
Kukamilika kwa asilimia 100 kwa Mradi wa Kusafirisha Umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga wenye msongo wa kilovoti (kV), 400.

Kukamilika kwa asilimia 98.5 ya Awamu ya Pili ya Mradi Kambambe wa Kupeleka umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini- REA.
Kuzinduliwa rasmi kwa Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kupeleka umeme Vijijjini unaolenga kusambaza umeme katika vijiji vyote visivyofikiwa na huduma hiyo.
 
Kukamilika kwa Kanuni za:
The Petroleum (Retail Operations in Townships and Villages) Rules,2016
The Petroleum (Natural Gas Pricing) Rules,2016
The Electricity (Supply Services) Rules, 2016

The Electricity (Market re- organization and competition) Rules,2016 na
The Mining (Minimum shareholding and Public Offering) Regulations 2016. Kanuni hizi zinasimamia utekelezaji wa Sheria zinazohusu Sekta za Nishati na Madini.

Kuanza kwa maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania.

Kuendeleza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini ambapo hadi sasa jumla ya Futi za Ujazo Trilioni 57.25 za gesi asilia zimegunduliwa.
Kukamilisha utafiti wa jio-sayansi (jiolojia, jiokemia na jiofikizia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na kuchora ramani za kuanisha kuwepo kwa madini mbalimbali ili kuhamasiaha uwekezaji kwenye maeneo ya Nachingwea, Ruangwa na Masasi.

Wizara kutenga maeneo 11 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo yaliyopo Msasa na Matabe Mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa yaliyopo Mkoani Kagera, Itigi, Mkoani Singida, D- Reef, Ibindi na Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa Mkoani Songea, Nzega Mkoani Tabora na Kitowelo Mkoani Lindi. Maeneo hayo yana ukubwa wa takriban hekta 38.567
 


Kufanyika kwa minada miwili (2) ya madini ya vito hususan tanzanite jijini Arusha ambapo Serikali ilipata jumla ya shilingi milioni 793 ikiwa ni mrabaha uliolipwa Serikalini kutokana na minada hiyo.

Watumishi Wa OSHA Wapewa Changamoto

No comments:


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwahutubia wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kikao chao cha baraza. Kulia ni Kaimu  Mtendaji Mkuu wa Wakala Bi. Khadija Mwenda na viongozi wa baraza hilo. 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mara baada ya kufungua kikao chao cha baraza.) 
Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi (hayupo pichani) alipofungua kikao cha baraza lao mjini Dodoma jana.


Mabadiliko ya mazingira ya ufanyaji biashara yanayoletwa na maendeleo ya uchumi wa viwanda pamoja na mnyororo wa thamani, yameelezwa kuwa changamoto kubwa katika jitihada za kuimarisha hali ya usalama na afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi hapa nchini.

Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Bw, Eric Shitindi, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mjini Dodoma leo.

Amesema mabadiliko hayo yanahusisha matumizi ya teknolojia za kisasa na ongezeko kubwa la idadi ya wafanyakazi katika sekta zote za umma na za binafsi jambo ambalo linahitaji utaalamu mkubwa katika kuweka na kusimamia mifumo ya kulinda afya na kuwahakikishia usalama wafanyakazi wote wanapokuwa katika sehemu zao za kazi.

“Hivyo mkiwa kama wataalamu katika masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi mnatakiwa kuwa na mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto hizo. Hii itakuwa ni pamoja na kubadilika kifikra na kimtazamo katika utendaji kazi,” alisema Katibu mkuu Shitindi.

Katibu mkuu huyo amesisitiza muhimu wa kutafuta mbinu mbadala ya kuweza kupanua wigo wa kufanya kazi hasa kwa kuzingatia ukubwa wa kazi zilizopo.

Aidha Bw. Shitindi ameupongeza OSHA kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango kazi wake katika kipindi cha robo tatu za mwaka huu wa fedha (2016/2017) ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika baraza hilo, taasisi imevuka malengo katika kaguzi, utoaji wa mafunzo ya usalama na afya kazini pamoja na huduma mbali mbali zitolewazo mahali pa kazi.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu aliahidi kuendelea kuisaidia OSHA kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za kiutendaji na kuwaasa watumishi wa Wakala kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepuka kujihusisha na vitendo vya upokeaji rushwa wanapotekeleza majukumu yao.

“Wizara imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya namna mnavyohudumia wateja na kushuka kwa maadili ya kiutendaji miongoni mwa watumishi, mfano masuala ya rushwa, hivyo wakati tunaendelea kushughulikia matatizo hayo ni vyema sasa mkaanza kubadilika kwa kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali ya utendaji kazi katika taasisi,” amesisitiza Bw, Shitindi.

Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi wa OSHA ambacho kimeanza leo kitamalizika kesho ambapo pamoja na mambo mengine kitapitia na kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha wa (2017/2018) ili kujiridhisha kama itawawezesha kufanikisha utekelezaji wa malengo ya wakala yaliyowekwa

Wanawake, vijana tegemeo katika kumaliza machafuko nchini Somalia

No comments:


Mane Ahmed, Ofisa Jinsia kutoka African Union Mission in Somalia (AMISOM) akizungumza na waandishi.

Washiriki wa mkutano wakifuatilia mada zilizowasilishwa.


Wanawake na vijana ni nyenzo muhimu katika uhamasishaji wa kumaliza machafuko yanayoendelea nchini Somalia, wakati kundi hilo pia likilengwa zaidi na vikundi vya kigaidi kutumika katika matukio ya kigaidi.

Hayo yamebainishwa na Mane Ahmed, Afisa Jinsia kutoka African Union Mission in Somalia (AMISOM), wakati wa mkutano wa siku tatu unaomalizika leo (Ijumaa) jijini Dar es Salaam jana.

Mkutano huo ulioandaliwa na AMISOM kwa ushirikiano na serikali ya Somalia unalenga kutafuta njia stahiki za kuzuia vijana kudahiliwa na vikundi vya kigaidi nchini humo.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umebainisha umuhimu wa ujengaji uwezo kama hatua madhubuti katika kueneza hali ya kuvumiliana ndani ya jamii na kuwapa sifa mbaya Al-Shabaab.

Akizungumza mkutanoni hapo, Bi Mane amesema kuwa Serikali ya Somalia imeanzisha ofisi ijulikanayo kama Counter-Violent Extremism (CVE) ikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kukamilisha rasimu ya kwanza ya Sera ya Kuzuia na Kupambana na Vikundi vyenye msimamo mkali.

Bi Mane alisema kuwa AMISOM imeanzisha Mtandao wa Kijinsia ambao umelenga katika kuzuia na kupambana na vikundi vyenye msimamo mkali kwa lengo la kusaidia juhudi za Shirikisho katika kuunganisha mtazamo wa kijinsia katika mpango na mikakati yake.

Bi Muna alisema: "Mkutano huu utawajengea uwezo viongozi wa dini, watendaji wa Somalia na kuongeza ufahamu wao juu ya umuhimu wa kuwajumuisha wanawake katika njia yao za kupambana na siasa kali na kubadilishana uzoefu na mbinu bora na wataalamu, watafiti, watendaji kutoka barani ambao wana ufanisi mkubwa katika kukabiliana na masuala yahusuyo vikundi vyenye misimamo mikali."

Aidha naye, Naibu Kamishna wa Polisi wa AMISOM, Christine Alalo alisema kuwa katika hatua hii muhimu ya safari ya Somalia kuelekea kwenye amani na utulivu, jukumu la wanawake, wanaume na vijana katika kukabiliana na vikundi vyenye msimamo mkali ni muhimu kutiliwa mkazo kwa kiasi kikubwa.

"Siyo siri kwamba wakati wa miongo miwili na nusu ya vita, wanawake na vijana wadogo wamekuwa wakitumika na makundi ya kigaidi katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kukusanya taarifa za kiusalama, na kubeba mabomu,” alisema.

Alibainisha kuwa AMISOM wamefanya mengi katika kupambana na hilo kupitia kitengo cha jinsia, wanawake na ulinzi wa mtoto.

Alisema kuwa AMISOM pia imesaidia wizara ya wanawake, jinsia na haki za binadamu katika kuandaa sera ya taifa ya jinsia, kwa kufanya mafunzo ya ujengaji uwezo kwa wanawake wa Somalia na viongozi wa dini katika kumaliza mambo hatarishi.

Mkutano huo wa siku tatu ambao unamalizika leo jijini Dar es Salaam, umewaleta pamoja watendaji, viongozi wa dini na asasi za kijamii kutoka nchi nane (Somalia, Tanzania, Ethiopia, Nigeria, Kenya, Mali, Djibouti, Alger) ukijadili juu ya mada zinazohusiana na kukabiliana na siasa kali na ugaidi.

Jumla ya viongozi hamsini, wa kidini; watafiti na watendaji, na wadau muhimu kutoka taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa wameshiriki katika mkutano huo.

RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI AMPOKEA WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA ALIYEWASILI MCHANA HUU JIJINI DAR

No comments:
 Rais Dkt John Pombe Magufuli akimpokea mgeni wake ,Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn aliyewasili hivi punde katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam.
 Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn akipewa maua ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kwa upendo nchini Tanzania,mara baada kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mapema leo mchana,na baadae kupokelewa na mwenyeji wake Rais Dkt John Pombe Magufuli,Waziri Mkuu Kassim Majliwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa.
Waziri Mkuu wa Ethiopia ,Hailemariam Dessalegn akishuka kwenye ndege mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere mapema leo mchana,na baadae kupokelewa na mwenyeji wake Rais Dkt John Pombe Magufuli,Waziri Mkuu Kassim Majliwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa.

Imeelezwa kuwa ujio wa Waziri huyo Mkuu wa Ethiopia ni pamoja na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

 Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo na kushuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Umakini Unahitajika Matumizi Ya Mitandao Ya kijamii

No comments:


facebook-whatsapp-370x264
Benjamin Sawe,Dar es Salaam.
Maelezo.
Zaidi ya asilimia 60 ya watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17 wanatumia zaidi ya masaa mawili kila siku kuangalia mitandao ya kijamii pamoja na vipindi mbalimbali vya Televisheni.
Hii inaweza kuwa njia kubwa ya kuunganisha, lakini pia kuna hatari zinazohusiana na kutumia muda mwingi sana kwenye vyombo vya habari kijamii.
Leo hii ni nadra kukuta familia ambazo watoto na vijana wake hawajaathirika na vyombo vya habari na elektroniki kama vile televisheni, intaneti na michezo mingine tofauti ya kompyuta.
Hata hivyo utumiaji mkubwa na wa masaa mengi wa vyombo hivyo hauwahusu watoto na vijana tu, bali watu wazima pia wameathirika na jambo hilo.
 Kutokana na sababu kadhaa za kimwili, kisaikolojia na kiroho, kuna udharura kwa watoto kusimamiwa vyema na wazazi, mashirika na taasisi za kielimu na kiutamaduni na kadhalika vyombo vya habari ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi mabaya ya vyombo hivyo vya elektroniki.
Licha ya kompyuta kuwa na pande chanya tofauti za kimaendeleo, hasa katika nyanja za kielimu na huduma za mawasiliano, lakini chombo hicho pia kina nafasi hasi kwa watoto na hata kwa watu wazima.
Utumiwaji usio na udhibiti wa chombo hicho na kadhalika vyombo vingine vya elektroniki kama vile televisheni, unaweza kuyaweka hatarini maisha ya watoto kutokana na athari zake mbaya kwa ustawi wa kiroho, kisaikolojia na kijamii wa watoto hao.
Harakati zetu za kifizikia na miamala yetu tofauti ya kijamii, ni umuhimu yenye taathira kubwa kwa afya na tabia za mtoto. Kinyume chake, ikiwa mtoto atatumia muda wake mwingi katika matumizi ya michezo ya kompyuta, basi hawezi kunufaika na upande chanya wa kujenga akili yake wala harakati bora kwa ajili ya kuufikia ukamilifu wake kijamii.
Mbali na hayo, watoto pia wanaweza kukabiliwa na hatari ya kutekeleza vitendo vya ukatili na visivyo vya kikatili hata katika umri wao mdogo. Hali hiyo ambayo inaweza kufikiwa ghafla au hata kwa makusudi, huwaletea watoto na vijana madhara yasiyoweza kufidika hasa kuhusiana na masuala ya kiafya, kisaikolojia sambamba na kueneza kwa kiasi kikubwa matatizo ya kimwili na kiakili kama vile utovu wa maadili, vitendo vya ukatili, madawa ya kulevya, tabia mbaya katika jamii, kuzorota thamani za familia na kuenea jinai na uhalifu wa kila aina katika jamii.
Ukweli ni kwamba, wazazi hawajawachwa peke yao katika jukumu la kutoa malezi bora kwa watoto wao, bali wataalamu wa mambo wamefanya utafiti wa kina katika uwanja huo na kuwasaidia katika suala hilo kwa kuwasilisha njia bora za malezi ambazo zinawavutia watoto na kuwafanya waishi maisha bora katika jamii.
Watafiti hao wanasema kuwa, licha ya kwamba haiwezekani kuwatenga watoto na ulimwengu wa michezo ya kompyuta lakini tunaweza kuwaepusha na madhara ya michezo hiyo kwa kutumia njia na mbinu zinazofaa.
Udhibiti fulani wa matumizi ya kompyuta kila siku au kwa wiki, ni moja ya njia hizo. Kwa mbinu hiyo, mtoto anaweza kutumia chombo hicho kwa muda na kiwango kilichoainishwa na kila pale anapokwenda kinyume na kiwango hicho, basi anapasa kuzuiwa na kuadhibiwa.
Hata hivyo utumiaji mabavu na nguvu hauna nafasi katika hapa. Katika kesi kama hiyo njia ya mazungumzo sanjari na kumzuia kwa muda, kutumia vitu anavyovipenda mtoto huyo, inafaa kutumiwa hapa.
Wakati mwingine mtoto hutumia vyema kompyuta kwa kujinufaisha kielimu na chombo hicho muhimu cha teknolojia na kwa kweli katika hali kama hii wazazi hawapaswi kumzuia mtoto kutumia chombo hicho cha kompyuta. Lakini jambo linalopaswa kuzuiwa ni tabia ya mtoto huyo kutumia wakati wake mwingi katika kichezo isiyofaa ya kompyuta.
Moja ya nyenzo zingine za udhibiti ambazo zinaweza kutumiwa na wazazi katika kusimamia mienendo ya mtoto, ni uwezekano wa kutumia mbinu zinazodhibiti mfumo wa kompyuta. Kwa utaratibu huo watoto hawawezi kuingiza program mpya au kuweka windozi tofauti ambazo ni rahisi kuweza kuwaharibu watoto.
Njia nyingine ni pamoja na kuzuia kuondolewa program zilizopo katika kompyuta au kuzizuia zisifanye kazi, ni moja ya njia ambazo zinaweza kutumiwa katika kuwadhibiti watoto.
Miongoni mwa njia nyepesi zaidi kwa wazazi katika kumlinda mtoto wao wakati wa kutumia njia na nyenzo zinazohusiana na ulimwengu wa intaneti, ni kuweka mfumo wa kompyuta nje ya chumba chake cha kulala. Njia hiyo itawasaidia wazazi wakati wa kutumia mtoto chombo hicho nao waweze kushuhudia na kufuatilia kwa karibu michezo na shughuliza zote za mtoto huyo anapotumia kompyuta.
Kwa hakika vivutio vya kompyuta na michezo mingine ya kielektroniki kwa watoto havina kikomo, na ikiwa hakutakuwepo usimamizi madhubuti wa wazazi kwa mtoto wao, basi huenda mtoto bila kujijua, akatumia wakati mwingi zaidi kuliko inavyotakiwa na hivyo kuathiri lishe, usingizi na hata masomo yake.
 Hapo ndipo wazazi wanapotakiwa kuwa macho na kuhakikisha wanasimamia vyema malezi ya mtoto wao sanjari na kumuandalia ratiba nzuri ya maisha yake na kuchunga sheria watakazomuainishia kila wiki.
Aidha wazazi wanatakiwa kumuweka mbali mtoto wao na ulimwengu wa elektroniki na michezo ya kompyuta wakati wa kipindi cha masomo. Watafiti wanasema kuwa,  kuna ulazima mkubwa wa kuzingatiwa wakati wa matumizi ya watoto kwa vyombo vya umeme kama vile kompyuta, labtop na tablet na kile ambacho kinahusiana na ulimwengu wa kielektroniki, kwani utafiti unaonyesha kwamba matumizi mengi ya vyombo hivyo kupita kiasi na kufikia kiwango cha uraibu, hupunguza uwezo wa kifikra wa mtoto.
 Na kukithiri kwa  maradhi hayo kwa watoto ndio mwanzo wa kufeli katika hatua zao za kielimu sanjari na kushindwa kukabiliana na mikikimikiki mingine ya kimaisha ambayo anapaswa kukabiliana nayo katika mustakbali wa maisha yake ya mbeleni.
 Katika matumizi ya michezo ya kompyuta au ulimwengu wa intaneti, kuna udharura wa kujitenga na mambo machafu yasiyofaa. Aidha inaelezwa kuwa, kutumia sana kompyuta na intaneti, taratibu huibua tatizo la unene, ambalo mara nyingi hupelekea watoto na hasa vijana wengi kujichukia wenyewe kutokana na tatizo hilo. Hivyo kuna haja kwa wazazi kuwaepusha watoto wao na unene na uzembe unaosababishwa na matumizi ya muda mrefu ya vyombo vya umeme hasa michezo ya kompyuta.
Wataalamu wengi wanaamini kuwa, ni muhimu kuwatenga watoto walio na umri wa chini ya miaka mitatu na aina yoyote ya matumizi ya kompyuta. Kwa maana nyingine ni kwamba, umri huo hauoani na matumizi ya kompyuta au video.
 Hata hivyo ikiwa mtoto aliye na umri wa chini ya miaka mitano ataingia katika ulimwengu wa matumizi ya vyombo hivyo na kuvizoea, basi lazima awekewe sheria na vidhibiti maalumu vya kumuwezesha kukabiliana na hatari ya ulimwengu huo. Kwanza anapasa kufahamishwa ni kwa kipindi gani anatakiwa atumie vyombo hivyo na kisha baada ya hapo ajishughulishe na kazi nyingine.
Watafiti wanapendekeza kuwa, mtoto mwenye umri wa kuinukia anatakiwa atazame kwa saa moja au masaa mawili filamu na katuni, upekuzi katika intaneti na michezo mingine ya video katika kompyuta. Ikiwa mtoto kwa siku atatumia dakika 45 kucheza mchezo wa kompyuta na muda mwingine mdogo kutazama televisheni na mwingine mfupi kujishughulisha na harakati za kifizikia, basi hakutakuwepo na wasi wasi wa kuathirika afya yake. Lakini ikiwa atatumia masaa mengi kujishughulisha na michezo ya kompyuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa, basi hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo.
Madaktari wanashauri kwamba, watoto wanatakiwa kutumia masaa mawili tu kwa siku kutazama televisheni. Televisheni ina athari nyingi muhimu kwa watoto wengi wanaosoma na hasa katika kupumzisha mwili na fikra zao.
Hivyo wazazi na walimu wanatakiwa kusimamia ni kiasi gani watoto wanapaswa kutazama televisheni. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya awali watoto wanaosoma shule za msingi, huwa hawana uwezo wa kupanga vyema ratiba za kutazama televisheni.

WANACCM TISA WANADAIWA KUFA MJAWA KUTOKANA NA MATUKIO YANAYOENDELEA YA MAUAJI

No comments:


Chama-Cha-Mapinduzi
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
VIONGOZI na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tisa kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti, wanadaiwa kuawa kwa kupigwa risasi na wengine kuchomwa moto kutokana na matukio ya mauaji ya mfululizo yanayoendelea wilayani hapo .
Aidha CCM mkoa na Taifa imeombwa kutupia macho suala hilo kwa upana na kulisimamia ili kubaini chanzo halisi kinachosababisha wauawe.
Kutokana na hali hiyo wanachama wa maeneo ya wilaya hiyo, wanashindwa kuvaa sare za chama na kuogopa kuitana majina ya vyeo vyao.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Mjawa ,Abubakar Seif, alisema baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wanashindwa kwenda ofisini kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza katika mkutano wa ndani katika kata hiyo,ulioitishwa na chama hicho mkoa alisema wanaishi kwa sintofahamu na imani inawatoweka.
Abubakar alisema watu wanakiogopa chama kwasasa na kukimbia miji na ofisi zao.
Anaeleza miaka ya nyuma watu walikuwa wakigombea nafasi mbalimbali za uongozi lakini kwa sasa wanakwepa na kuhofia uhai wao.
Abubakar alikiomba chama kiendelee kwa nguvu zake kutoa hamasa kwa wanachama wa Rufiji na Kibiti kurejesha amani kwa vijana.
“Ni mashaka makubwa kwanini wauwe viongozi wa CCM pekee, sawa kila mtu na umauti wake lakini si kihivii “
“Tatizo hapa ni masuala ya kisiasa ambapo ukanda huu unatawaliwa na mvutano wa kisiasa toka huko nyuma “alisisitiza.
Katibu wa CCM Kibiti, Zena Mgaya, alisema ulinzi ni wa kila mmoja ili kusaidiana na jeshi la polisi.
Aliomba waendelee kukipenda chama na kukisimamia kwani vitendo hivyo vinadhibitiwa kwasasa.
Zena alieleza haiwezekani chama kikakaa bila viongozi wa chini, amewapa moyo wasikate tamaa hali itakayosababisha kuendelea kushika dola.
Alisema Polisi wametanda kila kona kwa sasa hivyo amani itarejea.
Zena alisema homa na mtikisiko uliopo kwenye wilaya ya Kibiti na Rufiji inaumiza jamii hasa wanaccm na viongozi wake ambao hawaishi kwa raha saa 12 jioni inabidi waingie ndani kujifungia.
Aliyekuwa katibu wa CCM mkoani Pwani anaesubiri makabidhiano, Hassan Mtenga, alitoa pole na kusema amepokea changamoto hiyo na ataikabidhi kwa katibu aliyeteuliwa sasa Anastasia Amas.
Ni matukio takriban 11 ya mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama, wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambayo yanadaiwa kujitokeza wilayani Rufiji na Kibiti.
Katika matukio hayo ni pamoja la March 28 ambapo mwenyekiti wa (CCM) tawi la  Mparange na mjumbe wa serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini ,wilayani Rufiji mkoani Pwani, Michael Lukanda,aliuawa kwa kupigwa risasi ya kichwani na watu wasiojulikana.
Jingine ni march 12,mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo Hemed Njiwa aliuawa kwa kupigwa risasi.
Jan 19,mjumbe wa serikali ya kijiji cha Nyambunda ,Oswald Mrope, aliuawa kwa kupigwa risasi.
March 1,mwenyekiti wa kijiji cha Nyambunda Said Mbwana aliuawa.
Feb 24,watu watatu akiwemo afisa upelelezi wa polisi wilaya ya Kibiti Peter Kubezya aliuawa kwa risasi.
Octoba 24,2016 afisa mtendaji wa kijiji cha Nyambunda Ally Milandu alipigwa risasi na kufa na novemba 6,2016 ,mwenyekiti wa kitongoji cha Nyang’unda kijiji cha Nyambunda Mohammed Thabiti alipigwa risasi akielekea kwake.
Jeshi la polisi Pwani na serikali mkoani hapa, linaendelea kupambana kufuatia matukio hayo na kuimarisha ulinzi ikiwemo kusitisha usafiri wa bodaboda ifikapo saa 12 jioni.

WASANII MSIVUKE MIPAKA KATIKA UTENGENEZAJI WA KAZI ZENU KWA KUVUNJA SHERIA ZA NCHI: DKT MWAKYEMBE

No comments:


F
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akisalimiana na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego kwa mwaliko Ofisini kwake Mjini Dodoma kufanya mazungumzo yahusuyo mambo ya Sanaa ya Muziki.
F 1
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe Mjini Dodoma kwa mazungumzo.
F 2
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akisisitiza jambo kwa Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego mara baada ya mazungumzo Ofisini kwake Mjini Dodoma.
F 3
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) mara baada ya kumaliza mazungumzo na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego Ofisini kwake Mjini Dodoma.
F 5
Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) mara baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe Mjini Dodoma.
Picha zote na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma.
………………..
Na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa wasanii nchini kutovuka mipaka katika utengenezaji wa kazi zao mpaka kufikia hatua ya kuvunja Sheria na taratibu za nchi.
Ameyasema hayo Mjini Dodoma jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana  na kufanya mazungumzo na Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego kwa mwaliko wa Waziri huyo.
Amesema kuwa  wasanii ni nguzo muhimu katika nchi sio kwa kufanya kazi ya  kuburudisha na kuelimisha bali katika kuujenga Utamaduni wa nchi ambao ndio nguzo muhimu sana kwa malezi na makuzi ya wanajamii.
“Niwaombe wasanii nchini kuzingatia Sheria na taratibu za nchi katika utunzi wao na utenegenezaji wao wa kazi zao” Alisisitiza Mhe. Dkt Mwakyembe.
Aidha ameongeza kuwa Serikali haina nia ya kuwanyima uhuru wa kujieleza bali watambue kuwa nchi inaendeshwa kwa taratibu na Sheria ambazo zinatakiwa zifuatwe na watu wote.
Kwa upande wake Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  kwa kuwaunga mkono wasanii nchini na kuahidi kuongeza baadhi ya mambo katika wimbo wake wa “Wapo” na kuwaalika watanzania kama kuna kero zingine zinazowasumbua katika jamii wasiwasilishe kwake ili azizungumzie katika wimbo huo.
“Namshukuru Mhe. Rais kwa kutuunga mkono pia naahidi kufanya “remix” ya wimbo wa “Wapo” kwa kuongeza maneno niliyoshauriwa na Mhe Rais na Mhe. Waziri na kama kuna mengine kutoka kwa wananchi pia niko tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi” alisema Bw. Elibariki.
Hivi karibuni wimbo wa “Wapo” wa Msanii Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego ulifungiwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kosa la kutozingatia maadili na baadae kufunguliwa kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  kupitia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe.

TAARIFA KUTOKA UMOJA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM)

No comments:


boss7
Ndugu waandishi wa habari,
 
Tunawashukuru kwa kupokea wito wetu na  kuja, karibuni sana tunawaahidi kwamba
 tutaendelea kushirikiana nanyi katika kila hatua.
 
Aidha Umoja wa Vijana wa CCM unavipongeza sana vyombo vyote vya habari nchini kwa juhudi zenu za kuhabarisha, kuelimisha, kuwaasa, kuwaelekeza na kuihabarisha jamiii katika masuala kadhaa yanayohusiana na mipango ya maendeleo,   mikakati, sera na malengo ya Serikali  na mipango ya vyama vya siasa.
 
Ndugu Waandishi wa habari.
 
Tumewaita leo kuzungumzia mambo 2 makubwa, na suala zima la mtikisiko wa demokrasia katika  mchakato wa uteuzi wa wagombea Ubunge katika Bunge la Jumuiya ya  Afrika Mashariki  (EAC) ulivyoendeshwa ndani ya vyama vya upinzani  nchini.
 
Bunge la Afrika Mashariki kama mjuavyo ni chombo kikubwa na chenye heshima ya pekee katika kanda yetu. Kuwepo kwake kunaashiria muendelezo wa kufufua dhana, dhamira, mikakati, fikra na malengo ambayo yaliasisiwa na waasisi wa Mataifa yote yaliyomo  katika Kanda yetu ili hatimaye siku moja ishuhudiwe Kanda hii na Bara zima la Afrika likiunda dola moja.
 
Ni jambo la heri na faraja kuona EAC  ya  sasa ikiwa ni yenye kufikia malengo ya  utengamano na mafanikio hususan katika nyanja za kiuchumi na kiusalama kama vile  kuwa na  Pasi moja ya kusafria, miingiliano ya wananchi wake katika ufanyaji wa biashara pia mkakati kuelekea kupata
 viwango sawia vya ushuru wa Forodha.
 
Masuala mengine ni kuona  maeneo ya mipaka yetu kukiendelea kuwa na ustawi wa hali ya utulivu na usalama, wakati huo EAC ikifanya kila linalowezekana kumaliza migogoro yake ya kisiasa ambapo mazungumzo ya upatanishi huko Burundi yamekuwa yakiendelea  chini ya mpatanishi mkuu  Rais mstaafu Benjamin Mkapa sambamba na wananchi wa pande zote za nchi wanachama tukishuhudia  wakiishi kwa maelewano, umoja, udugu na mafahamiano.
 
Ni katika jumla ya mambo yanayofurahisha na pengine yakiwasuta na kuwaaibisha maadui na vibaraka ambao aghalab  hutumiwa kwa malipo yenye ujira wa dhambi  toka kwa mabeberu katika kuhakikisha  mipango batili ya kutaka kudhoofisha, kuigawa na kukwamisha juhudi za EAC isiimarike..
 
Aidha kuibuliwa na kupokewa kwa mpango uitwao ” One Stop Boarder” yaani (OSB)
 sasa umefanikiwa huko mipakani baina ya nchi wanachama.  Pia
kuanzishwa  miradi mikubwa ya kiuchumi mfano bomba la mafuta toka Kampala (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) ujenzi wa reli toka kigali hadi Uganda huku EAC ikielekea kuwa na sarafu moja kabla ya kufikiwa azimio la  uundwaji wa Shirikisho moja.
 
Umoja wa Vijana wa CCM tumelazimika kuyataja na kuyaainisha maeneo hayo yaliopata mafanikio kwa uchache  lengo likiwa ni kuonyesha  uwepo na ustawi wa EAC pamoja na umuhimu wa bunge lake kama ni jambo nyeti na wala si suala dogo au la mchezo mchezo kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeonyesha udhaifu.
 
Ndugu Waandishi wa Habari,
 
Baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeshindwa hata  kuteua wagombea ubunge wengi ili kuwania nafasi katika bunge hilo  la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu zinazotokana  aidha na ubinafsi, umimi na udikteta.
 
Tunachukua fursa hii kwanza kukipongeza Chama Cha Mapinduzi na wanachama wake wote 450 ambao kwa ujasiri, uwezo na kujiamini kwao wamethubutu kujitokeza na kuchukua fomu za  kuwania nafasi za ubunge wa EAC.
 
Kitendo cha wanachama hao wa CCM kujitokeza kwa wingi kimsingi
 kimeidhihirishia dunia kwamba chama chetu bado ni cha kidemokrasia
kinachoungwa mkono na kuaminiwa na wananchi wengi wakiwemo  Vijana, wanawake na wana taaluma mbali mbali wakitambua ndicho chama pekee imara chenye kujali, kuthamini na kufuata misingi ya usawa na demokrasia ya kweli.
 
Wanachama 450 wa CCM walichukua fomu kwa kufuata taratibu baada ya mchujo wa kidemokrasia kufanyika ndani ya CCM,  wanachama   12 wamebahatika kuteuliwa na vikao vya kikatiba  ambapo sasa wagombea hao watasimama mbele ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaka ridhaa  kwa kujieleza na kuomba kura.
 
Ndugu Waandishi wa habari,
 
Umoja wa Vijana CCM  kwa  tunasikitishwa sana na mwenendo wa demokrasia ndani ya vyama vya upinzani  katika uteuzi wa kuwapata wagombea wa ubunge  wa bunge la Afrika Mashariki (EALA)   Chadema, CUF  na NCCR Mageuzi kwa jinsi walivyowasilisha  uwakilishi haba na finyu lakini pia kujitokeza kwa wagombea wachache hali inayoonyesha uminyaji wa demokrasia ndani ya vyama vyao.
 
Chadema na washirika wao mara kadhaa hujigamba vichochoroni na kujionyesha kuwa wao ni  watetezi  wa demokrasia lakini unapofikia wakati wa utekelezaji wa jambo hilo  kwa vitendo, ndani ya chama hicho humea ukandamizaji wa haki na kujitokeza  upendeleo, ukanda, kubebana  aidha kwa asili, ujamaa na urafiki au kulipana fadhila.
 
Katu huu si mwenendo mwema ulioonyeshwa na vyama vya upinzani. Vimejipaka matope ya fedheha kwa kushindwa  kuonyesha kama ni waumini wa kweli wa demokrasia badala yake havikujali wala kuheshimu dhana ya demokrasia na kujikuta  vimejianika na kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa  vyama hivyo ni vya watu maalum vya kibwanyenye na vya kiimla .
 
Kufanya uteuzi wa wanachama wanaogombea nafasi za kidemokrasia kwa kumtazama asili yake, anatoka  kanda ipi, kabila, imani yake au nasaba licha ya
 kwenda kinyume na misingi ya Taifa letu lakini pia ni kinyume na
matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
UVCCM kwa kauli moja tunawaamsha na kuwatumia ujumbe watanzania wenzetu hususan Vijana mahali popote walipo wavikatae na kuvikwepa vyama vya aina hiyo, wasikubali kugawanywa kwa asili zao, imani au rangi na nasaba.
 
Taifa letu ni alama pana ya kuenzi na kudumisha demokrasia si tu barani Afrika lakini vile vile duniani kote, hivyo kwa umoja wetu, kwa nguvu zetu, akili na maarifa tulionayo, abadan tusijaribu kuichezea amani yetu, umoja na mshikamano wetu  uliojengwa na waasisi wa Taifa letu na kukubali
 kuvishabikia vyama na viongozi wasaka madaraka kwa hila ambao ni
 wafujaji na wakandamizaji wa misingi ya demokrasia ndani ya vyama kama
ilivyojionyesha  kwa vyama vya upinzani vya Tanzania katika uteuzi wa wabunge EAC.
 
Mchakato wa Uchaguzi ndani ya UVCCM.
 
Uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2017, unafanyika wakati ambapo CCM inatimiza miaka 40 tokea kuasisiwa kwake tarehe 5 Februari, 1977 na ni wakati ambapo nchi yetu inatimiza miaka 25 ya Mfumo wa Vyama Vingi ulioridhiwa na Mkutano Mkuu wa CCM kutokana na busara za Viongozi wake.
 
Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Chama na Jumuiya zake inaonesha mchakato wa Uchaguzi wa Jumuiya za CCM kuwa unaanza kabla ya ule wa CCM. Utaratibu huu unalenga kuwawezesha wanachama wa Jumuiya za CCM ambao watakuwa ni wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika CCM, au wale waliochaguliwa kuwakilisha Jumuiya zao katika Vikao vya CCM ili waweze kuhudhuria mikutano ya Chama inayowahusu.
 
Umoja wa Vijana wa CCM umekamilisha maandalizi yote ya msingi ya awali kwa ajili ya Uchaguzi unaotarajia kuanza tarehe 1 April, 2017 ikiwemo kusambaza vifaa katika Mikoa na Wilaya zote nchini wa ajili ya kufanikisha uchaguzi kwa wakati.
 
Aidha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi imekamilisha mapitio na uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Wilaya katika Jumuiya ambao watakuwa ndio wakurugenzi wa Uchaguzi katika maeneo yao.
 
Tunaendelea kuwakumbusha Watendaji wetu muda wote kusimamia haki, ukweli na usawa lazima vijana wa CCM muda wote tuishi katika maneno na maagizo ya Mwenyekiti wetu wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli.
 
Hatutamvumilia mtendaji yeyote atakayekiuka Kanuni, Taratibu na miongozo kwa makusudi ili kufurahisha kikundi au watu fulani. Uchaguzi huu 2017 UVCCM tunataka kuidhihirishia dunia na Vyama vya Upinzani kuwa CCM ni Chuo Cha Demokrasia ulimwenguni.
 
Mwisho niendelee kuwahamasisha vyema wote nchini yenye sifa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali za uongozi ndani ya CCM na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Shina, Tawi, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa.
 
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
 
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
 
KAIMU KATIBU MKUU
 Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Shaka Hamdu Shaka akizungumza na Wana Habari Makao Makuu UVCCM Upanga (PICHA NA FAHADI SIRAJI)
 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger