TRA

TRA

Friday, March 31, 2017

Mgororo wa Palestina na Israel, Trump ana ubavu?

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Julian Msacky

KAMA kuna mgororo unaisumbua dunia kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi ni wa Israel na Palestina.

Umoja wa Mataifa (UN) umesalimu amri. Mataifa ya Magharibi yanaugusagusa na kuacha ulivyo. 

Ni sawa na mfupa uliomshinda fisi. Swali sasa ni je, nani atamaliza mzozo huo? Ni viongozi wa kiserikali au dini?  

       RAIS DONALD TRUMP

Je, UN na mataifa mengine yataendelea kuangalia namna Wapalestina na Waisrael wanavyonyukana kila mara?

Historia inaonesha kuwa mgogoro huo umejikita katika masuala ya kidini hivyo ufumbuzi wake ni utata mtupu.

Tunaambiwa kuwa wakati Waisrael wakiwa utumwani Misri kuna nchi ilikuwa na asali na maziwa.

Nchi hiyo (Palestina?) ilikuwa na kila kitu, inapendeza, yenye rutuba na hakika ilikuwa ni kama paradiso.

Walipokuwa nchini Misri wana wa Israel walilalamika kuteswa hivyo wakamlilia Mungu ili awaokoe.

Mwenyezi Mungu akafanya hivyo kwa kumtumia Nabii Musa na kwa mkono wa Mungu aliwaondoa Misri.

Baada ya kufanya hivyo aliwaongoza Waisrael kwenda nchi ya ahadi.

Wakiwa tena njiani walipata mateso makali jangwani na shida zilipozidi walitamani Musa awarudishe Misri.

Mateso yalipokolea Waisrael waliamua kujitengenezea miungu ya shaba na kumweka pembeni Mungu wao.

Mwenyezi Mungu alichukizwa na tabia hiyo na kuvunja agano na wana wa Israel licha ya kuwa ni taifa teule.

Kadri siku zilivyosogea umri wa Musa nao ulisogea na alipofikisha miaka 120 alifariki dunia. Hakuona nchi ya ahadi.

Kwa sababu hiyo Waisrael walibaki wakirandaranda jangwani hadi nabii Joshua alipochukua nafasi ya Musa. 

Hii ilikuwa ni safari ndefu yenye majaribu mengi ili kupima imani ya Waisrael kwa Mwenyezi Mungu.


Kutokana na hali hiyo mgogoro wa Israel na Palestina unahitaji mkono wa Mungu kutuliza mzimu wa mababu. 
 
Hakuna mwenye jibu la moja kwa moja kama yupo kiongozi wa kisiasa au dini anayeweza kuleta amani maeneo hayo.

Amani ya kweli itapatikana endapo haki isipotamalaki na mkubwa kumheshimu mdogo ili kuondokana na mapambano ya Goliathi na Daudi

Bila kufanya hivyo Wapalestina wataendelea kujihami kwa kila mbinu ili kuzuia uvamizi katika ardhi yao. 

Kama zilivyo nchi nyingine Palestina inahitaji kutambuliwa na kupewa hadhi badala ya kunyanyapaliwa.

Kauli ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba:  

“Katika makubaliano yoyote ya amani, Israel lazima iwe na uwezo wa kudhibiti usalama katika eneo lote la Magharibi mwa mto Jordan”.

Eneo hilo linahusisha ukingo wa Magharibi na ni kitovu cha taifa la Palestina linalotarajiwa kuundwa kulingana na makubaliano ya kimataifa.

Ikumbukwe kwamba kilio kikubwa cha Palestina ni kuonewa pamoja na kuporwa haki zao asilia (ardhi) hivyo kubaki kama watoto yatima.

Pengine ni kwa kutambua ugumu wa mgogoro huo ndiyo maana Rais wa Marekani, Donald Trump alisema:

“Uongozi wangu unaunga mkono uundwaji wa taifa moja ili kumaliza mzozo wa Israel na Palestina,”.

Anachosema Trump nacho ni tatizo kwa sababu ni nani kati ya Palestina na Israel atakubaliana na hilo?

Ukimsikiliza Netanyahu ni kana kwamba anataka Israel imiliki eneo lote linalokaliwa na Palestina.

Tusisahau kuwa hivi sasa Israel inafikiria kuanzisha makazi mapya 6000 ingawa haifamiki yatatoka eneo la Palestina au la. 

Huu ni mgogoro mwingine kama nilivyogusia katika mada iliyopita. Hii inaonesha hali bado si shwari. 

Kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu wa Israel alimwambia Trump lazima Wapalestina waitambue Israel kama taifa la Kiyahudi na kutambua haki ya Israel kusimamia usalama katika eneo zima.

Hata hivyo, Trump alionekana kutomuunga mkono Netanyahu kuhusu suala hilo hususan eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa lugha nyingine Trump amevunja utamaduni wa viongozi wa Marekani kuikumbatia Israel. Hii inaashiria nini? 

Tuseme kwamba ile dhana kuwa ukimuona Mwisrael umemuona Mmarekani na ukimuona Mmarekani umemuona Mwisrael inafutika?

Pengine tukubaliane tu na ushauri wa Rais Trump kuwa pande zote mbili zinahitaji kuwa na maridhiano. 

Ni kwa njia hiyo pekee amani ya kweli itapatikana kati ya Wapalestina na Waisrael na si vinginevyo.

Lakini viongozi wakitanguliza jazba na ubabe kama anavyotaka Netanyahu badala ya amani ni vita.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger