BENKI
ya NMB imesaini makubaliano na Kampuni ya Mastercard kufanya kazi
kiushirikiano ili kuhakikisha inaiinua sekta ya kilimo nchini Tanzania
kwa kuanzishwa kilimo mtandao 'eKilimo' kinaomuwezesha mkulima kupata
taarifa za masoko na bidhaa kuondoa urasimu waliokuwa wakiupata wakulima
hapo awali. Huduma hiyo ya 'eKilimo’, ni jukwaa la kidigitali ambalo
litamsaidia mkulima kupata uwazi na usalama wa bidhaa zake kimasoko na
hata urahisi wa upatikanaji taarifa, huku ukiondoa urasimu uliokuwa
ukifanywa na madalali sokoni, jambo ambalo wakulima wengi wamejikuta
wakishindwa kunufaika kiufasaa kwa bidhaa zao.
Ushirikiano
huo umesainiwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker pamoja na Rais wa Kampuni ya
MasterCard barani Afrika, Bw. Raghu Malhotra, ambapo kwa pamoja
wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema huduma hiyo itawainua wakulima
kwa kiasi kikubwa endapo itatumiwa na wakulima. Kwa upande wake, Rais
wa Kampuni ya MasterCard barani Afrika, Bw. Malhotra, alisema kupitia
huduma hiyo mkulima anaweza kufanya mauzo na kulipwa kwa kutumia simu
iliyo na programu maalum huku benki ikipata taarifa, jambo ambalo
litamrahisishia shughuli zake na kuokoa muda mwingi wa kuzunguka.
Alisema
takwimu zinaonesha kilimo kinachangia kiasi kikubwa cha fedha katika
pato la taifa 'GDP', ambapo takribani shilingi bilioni 13.9 ikiwa ni
takribani asilimia 30, hivyo kuna kila sababu ya kuinua sekta hiyo ili
iendelee kufanya vizuri na pia kuwainua wakulima. "Kwa kutumia
teknolojia ya kidigitali huduma hii italeta uwazi kwenye mchakato wa
mauzo na ununuzi na kuongeza ufanisi katika eneo la ugavi, hivyo kuleta
manufaa ya kiuchumi.
Teknolojia
inapaswa kusaidia wakulima kupata ufumbuzi kwa huduma za kifedha, hivyo
kuwawezesha kuwa na maisha bora na familia zao hata baadae," alisema
Rais wa Kampuni ya MasterCard barani Afrika, Bw. Malhotra. Akizungumzia
huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker
alisema lengo kubwa ni kumuwezesha mkulima kunufaika zaidi na kilimo
anachokifanya, huku benki ikiendelea kujenga mazingira ya mteja kupata
huduma bora na kuaminika ili aendelee kupata mikopo kwa shughuli za
kilimo.
Alisema
mkulima anapokuwa na uhakika wa kupata taarifa sahihi za masoko na
kuweza kufanya mchakato mzima pasipo na urasimu hunufaika zaidi na
kuendelea kuaminika kwa taarifa zake benki jamboa ambalo ananufaika moja
kwa moja kupata mikopo ya kilimo, ambayo humuongezea tija. "Nia yetu
sisi ni kukua sekta ya kilimo Tanzania, na ndio maana tumeshirikiana na
Mastercard na kuja na teknolojia ambayo inaweza kubadilisha maisha ya
wakulima.
Uzoefu
wetu katika sekta ya kifedha unatufanya kutafuta wadau kama Mastercard
ambapo tumeona wamefanya vizuri nchini Kenya kuwasaidia wakulima kupitia
programu ya '2KUZE'. Ndio maana nasi tumeungana kuhakikisha wakulima
wadogo, wanunuzi na mawakala wananufaika kiuchumi," alisema Mkurugenzi
Mtendaji, Bi. Bussemaker.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (wa pili
kushoto) pamoja na Rais wa MasterCard Ukanda wa Mashariki ya Kati na
Afrika, Bw. Raghu Malhotra wakisaini makubaliano ya kiushirikiano jijini
Dar es Salaam kuhakikisha sekta ya kilimo nchini Tanzania inakuwa na
kilimo mtandao 'eKilimo' kinaomuwezesha mkulima kupata taarifa za masoko
na bidhaa kuondoa urasimu aliokuwa akiupata mkulima hapo awali. Wa
kwanza kushoto akishuhudia ni Kaimu Ofisa Mkuu Kitengo cha Wateja
wadogo, Abdulmajid Nsekela na Rais wa MasterCard wa nchi za Kusini mwa
Jangwa la Sahara, Daniel Monehin.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (wa pili
kushoto) wakibadilishana nyaraka za makubaliano na Rais wa MasterCard
Ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika, Bw. Raghu Malhotra (wa pili
kulia) mara baada ya kusaini makubaliano ya kiushirikiano jijini Dar es
Salaam kuhakikisha sekta ya kilimo nchini Tanzania inakuwa na kilimo
mtandao 'eKilimo' kinaomuwezesha mkulima kupata taarifa za masoko na
bidhaa kuondoa urasimu aliokuwa akiupata mkulima hapo awali. Wa kwanza
kushoto akishuhudia ni Kaimu Ofisa Mkuu Kitengo cha Wateja wadogo,
Abdulmajid Nsekela na Rais wa MasterCard wa nchi za Kusini mwa Jangwa la
Sahara, Daniel Monehin.
SHARE
No comments:
Post a Comment