Rais Donald Trump
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la upelelezi la Marekani FBI James Comey,
ameitaka wizara ya sheria ya nchi hiyo kukanusha hadharani madai ya Rais
Donald Trump kwamba mtangulizi wake Barack Obama alitoa amri ya kunasa
mawasiliano ya simu ya Trump wakati wa kampeni yake ya urais. Gazeti la
New York Times limewanukuu maafisa wa ngazi za juu serikalini ambao
wamesema wanaamini kuwa tuhuma za Trump dhidi ya Obama zilikuwa uongo
mtupu. Kwa mujibu wa ripoti ya New York Times, Comey alitoa rai hiyo kwa
wizara ya sheria siku ya Jumamosi, akisema madai ya Rais Trump hayakuwa
na ushahidi wowote, na kwamba yalitaka kuonyesha kuwa FBI ilivunja
sheria. Bado wizara ya sheria haijatoa tamko lolote. Wachambuzi wengi
wanahisi Trump amemshambulia Obama, kwa dhamira ya kupoteza dira ya
habari kuhusu tuhuma za kuwepo mawasiliano kati ya wasaidizi wake na
maafisa wa Urusi.
No comments:
Post a Comment