Viongozi wa Ujerumani wamekasirishwa na kauli ya Rais
wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye katika hotuba yake jana Jumapili
aliishutumu serikali mjini Berlin kuwa na mienendo ya kinazi.
Akizungumzia kauli ya Rais Recep Tayyip Erdogan katika kipindi kimoja
cha television, Waziri wa Sheria wa Ujerumani Heiko Mass, amesema
shutuma za rais huyo wa Uturuki ni za kipuuzi, zenye nia mbaya, na
zisizo na msingi. Lakini pia amesema pengine hakuna haja ya Ujerumani
kujibu uchokozi wa Rais Erdogan, ili isianguke katika mtego wake. Vile
vile alitahadharisha dhidi ya kumkataza Erdogan kuingia nchini Ujerumani
au kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na nchi yake, akisema hali hiyo
inaweza kuisukumia uturuki katika ushawishi wa rais wa Urusi Vladimir
Putin.Kauli ya Rais Recep Tayyip Erdogan ilitolewa jana katika mkutano wa wanawake mjini Istanbul, ambapo aliishutumu Ujerumani kuulinganisha utawala wake na magaidi, kutokana hasa na kukamatwa kwa mwandishi wa habari mwenye uraia wa Uturuki na Ujerumani Deniz Yucel, ambaye kulingana na Rais Erdogan, si mwandishi wa habari bali ni gaidi. Katika tuhuma zake kali, ndipo Erdogan akasema Ujerumani haijabadilika.
''Nilidhani enzi ya unazi imemalizika nchini Ujerumani, lakini sasa naona kinachoendelea huko, kila kitu kimekuwa wazi. Waziri wangu ambaye alitaka kukutana na waziri wenu, alitaka kutoa hotuba. Kwa nini mna wasiwasi?'' Aliuliza kwa dhihaka Erdogan.
Alipoulizwa kama anaweza kusafiri mwenyewe kwenda Ujerumani, Erdogan amesema akitaka anakwenda Ujerumani hata kesho, na ikiwa Ujerumani itamzuia kuingia au kuzungumza, atazua sokomoko.
Mvutano washamiri kati ya nchi hizo mbili
Kiongozi wa wabunge wa chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel, Volker Kauder, naye amemkosoa vikali Rais Erdogan. Amesema ni vigumu kuamini kuwa kauli kama ile inaweza kutolewa na kiongozi wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya ya Kujihami - NATO, dhidi ya nchi nyingine mwanachama.
Matamshi ya Rais Erdogan yametolewa wakati waziri wake mkuu akifanya juhudi za kupunguza mvutano kati ya Ujerumani na nchi yake, katika mazungumzo aliyoyafanya na Kansele Angela Merkel. Baada ya mazungumzo hayo yaliyodumu kwa saa nzima, Waziri Mkuu huyo wa Uturuki, Binali Yildirim, alisema Uturuki ingeweza kufanya mabadiliko kadhaa ya kimkakati katika kampeni ya kutaka mabadiliko ya katiba.
Waturuki wa Ujerumani wanayo sauti muhimu
Wiki iliyopita mamlaka nchini Ujerumani zilizuia mikutano kadhaa ya hadhara, ambamo mawaziri wa Uturuki wangepigia debe kura ya 'ndio' katika kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mwezi Aprili, inayonuia kuleta mabadiliko ya katiba, yanayompa madaraka makubwa Rais Erdogan. Nchi Ujerumani wapo waturuki zaidi ya milioni 1.4 wenye haki ya kupiga kura nchini mwao.
Msuguano mwingine umetokana na hatua ya Uturuki kumkama mwandishi wa habari mjerumani mwenye asili ya Uturuki, ambapo uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa asilimia 81 ya Wajerumani wanataka serikali ya Kansela Angela Merkel iwe na msimamo shupavu zaidi dhidi ya maneno ya Rais Erdogan na matendo yake.
SHARE
No comments:
Post a Comment