K-VIS
BLOG NA MASHIRIKA YA HABARI
HATIMAYE Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, Mzee
Issa Hayatou,(70), pichani juu, “ameng’oka” kwenye nafasi hiyo kufuatia ushindi mnono
alioupata mpinzani wake, Rais wa chama cha soka cha Madagascar, Ahmad Ahmad, kufuatia
uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo, uliofanyika mjini Addis Ababa Ethiopia leo
Machi 16, 2017.
Katika uchaguzi huo, Ahmad Ahmad alijikusanyia
jumla ya kura 30 ikiwa ni kura 10 zaidi ya Hayatou aliyeambulia 20.
Matokeo hayo yanahitimisha miaka
29 ya utawala wa Hayatou kama kiongozi wa juu wa soka barani Afrika.
Hayatou alikuwa rais wa CAF tangu
mwaka 1988 wakati huo Lionel Messi akiwa na miezi tisa tu tangu azaliwe wakati
mtawala huyo mzaliwa wa Cameroon alipotangazwa kusimamia soka la bara la
Afrika.
Wakati huo huo, kilio cha
Wazanzibara kimepata jibu baada ya mkutano mkuu wa 39 wa Shirikisho la soka
barani Afrika (CAF) unaoendelea mjini Addis-Ababa, Ethiopia, umepitisha ombi la
chama cha soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama rasmi wa CAF.
Ni jambo la kihistoria kwa
Zanzibar kwani safari hii ombi lao limepitishwa bila kupingwa na inakuwa nchi
ya 55 mwanachama wa kujitemea wa CAF.
Awali Zanzibar ilikuwa
inaunganishwa na Tanzania bara chini ya TFF na kupelekea kukosa haki za
kushiriki kama nchi kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF pamoja na yale ya
FIFA.
Pendekezo hilo lilipelekwa na
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndugu, Jamal Malinzi na lilipokelewa
na wajumbe 54 wengine waliokuwepo.
Hii maana yake ni kuwa kwa sasa
CAF ndio shirikisho mwanachama wa FIFA kwa upande wa mabara lenye wanachama
wengi zaidi kuliko wote.
Vilabu vya Zanzibar vimekuwa
vikishiriki mashindano mbalimbali ya CAF lakini kwa ngazi ya kitaifa hawakuwa
na ruhusa na walicheza kwa kuungana na Tanzania bara na kushiriki kama
Tanzania.
Kwa maana hiyo basi, chama cha
soka cha Zanzibar kitapata uwezeshaji wa kifedha moja kwa moja kutoka CAF na
FIFA kwa ajili ya timu ya taifa.
Rais mpya wa CAF, Ahmad Ahmad
SHARE
No comments:
Post a Comment