Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildrim amesema Marekani itahatarisha
uhusiano wake na Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya
NATO, iwapo wapiganaji wa Kikurdi watajumuishwa katika mapambano ya
kuukomboa mji wa Raqqa. Mji huo ni ngome ya kundi linalojiita Dola la
Kiislamu, IS. Uturuki na Marekani zinavutana juu ya mpango wa Marekani
wa kuukomboa mji wa Raqqa huku Uturuki ikipendekeza kuwa majeshi yake
pamoja na washirika wake wa nchini Syria wanatosha kukabiliana na
magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu katika operesheni hiyo. Yildrim
amesema nchi yake haitashiriki katika operesheni yoyote ambayo
itawajumuisha wapiganaji wa Kikurdi. Waziri mkuu wa Uturuki aliwaelezea
waandishi wa shirika la habari la AP pembezoni mwa mkutano na waandishi
wa habari wa nchi za kigeni, kwamba iwapo Marekani itayapendelea makundi
ya kigaidi kuliko Uturuki katika mapambano dhidi ya IS, basi huo
utakuwa ni uamuzi wa Marekani peke yake na kwamba Uturuki haitokubaliana
nao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment