Na Jumia Travel Tanzania
Hivi kuna mkazi yeyote wa jiji la Dar es
Salaam ambaye ni mgeni wa adha zitokanazo na mvua zinazonyesha? Sidhani
kama kuna mtu yeyote hafahamu ya kwamba mvua ikinyesha kutakuwa na foleni
zisizokwisha, barabara na mitaa tofauti jijini kujaa maji, mafuriko na
matamko kadha wa kadha kutoka kwa viongozi wa serikali kuwataka wananchi
wahame mabondeni.
Lakini ni wangapi wametafakari watawezaje
kukabiliana na mvua zitakaponyesha? Zipo mbinu nyingi tu ambazo Jumia
Travel inakushauri uzizingatie ili kipindi cha mvua nyingi za Dar es Salaam
kwako kiwe ni cha kawaida katika mwaka.
Amka mapema kukabiliana na foleni ili uwahi
shughuli zako
Hakuna wakati ambao kunakuwa na foleni
kubwa na zisizopungua kwa muda mrefu jijini Dar es Salaam kama kipindi cha
mvua! Lakini jambo hili sio la kushangaza kwa sababu kila mwaka hali hii
inajirudia.
Na hiki ni kipindi ambacho mabosi wengi
huchukia sana pengine kuliko vipindi vyote vya mwaka maana visingizio vya
wafanyakazi wao kuchekelewa kazini kwa sababu ya mvua huwa haviishi. Kwa
hiyo unakabiliana vipi na hali hiyo?
Kwanza kabisa lazima uwe makini katika
kuwahi kuamka mapema na pia njia ya usafiri utakayoitumia. Inakubidi kuwahi
kuamka mapema sana kama unategemea usafiri wa umma au binafsi. Kwa sababu
ukifanya hivyo kama kutakuwa na foleni barabarani basi utaziwahi
ukilinganisha na ukichelewa kuingia barabarani. Lakini pia kama unategemea
usafiri wa umma, mabasi ya mwendokasi ni mkombozi mkubwa kwenye kipindi
hiki. Hivyo kwa maeneo ambayo usafiri huu unapatikana ni vema kuutumia
ipasavyo kwa sababu yenyewe hayakai foleni kutokana na kuwa na njia zao
pamoja na kupewa kipaumbele.
Nunua vifaa vya kujikinga na
mvua
Kutokana na jiji la Dar es Salaam kuwa na
vipindi virefu vya jua na joto kali, imekuwa ni nadra sana kuwakuta wakazi
wake wana vifaa vya kujikinga na mvua kama vile mwamvuli, koti, sweta au
viatu vya mvua. Inashauriwa kuwa na vifaa hivi nyumbani kwako ili kujikinga
ifikapo kipindi cha mvua na sio kuanza kufikiria kununua kwani inawezekana
usiwe na bajeti hiyo pindi unapovihitaji. Vifaa hivyo ni muhimu kwani
hukukinga na baridi, kutolawana, magonjwa na hata kutunza mavazi yako
kutokana na maji ambayo huweza kusababisha kuharibika.
Umakini kwenye chombo chako cha
usafiri
Kwa wenye vyombo vya usafiri wanajua
wenyewe ni kadhia gani wanayokumbana nayo ikifika kipindi cha mvua. Kipindi
hiki ni jambo la kawaida kukuta magari kadhaa yamezimika au kukwama
barabarani kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi. Lakini pia barabara
nyingi huharibika na kutopitika kabisa hivyo kulazimisha chombo chako
kupita ni kujitafutia kuingia gharama zisizohitajika siku za usoni. Kama
inawezekana tafuta njia mbadala ya usafiri katika kipindi hiki au pita
kwenye njia ambazo una uhakika ni salama kwa chombo chako.
Kuwa makini na vifaa vyako vya
umeme
Siyo vifaa vyote vya umeme vimetengenezwa
vikiwa na uwezo wa kuzuia maji kutokuingia ndani yake. Licha ya makapuni
mbalimbali kuja na teknolojia hiyo lakini unashauriwa kuwa makini sana
aidha kwa kuvivika vifaa maalumu vya kuzuia maji au kuvikinga kabisa na
maji. Kipindi hiki ndicho ambacho wengi hupatwa na majanga ya kuharibikiwa
na simu, kompyuta, radio pamoja na luninga huko majumbani.
Kuwa makini na vyakula
utakavyokula
Kama huwa unakuwa makini na aina ya vyakula
unavyokula basi kipindi hiki inabidi uwe makini zaidi. Mvua zikinyesha
jijini Dar es Salaam ndiyo kipindi ambacho pia kunakuwa na mlipuko wa
magonjwa kadha wa kadha kama vile kipindupindu. Inashauriwa kula chakula
sehemu ambayo unaiamini na inayozingatia usafi wa hali ya juu au kama
inashindikana uwe unabeba chakula unachopika mwenyewe au kutokula kabisa.
Sio watu wote wana utaratibu wa kusoma
vitabu kwenye siku zao za kawaida badala yake wanatazama filamu, kusikiliza
muziki, kutoka wikendi au kupendelea kutembea. Lakini katika kipindi hiki
ambacho mvua zinanyesha, barabara hazipitiki, hali ya hewa ni baridi na
sehemu nyingi za starehe au kutembelea zinakosa watu ni vema ukajaribu
kusoma vitabu. Amini usiamini kuwa hata kutazama filamu na kusikiliza
muziki hufikia mahala vinachosha, hiki kinaweza kikawa ni kipindi kizuri
cha kujaribu kitu tofauti, nunua vitabu na usome ili uongeze
maarifa.
Hivyo basi tusiifanye mvua ikawa ni
kisingizio cha kutofanya shughuli zingine au majukumu mengine
yanayotukabili. Kila kipindi huja na changamoto pamoja na fursa zake, ni
vema kupambana nazo na kuzitumia ili kusonga mbele.
SHARE
No comments:
Post a Comment