Na:
Lilian Lundo – MAELEZO
Pombe kali
zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki
maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa
Jijini Dar es Salaam katika msako wa pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01
mpaka 03, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali
ya kusitisha pombe hizo za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
“Jumla ya katoni
99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba)
zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa na mililita 50, katoni 29,344 zenye ujazo wa
mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa
zenye ujazo wa mililita 100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,”
alifafanua Makamba.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala
4, baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio
vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika opesheni hiyo.
Makamba amesema kuwa,
pombe zilizokamatwa zimezuiliwa kuuzwa au
kusambazwa kutoka katika maeneo ambayo yamehifadhiwa yaani viwanda, maghala
pamoja na maduka ya jumla mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko.
Aidha wananchi wametakiwa
kushiriki katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kutoa taarifa
zitakazowezesha kubaini wanaokaidi agizo la Serikali la kuzalisha, kusambaza,
kuuza au kutumia pombe hizo kupitia namba ya simu 0685 333 444 kwa kutuma ujumbe mfupi wa meseji au whatsapp
au kwa kupiga simu.
Vile vile amesema
kuwa zawadi kati ya shilingi laki 5 hadi milioni 1 zitatolewa kwa mwananchi
atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote mwenye
ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha sheria, watu au
mtu anayeingiza pombe za viroba nchini
kutoka nje ya nchi kinyume na sheria na utaratibu, anayehamisha au kusafirisha
pombe za viroba kinyume na sheria, mtu mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha pombe
za viroba ambao hautambuliki na Serikali pamoja na mtu anayetumia stempu feki
za TRA .
Pombe za viroba
zimechangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya
Taifa, ajali na vifo vinavyosabaishwa na unywaji uliokithiri wa pombe hizo,
kuongezeka kwa vitendo vyauhalifu na kupotea kwa mapato yanayosababishwa na
wafanyabiashara wasio waamini.
Kutokana na athari
hizo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa
Mkoani Manyara, Februari 16 mwaka huu alitoa tamko la kusitisha uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na utumiaji wa pombe kali za viroba kwa nchi nzima kuanzia
Marchi 01, mwaka huu.
SHARE
No comments:
Post a Comment