Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine
Mahiga amefanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Kansela wa Ujerumani
Angela Merkel, Balozi Harro Adt, ambapo alipokea, niaba ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ujumbe maalum
kutoka kwa Kansela Markel.
Akizungumzia
ziara ya Balozi Adt nchini, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa "Kansela
Merkel amemtuma Balozi Adt, kuleta ujumbe maalum ambao ni ombi kwa Rais
Magufuli la kuisaidia Ujerumani katika kugombea nafasi ya kuwa mjumbe wa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi wa nafasi hiyo
unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018".
Balozi
Dk. Mahiga alieleza kuwa dhamira ya Ujerumani ya kugombea nafasi hiyo ni
kusaidia mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa
ni pamoja na kuridhia nchi za Afrika katika mchakato wa kupokea nafasi
mbili za kudumu katika baraza hilo. Nchi nyingine zinazogombea nafasi
hizo ni Israel na Ubelgiji.
Balozi
Mahiga alisema kuwa, Ujerumani imeahidi masuala kadhaa kama vile
kusimamia amani katika jumuiya ya kimataifa na katika ukanda wa Afrika,
kusimamia haki za binadamu katika ngazi ya dunia na kuendelea kuimarisha
uhusiano wake na nchi nyingine.
Aidha,
Ujerumani imesisitiza nia yake ya kuunga mkono mageuzi mapya katika bara
la Afrika ambayo yataikomboa Afrika na kuleta maendeleo zaidi barani
humu.
Katika
mazungumzo hayo, Balozi Dk. Mahiga alisema kuwa ameiomba Ujerumani
isaidie ujenzi wa jengo mahususi la mahakama ya Afrika iliyopo mjini
Arusha ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo mzima wa mahakama barani
Afrika pamoja na kuisaidia Afrika katika kupambana na masuala ya
mabadiliko ya tabianchi.
Kwa
upande wake, mjumbe maalum kutoka Ujerumani Balozi Adt, alisema kuwa
amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata alipowasili nchini.
Aidha,
Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujenrumani alieleza matumaini yake kuwa
Tanzania ambayo ni rafiki wa Ujerumani kihistoria itatoa msaada juu ya
nafasi hiyo ili kusaidia kutekeleza malengo waliojiwekea kiufanisi
kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu katika Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa.
Uhusiano
kati Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria na wakati wote nchi mbili
hizo zimekuwa zikifanya kila jitihada za kuuimarisha.
Chini ya
uhusiano huo, Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta
mbalimbali za maendeleo kama vile elimu, miundombinu na wanyamapori.
SHARE
No comments:
Post a Comment