Wa-Baha’i duniani kote Washerehekea Naw-Rúz
Naw-Ruz (Mwaka Mpya) katika Imani ya Baha’i ni mojawapo ya siku tisa zinazosherehekewa na Wa-Baha’i duniani kote. Naw-Rúz huashiria ujio wa musimu wa mchipuo katika mzingo wa Kaskazini.
Naw-Rúz ni siku ya kwanza ya kalenda ya Ki-Baha’i ambayo pia ni maarufu kama Badi (‘nzuri ajabu’) kalenda. Katika siku hii, Wa-Baha’i hawaendi kazini wala shuleni. Mtukufu Báb, Mtangulizi wa Baha’u’llah, Mtume Mwanzilishi wa Imani ya Bahá’í, aliteua siku hiyo kama siku takatifu na kuishirikisha na Jina Kuu Kabisa la Mungu. Kalenda ya Ki-Baha’i imethibitishwa na Baha'u'llah.
Kalenda ya Ki-Baha’i ina jumla ya miezi 19 ambayo kila moja ina siku 19 (jumla siku 361). Zaidi ya hapo zipo ‘Siku za Kati’ (4 katika mwaka wa kawaida na 5 katika mwaka mrefu) kati ya mwezi wa 18 na 19 kwa ajili ya kuurekebisha mwaka kufuata kalenda ya mwaka wa jua. Mnamo mwezi wa mwisho wa Ki-Baha’i, Wa-Baha’i hufunga na hawali chakula wala kunywa chochote kutoka alfajiri hadi jioni, na pia husali, hutafakari na kujitahidi kurekebisha tabia zao, kutakasa mioyo yao na kufikia kiwango cha juu zaidi cha kujitenga na vitu vya duniani. Sherehe ya Naw-Rúz hufika mwisho wa mwezi wa kufunga wenye siku 19.
Baha’u’llah amekuja kuleta umoja, kuunganisha jamii nzima ya wanadamu katika Hoja moja, Imani moja ya ulimwengu, kutokomeza kila aina ya ubaguzi na kuleta utambuzi kuwa sisi sote ni ndugu. Kwa uhakika, Baha’u’llah anatuambia, “Mwangaza wa Umoja una Uwezo mkubwa sana kana kwamba unaweza kuangaza dunia nzima.” Yeye anatuambia kwamba sisi sote ni kama matunda ya mti mmoja, majani ya tawi moja, mawimbi ya bahari kuu moja, maua ya bustani moja maridhawa ya jamii ya wanadamu.
Mnamo Naw-Ruz, Wa-Baha’i hukusanyika kwa furaha kubwa kabisa kwa sababu huu siyo tu mwanzo wa Mwaka Mpya, bali ilivyoelezwa na Abdu’l-Bahá, mwanae Bahá’u’lláh na Kiolezo Kamilifu wa Imani ya Baha’i, “Sasa ndio mwanzo wa duru la Uhalisi, Duru Jipya, Zama Mpya, Karne Mpya, Wakati Mpya na Mwaka Mpya. Kwa hiyo umebarikiwa sana.”
Katika zaidi ya maeneo 120,000 ambamo zaidi ya Wa-Baha’i milioni 6 huishi ulimwenguni kote, sherehe za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Ki-Baha'i zinachukua maumbile tofauti.
Jamii Baha’i ya Dar es Salaam itasherehekea Naw-Rúz siku ya Jumapili, tarehe 19 Machi, 2017 saa 12:30 jioni katika Baha’i Senta, iliyopo katika Mtaa wa Mfaume, Upanga Magharibi. Kila mmoja anakaribishwa kwa moyo mkunjufu katika sherehe hii yenye furaha na nderemo. Ratiba itakuwa na sehemu ya maombi ambamo sala na dua za Ki-Baha’i zitasomwa na kuimbwa katika lugha mbalimbali, kinafuata ni kujuana hali na kuburudika pamoja. Karibuni tena.
SHARE
No comments:
Post a Comment