Mitambo ya kusukuma maji katika eneo la Ruvu Juu ambayo ni mipya na sasa inaongeza idadi ya uzalishaji maji toka lita milioni 82 hadi milioni 196 kwa siku. |
Pampu nne za kunyonya maji kutoka mtoni katika kituo cha Ruvu Darajani zikiwa zinafanya kazi baada ya umeme kuongezwa. |
Maji yakiingia toka katika mitambo ya kunyonya maji tayari kwa kusafishwa kwa kuweka dawa ndani ya eneo hili na kisha kupelekwa katika mtambo mwingine wa kusafisha maji tayari kwa kusafirishwa. |
Mtambo huu ni sehemu ambapo maji huendelea kusafishwa na kisha kupelekwa katika mtambo maalum wa kukusanya na kusafirisha kwenda kwa wananchi. |
Matanki makubwa ya maji yenye mitambo maalum ya kusafisha maji kama inavyoonekana hapa maji yakiendelea kusafishwa. |
Sehemu hii ni ya mtambo ambapo maji yanawekwa dawa na kisha kupelekwa katika sehemu ya mtambo mwingine kwa ajili ya kusafishwa na kusafirishwa kwa wananchi. |
(PICHA/HABARI NA MWANDISHI WETU)
Baada ya kazi ya kuunganisha umeme wa
kutosha kukamilika 15 Aprili, 2017 kazi ya kuwasha pampu kubwa mpya za
majighafi na majisafi katika Mtambo wa Ruvu Juu sasa imekamilika rasmi ambapo
mtambo huo sasa umeanza kuzalisha lita milioni 196 kwa siku. Taarifa ya Mamlaka
ya Majisafi na Majitaka Dar Es salaam (DAWASA) inaeleza.
Ili kufikia uwezo huo wa uzalishaji
kutoka lita milioni 82 zilizokuwa zikizalishwa hapo awali, kazi mbalimbali
zilifanyika ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma maji na ufungaji wa
pampu mpya, maeneo mapya ya kusafisha maji, mitambo ya kuchuja maji, maeneo ya
kuchuja tope na tenki kubwa la kuhifadhia maji safi.
Katika kuhakikisha kuwa maji hayo
yanawafikia wananachi, kituo kipya cha kusukuma maji safi na salama kilijengwa
sambamba na mabomba makuu ya kusafirishia maji hayo yenye jumla ya urefu
wa kilomita 70 kutoka Mlandizi hadi Dar es salaam.
Aidha, tenki jipya lenye uwezo
wakuhifadhi lita milioni 10 limejengwa eneo la Kibamba lenye mwinuko; na kutoka
hapo maji hushuka kwa nguvu ya mtiririko hadi katika matenki ya Kimara.
Kazi iliyokuwa imebaki ilikuwa ni
kuongeza nguvu ya umeme ili kuwezesha pampu hizo mpya kufanya kazi. Hivi sasa
kazi hiyo imekamilika, ukaguzi umefanyika na pampu moja baada ya nyingine
zimewashwa ili kuhakiksha mfumo mzima sasa unafanya kazi.
Hadi kufika jana jioni (17
Aprili) maji yalikuwa yanaingia katika matenki yote kwa kupitia mabomba
mapya bila matatizo.
Mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu sasa
unapokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo kituo kidogo
cha umeme cha Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo inawezesha
pampu zote mpya na za kisasa zilizofungwa kuwashwa kwa wakati mmoja.
Mikataba ya jumla ya dola za Marekani
milioni 99 ya upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu
mpaka Kimara, ujenzi wa tanki kubwa lenye ujazo wa lita million 10, ofisi kwa
ajili ya shughuli za uendeshaji wa huduma na nyumba za watumishi wa mtambo
ilisainiwa mwaka 2014. Fedha hizo zilikuwa ni mkopo wa masharti nafuu toka
Benki ya Exim ya India.
Kazi inayopewa msukumo mkubwa kwa
sasa ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji yaliyoongezeka ili
wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na jitihada na uwekezaji uliofanywa na
Serikali yao.
Maeneo yanayonufaika ni pamoja na
miji ya Kibaha, Mlandizi na baadhi ya Vitongoji vyake katika mkoa wa Pwani
pamoja na maeneo yote yaliyopo jirani na barabara ya Morogoro yaani Kiluvya,
Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo, Malamba mawili, Msigani, Msakuzi, Makabe,
Kibangu, External, Makuburi, Tabata, Segerea, Buguruni pamoja na Vingunguti.
SHARE
No comments:
Post a Comment