TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
KAMA mnavyofahamu, Chama Cha
Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kina historia ndefu ya kutetea
maslahi ya wakulima masikini na
wafugaji nchini dhidi ya wimbi la sasa la wawekezaji wa kigeni na wa ndani
kukodishwa ardhi kubwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kilimo kikubwa cha
kibiashara kikiwemo cha nishati mimea (biofuels) au nishati hai kama wengine wanavyoiita, kilimo cha miwa na miti
ya mbao.
Katika siku za karibuni, migogoro ya
wakulima na wafugaji imekuwa ikiongezeka siyo tu kwa idadi bali pia kwa madhara
yanayotokana na migogoro hiyo. Kadhalika migogoro hii haipo katika sehemu moja
ya nchi bali imesambaa karibu nchi yote, hasa katika sehemu za mashambani
ambako pia malisho na maji yanapatikana. Vifo, majeruhi, kuchomwa nyumba na
kuuawa mifugo ni mambo yanayoashiria ukubwa wa migogoro.
Mamlaka kadhaa zimefanya jitihada
mbalimbali kutafuta suluhu ya migogoro hiyo lakini mafanikio yamekuwa haba.
Serikali za vijiji zimekuwa zikisuluhisha migogoro hiyo, na hata pale ambapo
wameweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kushirikisha makundi yote kama
njia mojawapo ya kumaliza tatizo hilo, mipango hiyo imekuwa haiheshimiki na
mara nyingi wafugaji wamekuwa wakiondoka kwenye maeneo yao na kuingiza mifugo
kwenye mashamba ya wakulima.
Kamati za usalama za wilaya na mikoa
pia zimefanya jitihada kubwa kutatua migogoro hii. Kuna wakati wizara kadhaa
ziliungana ili kutafuta suluhu pale mapigano makali yalipotokea Wilayani
Mvomero kati ya wakulima na wafugaji ambayo yalisababisha vifo na nyumba
kuteketezwa kwa moto. Kinachoonekana kuchochea migogoro hiyo ni kundi moja
kutoka sehemu yake na kulifuata kundi jingine na kufanya uharibu huko, kisha
kutoroka na kurudi maeneo yao.
Migogoro hii haiwezi kuachwa ikaendelea kwani
pamoja na kugharimu vyakula na mifugo, husababisha uharibu wa vyanzo vya maji
na mazingira kwa ujumla hasa pale mifugo inapoingizwa sehemu isiyoruhusiwa na
wakulima kuendesha shughuli zao maeneo yaliyozuiliwa.
Ndiyo maana JET inachukua nafasi hii
kupongeza hatua zilizochukuliwa na wakuu wa nchi kwa nia ya kukomesha migogoro
hii na kurudisha amani katika meneo husika ili wananchi waweze kuendelea na
kazi zao za kuendesha maisha na kujitafutia maendeleo.
Akiongea katika kijiji cha Fukayosi
wilayani Bagamoyo, Rais Dkt. John Magufuli aliagiza uongozi wa wilaya kuhakikisha
kuwa kila mfugaji au mkulima atayempiga mwingine au kuingilia maeneo yake ni
lazima akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Rais
alisistiza kuwa kuwepo kwa migogoro kunasababisha uvunjifu wa amani na kuathiri
maisha ya kila siku ya jamii husika, hivyo wote wanaosababisha mambo hayo
lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Agizo la Mh. Rais limefuatiwa na amri
ya Mh. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoitoa katika wilaya ya Bagamoyo tena
wiki iliyopita, akitaka wale wote wanaopiga wakulima na kuigiza mifigo katika
mashamba yao wasakwe, wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hii ni hatua muhimu iliyochukuliwa na
viongozi wakuu wa nchi kwa nia ya kuhakikisha kuwa migogoro baina ya makundi
hayo mawili inakomeshwa na amani kurejeshwa. Amri zilizotolewa na wakuu wa nchi
ni ishara tosha kuwa migogoro hii imefika hatua mbaya na ni wajibu wa mamlaka
husika kutekeleza maagizo hayo ili kuleta amani baina ya makundi hayo.
Tunawapongeza viongozi wetu kwa hatua
hiyo na nyinginezo walizokwisha kuchukua. Ni imani yetu kuwa wahusika
watatekeleza maagizo hayo na kwamba tutafika mahali ambapo wakulima na wafugaji
wataishi kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwani kila kundi linamhitaji mwingine
ili liweze kustawi.
SHARE
No comments:
Post a Comment