DK HASSAN ABBASI
UMUHIMU WA JAMII KULINDA HAKI NA USALAMA WA WANAHABARI
Dodoma, Jumatatu, April 24, 2017:
Serikali
imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya
waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya
wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda
kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti
polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika
shambulizi hilo.
Tunachukua fursa
hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa
kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na
nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika
migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.
Kifungu cha 7
(1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru
wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya
matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa
kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa
mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.
Tunawatakia
nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na
jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba
wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika
vilifanyiekazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa
Serikali
SHARE
No comments:
Post a Comment