Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Eric Shitindi, akiwahutubia wafanyakazi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kikao chao cha baraza. Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala Bi. Khadija Mwenda na viongozi wa baraza hilo. |
Na Mwandishi Wetu
Mabadiliko ya mazingira ya ufanyaji biashara
yanayoletwa na maendeleo ya uchumi wa viwanda pamoja na mnyororo wa thamani,
yameelezwa kuwa changamoto kubwa katika jitihada za kuimarisha hali ya usalama na
afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi hapa nchini.
Changamoto hiyo imetolewa na Katibu Mkuu katika
Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Bw, Eric
Shitindi, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usalama
na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mjini Dodoma leo.
Amesema mabadiliko hayo yanahusisha matumizi ya
teknolojia za kisasa na ongezeko kubwa la idadi ya wafanyakazi katika sekta
zote za umma na za binafsi jambo ambalo linahitaji utaalamu mkubwa katika
kuweka na kusimamia mifumo ya kulinda afya na kuwahakikishia usalama
wafanyakazi wote wanapokuwa katika sehemu zao za kazi.
“Hivyo mkiwa kama wataalamu katika masuala ya
Usalama na Afya mahali pa kazi mnatakiwa kuwa na mikakati mipya ya kukabiliana
na changamoto hizo. Hii itakuwa ni pamoja na kubadilika kifikra na kimtazamo
katika utendaji kazi,” alisema Katibu mkuu Shitindi.
Katibu mkuu huyo amesisitiza muhimu wa kutafuta
mbinu mbadala ya kuweza kupanua wigo wa kufanya kazi hasa kwa kuzingatia ukubwa
wa kazi zilizopo.
Aidha Bw. Shitindi ameupongeza OSHA kwa mafanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango kazi wake katika kipindi cha robo
tatu za mwaka huu wa fedha (2016/2017) ambapo kwa mujibu wa taarifa
iliyowasilishwa katika baraza hilo, taasisi imevuka malengo katika kaguzi, utoaji wa mafunzo ya
usalama na afya kazini pamoja na huduma mbali mbali zitolewazo mahali pa kazi.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu aliahidi kuendelea
kuisaidia OSHA kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za kiutendaji na kuwaasa watumishi
wa Wakala kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuepuka kujihusisha na
vitendo vya upokeaji rushwa wanapotekeleza majukumu yao.
“Wizara imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya namna
mnavyohudumia wateja na kushuka kwa maadili ya kiutendaji miongoni mwa
watumishi, mfano masuala ya rushwa, hivyo wakati tunaendelea kushughulikia
matatizo hayo ni vyema sasa mkaanza kubadilika kwa kufuata sheria, taratibu,
kanuni na miongozo mbalimbali ya utendaji kazi katika taasisi,” amesisitiza Bw,
Shitindi.
Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi wa OSHA ambacho
kimeanza leo kitamalizika kesho ambapo pamoja na mambo mengine kitapitia na
kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha wa (2017/2018) ili
kujiridhisha kama itawawezesha kufanikisha utekelezaji wa malengo ya wakala
yaliyowekwa.
SHARE
No comments:
Post a Comment