KAMATI ya Ulinzi na Usalama wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeziruhusu
halmashauri za Msalala na Ushetu kuanza kuteketeza wanyama wakali aina
ya fisi, wanaotishia usalama wa wananchi.
Taarifa hiyo ilitolewa kwa vyombo vya habari hivi karibuni na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema hayo baada ya kikao cha
kawaida cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilicholenga
kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo.
Berege alisema kwa sasa halmashauri hizo mbili, Msalala na Ushetu,
zinaendesha kazi ya kuwasaka fisi hao wanaotishia maisha ya wananchi na
kuwaua kwa kutumia bunduki ili kunusuru maisha ya wananchi hao.
“Hawa fisi wakiingia vijijini wanatishia maisha ya wananchi hasa
wanawake na watoto, lakini fisi hawa wanawaogopa wanaume hivyo kwa
ruhusa ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, tumeanzisha oparesheni
maalumu ya kuwatokomeza fisi kwa kuwaua kwa kutumia bunduki na sumu,”
alisema Berege.
Alisema siku hiyo wakati akizungumza na wandishi wa habari ofisini
kwake, fisi mmoja tayari alikuwa ameuawa na maofisa wa idara ya
wanyamapori katika Kata ya Chela, baada ya kutaka kutafuna watoto.
Aliswema fisi waliouawa hadi sasa ni 14. Akifafanua juu ya idadi ya fisi
waliouawa ili kunusuru wananchi kuliwa na fisi hao, mkurugenzi huyo
alisema katika Kijiji cha Kakola waliuawa fisi saba, Kata ya Ngaya fisi
sita na Kata ya Chela aliuawa fisi mmoja.
IMEANDIKWA NA RAYMOND MIHAYO,- HABARILEO KAHAMA
SHARE
No comments:
Post a Comment