NA MAGRETH KINABO –MAHAKAMA YA TANZANIA.
JAJI Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Ferdinand
Wambali, (pichani kushoto), amewataka Majaji na Mahakimu kuzingatia maadili ya Uhakimu na Utumishi
wa Umma na kutenda haki wakati wanapotimiza majukumu yao.
Aidha, Jaji huyo alisema Majaji na mahakimu wanapotimiza
majukumu yao wanapaswa kuzingatia kanuni za utendaji wao na za utumishi wa umma
hatua ambayo itawafanya kukidhi matakwa ya wananchi wanaowahudumia.
Kauli hiyo, imetolewa na Mhe. Jaji huyo
wakati akizungumza na baadhi ya Majaji na Mahakimu mbalimbali katika
kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi mndogo wa Bunge
uliopo jijini Dar es Salaam.
“Suala la maadili lilianza tangu enzi za kale, jamii
ilikuwa inajiwekea maadili, uwepo wa maadili ni heshima na utii, tabia ya
uaminifu, uwajibikaji na kufuata utaratibu kila unapotekeleza kazi,”
alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi huku akisema masuala yalizishazungumziwa na
baadhi ya viongozi wa kitaifa, akiwemo Baba wa Taifa mwaka Machi 15,
mwaka 1984 na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa Novemba 27, mwaka 2011.
Aliongeza kuwa suala la maadili ni muhimu katika
kupambana na rushwa, pia linafanya Jaji na Hakimu awe na tabia njema mbele ya
jamii, hivyo kazi hizo zinahitaji uadilifu na mtu mwenye hofu ya Mwenyezi
Mungu.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es
Salaam Mhe. Beatrice Mutungi akifungua kikao hicho, alisema kuwa lengo la kikao
hicho lilikuwa kujadili changamoto za kada hizo na kubadilishana uzoefu wakati
wa kutatua changamoto hizo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya viongozi
mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.
SHARE
No comments:
Post a Comment