Serikali imesema kuwa mabadiliko ya
sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji
wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki
nchini ili kuruhusu mfumo wa Soko Huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango
vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
alipokuwa akijibu swali la msingi
la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jesca
David Kishoa (CHADEMA), aliyehoji licha ya kuwa na benki nyingi zaidi kuliko
nchi zote Kusini na Mashariki mwa Afrika, kwa nini wingi huo bado haujaleta
unafuu katika tozo ya riba.
Akijibu
swali hilo Mhe. Dkt. Kijaji alisema kuwa, viwango vya riba za mikopo hupangwa
kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, uendashaji, bima, sifa za
mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo, pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
“Dhana ya uhitaji na utoaji wa mikopo siyo kigezo pekee kinachoweza kupunguza viwango vya riba hapa nchini, hatari ya kutolipa mkopo ni kigezo kikubwa kinachotumiwa na benki kupanga viwango vya riba za mikopo, hususan kwa wajasiriamali wadogo”. Alisema Dkt. Kijaji
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa, uzoefu uliopo unaonesha kuwa, benki zinapendelea kukopesha
wajasiriamali waliojiunga katika vikundi kuliko mjasiriamali mmoja mmoja ili
kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika.
Aidha, Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jesca David Kishoa, alihoji ni kwa nini Serikali isiweke ukomo wa riba kisheria kwa benki hizo ili kumsaidia mjasiriamali wa sekta binafsi kama ilivyofanya nchi ya Kenya.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya Mwaka 1991, iliyotungwa kwa kuzingatia misingi ya mfumo wa soko huria, Benki Kuu imepewa jukumu na mamlaka ya kusimamia na kuzichukulia hatua taasisi za fedha zinazoendesha shughuli zao kwa hasara.
Aliongeza kuwa, kutoa maelekezo kwa benki kutumia viwango fulani vya riba, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuzichukulia benki hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza.
Katika
swali la nyongeza Mbunge huyo, alieleza kuwa mikopo isiyolipika imekua kwa
kiwango kikubwa tangu mwaka 1991 huku akitaja sababu kubwa mbili ambazo ni
mazingira magumu ya biashara pamoja na riba kubwa kwa wafanyabiashara hao.
‘’Je
Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kwa kuwapa riba nafuu ili iweze
‘Kustimulize’ (kuchochea) biashara zao’’. Alihoji Mhe. Kishoa.Akijibu
swali hilo la nyongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa mwaka 1991 ya sheria ya
Mabenki na Taasisi za fedha, Benki Kuu au Serikali haiwezi kutoa mweleko au
ukomo wa Taasisi za fedha.
Mwisho
SHARE
No comments:
Post a Comment