Na Nuru Juma & Husna Saidi-Maelezo.
Shirikisho la Mpira wa Kikapu
Tanzania (TBF) linajiandaa kushiriki mashindano ya kanda ya Zone 5
Kimataifa kwa watoto chini ya umri wa miaka 16 yatakayofanyika mjini
Mombasa nchini Kenya kuanzia tarehe 1-6 Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa
habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es salaam
leo, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Michael Mwita alisema
mashindano hayo yatatumika kupata timu itakayowakilisha kanda ya Zone 5
na baadaye kuwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Dunia ya
mchezo huo.
Alifafanua kuwa zimeundwa timu
kutoka Mikoa mbali mbali ambapo mazoezi rasmi ya mchujo wa wachezaji
kupata timu itakayowakilisha Taifa yataanza tarehe 20 mwezi huu katika
viwanja vya JMK sports Complex jijini Dar es Salaam.
“Tumeshathibitisha ushiriki wa
timu yetu na vijana wameshaanza mazoezi tangu mwezi Januari na tumeandaa
bajeti ya mil.30 ili kuweza kufanikisha mashindano hayo ambayo kwa
Tanzania ni mara ya kwanza kushiriki”, alieleza Mwita.
Aliongeza kuwa mshindi
atakaepatikana kwa kanda ya Zone 5 atakutana na washindi wengine wa
kanda sita kwa upande wa bara la Afrika na kisha kupata timu
itakayowakilisha bara la Afrika na kukutana na bara la Amerika, bara la
Ulaya na bara la Amerika ya Kusini ili kumpata mshindi wa Dunia.
Kwa upande wake kocha wa timu
hiyo, Bahati Mgunda alisema ameamua kuteua makocha wasaidizi katika
Mikoa mbali mbali ili mchezo huo wa kikapu uweze kuenea nchi nzima.
Mgunda alisema wanahitaji kuwalea
watoto wa jinsia zote wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 14 watakaopenda
kujiunga na mchezo huo wa mpira wa kikapu na baadaye kuwaunganisha
katika timu kubwa na kuweza kushiriki mashindano ya Kitaifa.
Katika kanda ya Zone 5 nchi
zitakazoshiriki mashindano hayo ni Tanzania, Kenya, Sudan, Sudani
Kusini, Uganda, Burundi, Rwanda, Misri na Somalia.
SHARE
No comments:
Post a Comment