TRA

TRA

Wednesday, May 17, 2017

WADAU WAIPONGEZA SERIKALI KWA UAMUZI WA KUIVUNJA MAMLAKA YA USTAWISHAJI WA MAKAO MAKUU, DODOMA (CDA)

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !




NA FRANK SHIJA - MAELEZO
WADAU mbalimbali wameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuivunja Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) iliyofikiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Wakitoa maoni yao juu ya umauzi huo wa Serikali, wameeleza kuwa kuvunjwa kwa Mamlaka hiyo kumekuja wakati muafaka kwani kutapunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiendelea katika Manispaa ya Dodoma.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana,iliyokuwa inashughulikia changamoto za wananchi dhidi ya CDA, Bw. Aron Kinunda alisema kuwa uamuzi huo huko sahihi kwani umekuja wakati muafaka kwa kuzingatia malengo halisi ya uanzishaji wa mamlaka hiyo kuwa yamekamilika kwa asilimia kubwa ukizingatia na mahitaji halisi ya wakati huu.
“Ni hatua nzuri katika mustakabari wa maendeleo ya Dodoma, kwani sasa migogoro mingi ya ardhi iliyokuwa inatokana na mgongano wa kisheria haitarajiw kujitokeza tena na badala yake Manispaa itajikita katika kuweka mazingira rafiki ya umiliki wa ardhi ikiwemo kuongeza muda wa hati ya umiliki kutoka miaka 33 hadi 99 kama ambavyo maeneo mengine ya nchi yanavyofanya.” Alisema Kinunda.
Aliongeza kuwa wananchi watakuwa wamefarijika sana kwani walikuwa wanaiona CDA kama adui yao mkubwa ambapo imesababisha malalamiko mengi ya kuchukuliwa ardhi zao bila ya kulipwa fidia na urasimu katika upimaji na utoaji wa hati za viwanja.
Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuwa CDA hakuna usimamizi mzuri wa ardhi jambo linalosababisha kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi itokanayo na mgongano wa kisheria uliopo kati ya Mamlaka hiyo na Manispaa ya Dodoma.
“Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999 inatambua umiliki wa ardhi upo chini ya Serikali za Mitaa, kitu ambacho kwa Dodoma ni tofauti kwa kuwa ardhi yote iliyopimwa iko chini ya CDA kitu ambacho hata Manispaa imekuwa mpangaji,” aliongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Dodoma, Mzee Chidawali amesema kuwa uamuzi wa uamuzi huo umepokelea kwa nderemo na vifijo na ambapo asilimia kubwa ya wakazi wa Dodoma wanaona ni kama ukombozi kwao.
“ Rais Magufuli anapaswa kupongezwa sana kwa uamuzi aliouchukua wa kuivunja CDA hakika amefanya jambo jema sana, sasa wananchi watapata ahueni katika kushughulikia masuala yao ya umiliki wa ardhi,” alisema Chidawali.
Aidha aliongeza kuwa katika upande wa taaluma ya uandishi wa habari uamuzi huo umewasaidia kurejesha uhusiano mwema baina yao na wananchi kwani wamekuwa wakiacha kuripoti habari za maendeleo badala yake wamekuwa wakijikuta wanaandika habari kuhusu migogoro ya ardhi zaidi iliyokuwa inasababishwa na CDA.
Chidawali alisema kuwa baada ya kupata taarifa juu ya uamuzi huo amepata fursa ya kusikia maoni ya wadau mbalimbali ambapo kwa nyakati tofauti wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua jambo linalotoa tafsiri chanya juu ya dhamira njema ya Serikali yake ya kuwajali wanyonge.
“Binafsi nje ya taaluma ya habari mimi ni mzawa wa Dodoma tumekuwa na malalamiko ya muda mrefu hasa kuhusu uhalali wa kumiliki ardhi, tunaitwa wavamizi katika maeneo ambayo tumekuwa tukiyamiliki enzi na enzi,” alifafanua Chidawali.
Naye Mwenyekiti wa Soko la Chadulu Jakton K. Matoto amesema kuwa Jumuiya yao imepokea kwa mikono miwili uamuzi huo na kuongeza kuwa ni imani yao kuwa baada ya Manispaaa kuchukua majukumu ya CDA itakwenda kufanya mapitio na kutatua migogoro yote iliyokuwa ikiendelea kutokana na uwepo wa mamlaka hiyo.
Mwenyekiti huyo ameonyesha matumaini ya mji wa Dodoma kukua kutokana na kile anachodai kuwa CDA ndiyo cahnzo cha Dodoma kubaki nyuma kimaendeleo kwani wawekezaji wengi wamekuwa wakishindwa kuwekeza kutokana na muda mfupi wa hati ya umiliki wa ardhi ambapo mmiliki anapewa miaka 33 wakati maeneo mengine ya nchi muda ni miaka 99.
Wakati huohuo Matoto ametoa rai kwa Manispaa ya Dodoma kujipanga ili kuendana na hali ya mahitaji ya sasa ikiwa ni mapoja na upimaji wa viwanja kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa.
Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma ilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutengeneza master plan na kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo zaidi ya ekari 260,000 za ardhi zimepimwa na na kupatiwa hati zinazomilikiwa na CDA, kufuatia kuvunjwa kwake na maelekezo ya Rais kuwa rasirimali zote ziwe chini ya Manispaa ya Dodoma ambayo itaendeleza shughuli zilizokuwa zikifanya na mamlaka hiyo kwa mujibu mtaratibu na sheria za nchi.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger