Moja ya matrekta ya
Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland likijaribiwa kuwashwa mara baada ya
kuunganishwa sehemu zake na Wataalam wa kuunganisha matrekta ya Ursus kutoka
Poland na Tanzania.
|
Wataalam wa
kuunganisha matrekta ya Ursus kutoka Poland na Tanzania wakiendelea na kazi ya
kuunganisha sehemu za matrekta hayo ndani ya kiwanda TAMCO lililoko Kibaha
Mkoani Pwani.
|
Matrekta ya Kampuni
ya Ursus SA ya nchini Poland yakiwa yamewekewa majembe yake tayari kwa kuanza
kufanya kazi ya kulima mashambani.
|
Matrekta ya Kampuni ya Ursus SA ya nchini Poland yakiwa yamewekewa namba za usajili za Tanzania tayari kuanza kufanya kazi ya kulima mashambani. |
(PICHA/HABARI NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
Mradi
wa matrekta aina ya Ursus ambayo yanatengenezwa na Kampuni ya Ursus SA iliyopo
nchini Poland yatawasaidia wakulima nchini kuondokana na adha ya kulima kwa
kutumia jembe la mkono na kuwaongezea mazao na kipato.
Hayo
yamesemwa hivi karibuni na Msimamizi wa Mradi wa Kuunganisha Matrekta hayo
katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha Mkoani Pwani, Mhandisi Adam Mbula wakati
alipokutana na Waandishi wa habari na kuwaeleza shughuli zinazofanywa katika
kiwanda hicho.
Mhandisi
Mbula amesema kwamba, mradi huo wa matrekta ni mradi unaotokana na mkopo wa
riba nafuu wa dola za Marekani milioni 55 uliotolewa na Serikali ya Poland kwa
ajili ya kuisaidia Tanzania katika kukuza uchumi hususani katika sekta ya
kilimo.
Amefafanua
kuwa, jumla ya matrekta 2,400 yanatarajiwa kuletwa katika kiwanda hicho na
kuunganishwa vipuri vyake ambapo kwa kuanzia kuna matrekta 2,004 na zana zake
200 yaani na majembe yake na jumla ya matrekta 35 yameshaunganishwa na zoezi la
uunganishaji linaendelea.
Amebainisha
kuwa, matrekta yanayounganishwa kiwandani hapo ni ya aina tatu yenye hosi pawa ya
50, 65, 75-85 kwakuwa kutakuwa na matrekta yenye 4x4 na 2x2 kiwandani hapo.
“Matrekta
yanayokuja hapa tunayaunganisha vitu vichache tu kama vile mfumo wa umeme,
mfumo wa mafuta, matairi, sehemu za kupoza injini kwakuwa tayari yameshafungwa
injini na transmisheni zake, lakini baadaye kitakapojengwa kiwanda rasmi, tutakuwa
tunafanya kila kitu hapa hapa na hii itaiwezesha Tanzania kujulikana”, alisema
Mhandisi Mbula.
Kuhusu
suala la upatikanaji wa masoko amesema kwamba, masoko yapo na tayari kuna
maeneo ambayo matrekta hayo yatakuwa yakipelekwa na vituo hivyo vitakuwa vinatoa
huduma ya mauzo ya matrekta na pia kuelimisha wakulima juu ya namna ya kutumia
matrekta hayo ambapo ameyataja maeneo hayo ni pamoja na Morogoro, Dodoma,
Njombe, Lindi, Katavi, Manyara na Nyanda za Kanda ya Ziwa ni Geita na Simiyu.
Aidha,
shughuli ya uunganishaji wa matrekta hayo imeanza tangu tarehe 22 Aprili, 2017
na amesema kwamba lengo ni kuyauza matrekta hayo ambapo bei bado haijatangazwa
kwakuwa kuna kitengo maalum kinachoshughulikia suala hilo na hapo baadaye itatangazwa
baada ya kujua gharama zilizotumika kuyakomboa matrekta hayo, lakini pia
amesema kwamba yatatolewa kwa wakulima kwa mkopo kwakuwa uwezo wao wa kuyanunua
ni mdogo.
Mhandisi
Mbula ameweka wazi kuwa mkopo huo unatarajiwa kurudishwa kutokana na mauzo ya
matrekta hayo ambapo kwa sasa Serikali imepewa muda wa miaka mitano (grace
period) ya kuanza kulipa mkopo huo.
Mradi
wa Matrekta ya Ursus SA ni Mradi wenye Mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na
Poland katika kusaidiana katika masuala ya kiuchumi hususani kilimo na
unahusisha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
SHARE
No comments:
Post a Comment