WANAWAKE wawili wameuawa kikatili kwa kushambuliwa na mashoka na waume
zao wa ndoa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoa wa Rukwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Polycarp Urio amethibitisha
kutokea kwa matukio hayo akisema chanzo ni wivu wa kimapenzi wa waume
zao.
Wanawake waliouawa ni Theresia Baltazar ambaye wakati wa uhai wake
alijulikana kwa jina lingine la Selemani (49) mkazi wa kijii cha Msia
kilichopo Bonde la Ziwa Rukwa, Sumbawanga. Theresia aliuawa kikatili kwa
kukatwa na shoka kichwani na shingoni na mumewe wa ndoa, Patrick
Kipesa(39). Kwa mujibu wa Kamanda Urio, tukio hilo lilitokea Mei 14
mwaka huu saa 1.30 asubuhi kijiji cha Msia kata ya Milepa, tarafa ya
Mtowisa, Sumbawanga.
“Baada ya mwanaume huyo kumuua mkewe kikatili naye alijiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani sebuleni kwake,” alisema.
Inadaiwa chanzo cha kufanya mauaji hayo na yeye kujiua ni wivu wa
kimapenzi baada ya kuhisi mkewe ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume
mwingine ambaye hajafahamika kwa majina.
Mwingine aliyeuawa ni Fatma Yusuph (22) mkazi wa Mtaa wa Sengetela Manispaa ya Sumbawanga.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda, Urio Fatuma ameuawa kwa kukatwa panga
shingoni na mzazi mwenzake aliyetoroka baada ya kutenda uhalifu huo na
jitihada za kumsaka sheria iweze kuchukua mkondo wake zinaendelea.
“Marehemu (Fatuma) alifika kituo cha Polisi kutoa taarifa ya kujeruhiwa
akiwa na hali mbaya ambapo alipewa PF3 ili akatibiwe ndipo mauti
ilimkuta akitibiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga”
alieleza Kamanda Urio.
Naye kikongwe Abel Sikazwe (90) aliyekuwa mgane kwa muda mrefu akiishi
peke yake kwenye nyumba yake, aliuawa kwa kupigwa kichwani na kitu
chenye ncha kali kisha kuvunjwa mkono na mguu kwa imani za kishirikina.
Taarifa za uhakika kutoka kijiji cha Muzi zinaeleza kuwa tangu enzi za
uhai wake marehemu Sikazwe alikuwa akihusishwa na ushirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Polycarp Urio amethibitisha
kutokea kwa matukio yote hayo ambapo alisema mtuhumiwa mmoja
anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano akihusishwa na mauaji ya
kikongwe Sikazwe.
Alisema marehemu Sikazwe aliuawa juzi akiwa amelala peke yake nyumbani
kwake ambapo watu hao baada ya kumuua, waliutelekeza mwili wake mbele ya
nyumba yake na kutokomea kusikojulikana.
Kaimu Ofisa Tarafa, Peter Mankambila alithibitisha kuwa kikongwe huyo
alikuwa akiishi peke yake baada ya kufiwa na mkewe miaka kadhaa
iliyopita.
“Mwili wa marehemu huyo uligunduliwa na mjukuu wake wa kike wakati
alipofika nyumbani kwake alfajiri kumsalimia. Ndugu wa marehemu
waliutaarifu uongozi wa kijiji,” alieleza.
Kamanda Urio alisema miili ya marehemu imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko.
IMEANDIKWA NA PETI SUMAYE MTANZANIA SUMBAWANGA
SHARE
No comments:
Post a Comment