Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma
Saadala akitoa ufafanuzi kwa Balozi mdogo wa China Zanzibar Bw. Xie Xiaowu juu
ya michoro na picha za waasisi mbali mbali wa vyama vya ukombozi duniani
zilizopo katika chumba cha historia alichofariki Mwasisi Mzee Abeid Amani
Karume Kisiwandui Zanzibar.
(PICHA NA
AFISI KUU ZANZIBAR).
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma
Saadala akizungumza na Balozi mdogo wa China Zanzibar Bw. Xie Xiaowu juu ya
masuala mbali mbali ya kimaendeleo huko Afisi Kuu Zanzibar.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Juma Abdalla
Saadala “Mabodi” amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kuenzi kwa
vitendo ushirikiano uliodumu zaidi ya karne moja baina ya chama hicho na Chama
Cha Ukombozi cha China (CPC).
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Balozi Mdogo
China Zanzibar Bw. Xie Xiaowu uliotembelea Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar.
Amesema ushirikiano uliopo baina ya vyama na serikali
za nchi hizo zimeimarika na kuzaa matunda yanayowanufaisha wananchi wa pande
zote mbili katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Dkt. Mabodi alieleza kwamba njia pekee ya kulinda
hazina hiyo ni kuwarithisha Vijana Elimu na ujuzi zitakazowasaidia kupata
uwezo wa kitaaluma wa kulinda urithi huo dhidi ya maadui na wapinga
maendeleo wa nchi hizo.
“ Ushirikiano baina ya CPC na CCM ni ya muda mrefu
hivyo sisi vizazi vya sasa ni lazima tujivunie huku tukiyalinda ili tuendele
kunufaika na fursa za nchi hizo.
Kwa upande wake Balozi Mdogo wa China Bw. XIE XIAOWU
ameahidi kwamba China itatoa ushirikiano wa Ari na Mali ili kuhakikisha
Zanzibar inakuwa nchi yenye nguvu kiuchumi na kijamii.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano
baina ya vyama hivyo na serikali zake ili viweze kutekeleza kwa ufanisi
mikakati ya kimaendeleo iliyoachwa na Viongozi Wakuu wa taasisi hizo toka enzi
za kusaka uhuru wa nchini hizo.
Sambamba na hayo Balozi huyo Bw. Xie Xiaowu alisifu
juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inayotokana na CCM kuwa zinaongeza ushawishi na nia ya China kuendelea kusaidia
sekta mbali mbali nchini ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Pamoja na Hayo alimpongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Mabodi kuwa ni kiongozi mchapakazi kutokana na kuwa karibu na
taasisi za kimataifa pamoja na wananchi kwa ujumla licha ya kuteuliwa kushika
nafasi hiyo kwa muda mfupi.
“ China inathamini juhudi mikakati mbali mbali
ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi kwa lengo la kutekeleza Ilani
ya Uchaguzi ya Chama Tawala, hivyo na sisi bado tuna nia na mikakati ya
muda mrefu ya kuwaunga mkono kupitia sekta za Afya, Elimu, Uvuvi na
Miundombinu”, alifafanua Balozi huyo wa China.
Baada ya ziara hiyo Ujumbe wa China ulitembelea sehemu
mbali mbali za makumbusho zikiwemo sehemu aliyouliwa aliyekuwa Rais wa Kwanza
wa Zanzibar na mwenyekiti wa balaza la mapinduzi Marehemu Mzee Abeid
Karume kisiwa ndui mjini zanzbar.
SHARE
No comments:
Post a Comment