Mwenyekiti wa Chama cha Watu
wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Nemes Temba (katikati) akisisitiza
jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino mapema hii leo
jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es
Salaam Bw.Gabriel Aluga na kushoto ni Afisa Mawasiliano na Habari wa
chama hicho Bw. Josephat Torner.
Afisa Mawasiliano na Habari wa
Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Josephat Torner
(katikati) akifafanua jambokwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
wakati akielezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya
ualbino mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa
chama hicho Taifa Bw. Nemes Temba na kushoto Mwekahazina wa chama hicho
Bw. Abdulah Omar.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS)
Bw. Nemes Temba (mwenye koto jeusi) wakati akielezea maadhimisho ya
siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi mapema hii leo jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Eliphace Marwa-MAELEZO)
…………………………
Na Husna Said na Nuru Juma- MAELEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino
yatakayofanyika Juni 13 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri mjini
Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar
es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania Nemes
Colman Temba alipokutana na waandishi wa habari.
Temba alisema maadhimisho ya mwaka
huu yanalenga kuibua mijadala na tafakuri kwa wadau juu ya ukusanyaji
endelevu wa takwimu,uchambuzi na upatikanaji wa watu wenye Ualbino kwa
wakati ili Serikali iweze kuwasajili, kuwahudumia na kuhakikisha kuwa
watu wenye ulemavu wa ngozi wanakuwa salama.
“Bila ya utaratibu mzuri wa
upatikanaji wa Takwimu Serikali haitaweza kupanga vyema juu ya ustawi wa
watu wenye ualbino, hivyo maadhimisho ya mwaka huu yataibua mjadala wa
umuhimu wa upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka ofisi ya Taifa ya
takwimu kwaajili ya kusaidia katika mipango ya maendeleo ya watu wenye
ualbino”,alisema Temba.
Aidha alisema Ofisi ya Taifa ya
Takwimu katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 iliyojumuisha
takwimu za watu wenye ualbino ilisaidia kubaini idadi ya watu hao ambapo
walikuwa 16,376 wakiwemo Wanaume 7,620 na Wanawake 8,756.
Mwenyekiti huyo alitumia fursa
hiyo kuishukuru Serikali ya Mh.Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusikiliza
na kutekeleza ombi la masuala ya watu wenye ulemavu kuhamishiwa ofisi
ya Waziri Mkuu kwani lilikuwa ombi la muda mrefu kwaajili ya ustawi wa
watu wenye ualbino na wenye ulemavu kwa ujumla.
Kwa upande wake afisa habari na
uhusiano wa wa chama hicho, Josephat Torner alisema kuwa, mauaji dhidi
ya watu wenye ualbino yamepungua kwa kiasi kikbwa kulingana na hapo
awali na mapambano dhidi ya vitendo hivyo bado yanaendelea licha ya
ukimya uliokuwepo kwa sasa.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu Takwimu na Tafiti kwa Ustawi wa Watu Wenye Ualbino
yatahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wadau toka Sweden,
Uholanzi, Marekani, Canada, Uingereza, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo na Mataifa mengine.
Siku hiyo ya kimataifa ya uelewa
juu ya Ualbino itatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo hamasa
kupitia vyombo vya habari,uendeshaji wa kliniki za ngozi kwa maalbino
pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria,midahalo na makongamano na
ukusanyaji wa takwimu za watu wenye ualbino.
SHARE
No comments:
Post a Comment